Prime
Kauli ya CCM kuhusu Askofu Gwajima kuwania ubunge

Muktasari:
- Kuhusu mjadala unaoendelea kuhusu hatima ya ubunge wa Askofu Gwajima, CCM imetoa tamko la kuzima mijadala hiyo.
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, kimetoa kauli kuhusu Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima kama anaruhusiwa kugombea tena au lah!
Kauli ya CCM imekuja wakati ambao Askofu Gwajima yupo kwenye wimbi zito baada ya kanisa lake kufutwa.
CCM imesema kuwa anaruhusiwa kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania tena nafasi hiyo kupitia chama hicho.
Chama hicho tayari kimeshatangaza tarehe rasmi ya kuanza uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi ya ubunge na udiwani ndani ya chama hicho.
Akizungumza na Mwananchi jana Juni 11, 2025 baada ya kikao cha ndani, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Shaweji Mkumbura amesema uchukuaji fomu utaanza Juni 28 hadi Julai 2, 2025, kwa wanachama wote wenye nia, akiwemo Askofu Gwajima.
“Uchukuaji wa fomu ni haki ya kila mwanachama. Hata Gwajima mwenyewe ana haki kama wengine. Tunachotaka kuona ni ushiriki wa kidemokrasia. Tunaanza tarehe 28 Juni hadi Julai 2. Haya mambo yamewekwa wazi, hakuna cha kuficha,” amesema Mkumbura.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mjadala unaoendelea miongoni mwa wanachama wa chama hicho juu ya hatima ya Askofu Gwajima, hususan suala la kuchukua fomu ya kuwania tena nafasi hiyo pamoja na utekelezaji wa ahadi zake za mwaka 2020, Mkumbura amesema ni mengi yanayosemwa kumuhusu mbunge huyo.
Amekiri wapo baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wamehoji kutaka kujua iwapo anaruhusiwa kuchukua fomu na kama ametekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi wa jimbo hilo ambazo hazimo kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.
“Kwa kuwa hakuna maelekezo au taarifa yoyote kutoka kwenye uongozi wa juu kuhusu Gwajima, hatuwezi kumzuia kuchukua fomu atakapohitaji kufanya hivyo. Maamuzi mengine yataachwa kwa wahusika wenyewe yaani mamlaka,” amesema.
Akijibu swali la utekelezaji wa ahadi za mbunge huyo mwaka 2020, mwenyekiti huyo amesema zilikuwa za kwake binafsi (Gwajima) na hazikuwa sehemu ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Maswali haya yamekuja kufuatia kauli ya Gwajima, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), aliyoitoa Mei 25, 2025 katika mkutano na waandishi wa habari.
Gwajima alizungumzia masuala ya utekaji, huku akijitambulisha kama mjumbe wa NEC ya CCM mwenye uwezo wa kumfikishia ujumbe Mwenyekiti wa Taifa wa CCM (Rais, Samia Suluhu Hassan).
Pia alitoa mifano akihoji hali ingekuwaje ikiwa watu wa viongozi wakuu akiwemo Rais Samia wangetekwa kama wanavyotekwa watoto wa wengine.
Kauli hiyo ilizua mjadala mpana na katika mkutano mkuu wa CCM Rais Samia alitoa maelekezo kuhusu uteuzi, ambayo yalitafsiriwa kama yanamhusu mwanasiasa huyo.
“Tukitoa mwanya ndugu zangu, tukipitisha wanaotafuta tu na mie niwemo, ndio tunapata wale wanaokwenda huko. Chama kinakuwa Gwajimanised. Kwa hiyo kwa vyovyote vile tusi Gwajimanised chama chetu, Magwajima tuyaache nje.
“Hakuna kuoneana aibu wala haya,” alisisitiza Rais Samia kwenye mkutano mkuu wa CCM jijini Dodoma Mei 30, 2025.
Juni 1, 2025, wakati wa mahubiri katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Gwajima alisisitiza msimamo wake kuwa bado ni mwanachama hai wa CCM na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.
“Mimi hadi leo ni mwanachama wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu. Sitaki utekaji na narudia tena; sitaki watu kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha,” alisema Gwajima.
Siku iliyofuata Juni 2, 2025, Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa alitangaza kulifuta kanisa hilo linaloongozwa na Gwajima, akieleza kuwa limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na kuichonganisha Serikali na wananchi.
Hajaonekana jimboni
Alipoulizwa kama anawasiliana na mbunge huyo, mwenyekiti Mkumbura amesema licha ya kumtafuta kwa simu mara kadhaa, hajafanikiwa kumpata na wala hajaonekana bungeni.
Amesema mara ya mwisho walikutana Januari 18, 2025 kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM.
“Nimejaribu kumpigia simu Gwajima lakini hapokei. Hata nilipomuuliza mbunge mwenzake aliniambia hajamuona. Siwezi kusema amekimbia au amefungiwa, lakini tangu Januari hadi leo hajaonekana jimboni. Hajahudhuria mikutano ya chama, hatujapokea taarifa yoyote rasmi kutoka kwake. Hili ni jambo linalotufanya tujiulize maswali kadhaa yasiyo na majibu,” amesema mwenyekiti huyo wa CCM.
Amesisitiza kuwa chama kinafuatilia mwenendo wa kila mwanachama na uamuzi wa nani atapewa nafasi ya kugombea katika uchaguzi mkuu ujao, yatazingatia utendaji kazi, maadili na ushiriki wa karibu wa mwanachama.
Hata hivyo, katika mkutano mkuu wa CCM uliofanyika Mei 29-30, 2025 jijini Dodoma, Askofu Gwajima alikuwa miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, kuanzia Aprili 8, 2025, Bunge la bajeti lilianza jijini Dodoma na linaendelea mpaka sasa na huenda kutoonekana kwa Askofu Gwajima jimboni anakuwa bungeni.