Prime
Kilio utekaji, watu kupotezwa chatua UN, Serikali kutoa tamko

Muktasari:
- Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Geneva, Balozi Abdallah Possi amesema msimamo wa kidiplomasia utatolewa kuanzia Jumatatu kwenye vikao vya Baraza la Haki za Binadamu.
Dar es Salaam. Wakati wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) wakiwasilisha kwa umoja huo masuala kuhusu matukio ya utekani na watu kutoweka nchini Tanzania, Serikali imesema msimamo wa kidiplomasia itautoa kwenye vikao vya Baraza la Haki za Binadamu.
Kupitia tovuti ya Umoja wa Mataifa jana Juni 13, 2025 imechapishwa taarifa ya wataalamu wa UN wakitoa wito kwa Serikali ya Tanzania kukomeshamatukio ya ‘kupotezwa’ wapinzani wa kisiasa, watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari, kama njia ya kuwanyamazisha kuelekea uchaguzi.
"Kuminya uhuru wa vyombo vya habari na waandishi na kuwatisha watetezi wa haki za binadamu ni jambo lisilokubalika. Tumeshtushwa na taarifa za mwenendo wa ukandamizaji kuelekea uchaguzi mkuu wa Tanzania Oktoba," imeeleza taarifa ya wataalamu hao.
Wito huo umetolewa ikielezwa ni kutokana na matukio ya kutoweka wanaharakati wa haki za binadamu na waandishi wa habari, Boniface Mwangi wa Kenya na Agather Atuhaire wa Uganda, jijini Dar es Salaam, Mei 19, 2025, ambao baadaye walipatikana kwenye mipaka ya nchi zao.
Wakati wengine wakizuiwa, Mwangi na Atuhaire waliingia Tanzania kufuatilia kesi dhidi ya kiongozi wa chama cha Chadema, Tundu Lissu anayestakiwa kwa uhaini na kuchapisha taarifa za uongo.
Imeelezwa wawili hao walikamatwa na polisi pasipo taarifa kutolewa na baadaye Mei 22, 2025, Mwangi alipatikana akiwa ametupwa Ukunda, mji wa pwani nchini Kenya, na siku moja baadaye Atuhaire aliachwa mpakani mwa Tanzania na Uganda. Wawili hao walidai waliteswa na kudhalilishwa kijinsia.
Hayo yakielezwa na wataalamu wa UN, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Geneva, Balozi Abdallah Possi amesema msimamo wa kidiplomasia kuhusu taarifa hiyo utatolewa kuanzia Jumatatu kwenye vikao vya Baraza la Haki za Binadamu.
“Sisi kama nchi tutatoa msimamo ndani ya siku chache zijazo, kuanzia Jumatatu tuna vikao vya haki za binadamu vinaanza, misimamo yetu tutaitoa pale, la sivyo chochote nitakachokisema sasa hakitakuwa rasmi,” amesema na kuongeza:
“Jumatatu kamishna wa haki za binadamu atatoa taarifa zake, hapo tutajua nini kinachoendelea na kama nchi msimamo wetu ni nini. Tunalifanyia kazi ndani ya hizi wiki mbili za mwisho, tutakuwa na kikao cha baraza la haki za binadamu kuna taarifa zihusuzo haki za binadamu Tanzania zitatoka.”
Katika hatua nyingine Balozi Possi amesema katika historia ya nchi, kwa sasa Tanzania ipo katika nafasi nzuri katika masuala ya haki za binadamu ikilinganishwa na awali.
Wataalamu wa UN katika taarifa yao wamedai: "Zaidi ya matukio 200 ya ‘kupotezwa’ yameripotiwa nchini Tanzania tangu mwaka 2019.”
“Kukamatwa kiholela, kuteswa na kutoweka kwa Mwangi na Atuhaire kunaashiria mkakati wa wazi wa kuzuia sauti za upinzani na kukwepa sheria na taratibu za haki," wameeleza.
Imeelezwa katika taarifa hiyo kuwa, viongozi wa upinzani na wafuasi wao wameripoti ongezeko la mashambulio na ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa katika maeneo yenye mvutano mkubwa wa kisiasa.
Ukiukwaji huo umeelezwa unajumuisha kukamatwa kiholela, unyanyasaji, mateso na kutoweka kwa viongozi vijana, watetezi wa haki za binadamu, na wanachama wa vyama vya upinzani.
“Ni wito kwa mamlaka za Tanzania kuchukua hatua za haraka kuacha kuficha taarifa za waliokamatwa kwa kuwa ni sawa na kuwapoteza. Pia zichunguze na kuwawajibisha wanaokiuka haki,” wamesema wataalamu hao na kuongeza:
“Serikali inapaswa kutoa haki na fidia kwa waathirika zikijumuisha huduma za matibabu, msaada wa kisaikolojia na kisheria, vyote vikizingatia jinsia kwa waathirika wa mateso na unyanyasaji wa kijinsia."
