Prime
Misukosuko anayopitia Mdude Nyagali

Muktasari:
- Inadaiwa watu waliojitambulisha askari polisi wamevamia nyumbani kwake, wakampiga na kumkamata. Hata hivyo, Jeshi la Polisi limekanusha madai hayo.
Mbeya/Dar. Kwa mara ya sita tangu mwaka 2016, mwanaharakati Mdude Nyagali, amejikuta kwenye misukosuko, safari hii ikidaiwa watu waliojitambulisha askari polisi wamevamia nyumbani kwake, wakampiga na kumkamata.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga leo Ijumaa Mei 2, 2025 kupitia taarifa kwa umma amekanusha taarifa hizo zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikilihusisha Jeshi hilo na tukio la kuvamiwa na kupigwa Mdude.
Kwa mara kadhaa Mdude amejikuta mikononi mwa polisi akituhumiwa kwa uchochezi, pia amewahi kufikishwa mahakamani.
Kamanda Kuzaga amesema Jeshi la Polisi limepokea taarifa kutoka kwa Sije Emmanuel (31), mkazi wa Iwambi ambaye ni mke wa Mdude ikielezwa saa 8:00 usiku wa kuamkia leo Mei 2, 2025 wakiwa wamelala katika Mtaa wa Ivanga, Kata ya Iwambi, jijini Mbeya watu wasiofahamika waliwavamia kwa kuvunja mlango na kuingia ndani ambako walimjeruhi mume wake sehemu mbalimbali za mwili wake.
Amesema watu hao baada ya kutekeleza tukio hilo walitoweka naye kumpeleka kusikojulikana.
Kamanda Kuzaga amesema Polisi linaendelea na ufuatiliaji ili kumpata Mdude na kuwabaini waliohusika na tukio hilo kwa hatua zaidi za kisheria.
Ameiomba jamii kutoa ushirikiano kwa yeyote mwenye taarifa za mahali alipo Mdude na waliohusika na tukio hilo.
Awali, Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale alilitaka Jeshi la Polisi kueleza iwapo linamshikilia Mdude na kutaja kosa wanalomtuhumu kutenda.
Mbeyale alidai majirani wa Mdude walimweleza watu waliovunja mlango, kumshambulia na baadaye kuondoka naye walijitambulisha kuwa ni askari Polisi.
"Tunaendelea kufuatilia na baadaye kama chama tutatoa tamko kuhusu tukio hilo," amesema na kuongeza:
"Ukamataji wake haukufuata taratibu, kulikuwa na purukushani kubwa na damu ilimwagika. Zaidi ya hayo, hawakutoa taarifa yoyote kwa viongozi wa serikali ya mtaa ambako alikuwa akiishi," amesema.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi kupitia akaunti yake ya mitandao ya kijamii alieleza kuwa amepokea taarifa kuwa usiku wa kuamkia leo Polisi limefika nyumbani kwa mwanaharakati Mdude, wakavunja mlango, wakaingia ndani, wakampiga kwa kutumia vitu mbalimbali na kumsababishia majeraha kabla ya kuondoka naye.
“Hili ni tukio jingine linaloendeleza mfululizo wa vitendo vinavyolenga kuwadhulumu na kuwaumiza wale wanaoonekana kuwa wakosoaji wa Serikali, kinyume cha sheria na misingi ya haki za binadamu.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuhakikisha usalama wa Mdude Mpaluka Nyagali na kuhakikisha anapatiwa matibabu stahiki mara moja,” amesema.
Matukio mengine
Tukio hilo si la kwanza kwa Mdude, mwaka 2016 alikamatwa kwa tuhuma za uchochezi wilayani Mbozi mkoani Songwe, baadaye akahamishiwa Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.
Tukio kama hilo lilijirudia Novemba 1, 2017 alipokamatwa mkoani Songwe kwa tuhuma zinazofanana na za 2016 alihamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam alikokaa kwa siku 21 pasipo kupelekwa mahakamani.
Novemba 23, mwaka huohuo, Mdude alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mbozi, akituhumiwa kwa uchochezi.
Mwanaharakati huyo ambaye ni kada wa Chadema alidaiwa kutekwa kati ya Mei 4 hadi 9, mwaka 2019 akiwa katika ofisi yake Vwawa mkoani Songwe. Baadaye alipatikana katika Kijiji cha Makwenje mkoani Mbeya akiwa amejeruhiwa.
Juni 17, 2023 mwanaharakati huyo alikamatwa na Jeshi la Polisi kwa kushiriki maandamano kupinga mkataba wa uboreshaji na uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam kati ya DP World na Serikali.
Alikamatwa tena Julai 14, 2023, alipowasili jijini Dar es Salaam kufanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu mkataba huo wa bandari.