Kauli za ndani
Hayo yakielezwa na wataalamu wa UN, malalamiko kuhusu matukio kama hayo kimekuwa cha muda sasa, mathalan, Agosti 10, 2024 Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilitoa tamko kulaani ongezeko la matukio ya utekaji na watu kupotea nchini kikitoa orodha ya watu 83 waliofikwa na kadhia hiyo.
Mbali ya hayo, TLS ilimshauri Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume kuchunguza ushiriki wa Jeshi la Polisi kwenye matukio ya utekaji, ikielezwa limekuwa likituhumiwa kushiriki katika vitendo vya utekaji.
Si hivyo pekee, katika kipindi cha hivi karibuni baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wanahoji ukimya wa vyombo vya dola kuhusu hali hiyo wakitaka kufahamu nafasi ya vyombo hivyo katika kulinda amani na kusimamia haki kwa wote.
Juni 11, 2025, Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila alihoji suala hilo akitoa mfano kwamba kama zamani wauaji wa wenye ualbino na hata waliogushi vyeti walikuwa wanapatikana haraka, kwa nini wanaoua na kuteka watu sasa hawakamatwi.
Vilevile, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yuda Thadeus Ruwa’ichi katika tukio tofauti alisema ni muhimu kushughulikia mambo ya kitaifa kwa ukweli, haki na amani ili “tuweze kudai kweli kwamba sisi ni kisiwa cha amani”.
Alishauri Tanzania isijiite kisiwa cha amani kutokana na haya yanayoendelea, na wananchi wamuombe Mungu awape amani yake.
Wiki chache zilizopita, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alizungumzia masuala ya utekaji akieleza ni jambo linaloipa sifa mbaya nchi, huku akisema anaamini si vyombo vya dola vinavyofanya masuala ya utekaji, kwa kuwa vyenyewe vina uwezo wa kufanya mambo yake kwa weledi.
Si hao tu, hata Askofu Mkuu Renatus Nkwande alizungumzia masuala hayo kwenye ibada ya mazishi ya Mzee Silvin Mongella, akitoa ushuhuda alivyokuwa anafuatiliwa na gari fulani kwa umbali mrefu.
Vilio hivyo vinatokana na kutekwa na kupotea kwa watu mbalimbali akiwemo karibuni kabisa, Mdude Nyagali aliyefuatwa nyumbani kwake na kutekwa na hadi sasa hafahamiki alipo.
Wengine wa karibuni Mzee Ali Kibao aliyetekwa ndani basin a mwili wake ukapatikana siku iliyofuata ukiwa na majeraha na kumwagiwa tindikali, Shadrack Chaula aliyechukuliwa nyumbani kwao mkoani Mbeya pamoja na vijana watatu wa Temeke – Deusidedit Soka, Jacob Mlay na Frank Mbisa.
Hatua zinachukuliwa
Hata hivyo, kwa nyakati tofauti viongozi wa Serikali wamezungumzia kuhusu madai hayo ya matishio ya kiusalama yakiwamo matukio ya ama watu kutekwa au kuuawa na kutoa hakikisho la usalama.
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alitumia hotuba ya bajeti bungeni Juni 12, 2025 kuzungumzia hali hiyo kwa kina, akitoa hakikisho la vyombo vya dola kutuliza hali hiyo kama ambavyo vimekuwa vikifanya kwa awamu zote.
Akiangazia hali ya ulinzi na usalama nchini, Dk Mwigulu alisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama bado vina uwezo na nguvu ya kuhakikisha amani na utulivu nchini vinakuwepo, na haviwezi kushindwa kukabiliana na vitisho vinavyohatarisha maisha ya wananchi.
Julai 15, 2024 akiwa mkoani Simiyu, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Camillus Wambura alisema ni matukio ya utekaji na watu kujiteka yapo lakini Polisi wanapambana kuwakamata wahalifu na kuwaokoa wanaotekwa na hawahusiki na matukio hayo.
“Hatuhusiki na utekaji watu, sisi ni Jeshi ambalo linalinda usalama wa watu na mali zao, wanaoleta tuhuma za namna hiyo ni vitendo vya kutuvunjia adabu, matukio ya utekaji yaliyofanyika Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa na kuwakamata wahalifu na kuwaokoa wale waliotekwa,” alisema IGP Wambura.
Julai 3, 2024 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema Tanzania iko salama na vitendo vya utekaji havipaswi kukaliwa kimya.
"Baadhi ya wanasiasa wanaufanyia siasa uhalifu huu wa utekaji, nadhani mmesoma gazeti moja limeandikwa utekaji, taharuki kubwa inazushwa katika jamii, kwamba Tanzania kuna kutekwa tekwa hovyo, tena kunasibishwa na vyombo vyenye dhamana ya kulinda watu au Serikali. Nihakikishe tu Tanzania iko salama. Vyombo vinaendelea kuwatafuta kwa kuwa vina uwezo wa kuwakamata,” alisema.