Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utulivu watanda makanisa ya Askofu Gwajima

Muktasari:

  • Serikali imetangaza kulifuta Kanisa la Ufufuo na Uzima kwa kukiuka sheria ya Jumuiya Sura ya 337. Kwa mujibu wa Askofu Josephat Gwajima, makanisa hayo yapo zaidi ya 2,000 ndani na nje ya nchi.

Dar/mikoani. Siku moja baada ya Serikali ya Tanzania kutangaza kulifuta Kanisa la Ufufuo na Uzima, hali imekuwa tofauti katika makanisa hayo mikoani kwa kila mmoja kusema lake.

Uamuzi wa Serikali kulifuta kanisa hilo linalomilikiwa na Askofu Josephat Gwajima ni kile kilichoelezwa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa ni ukiukwaji wa Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

Msingi wa hayo ni mkutano wa Askofu Gwajima na waandishi wa habari, alioutumia kueleza anavyochukizwa na matukio ya kutoweka na kutekwa kwa watu huku akitoa mfano wa hali ingekuwaje iwapo matukio hayo yangewakuta watoto wa viongozi akiwemo yeye mwenyewe.

Kihampa alichukua uamuzi huo kwa kumwandikia barua Askofu Gwajima juu ya kufutwa kwa kanisa hilo na nakala kuituma kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura ili kusimamia utekelezaji wa agizo hilo.

“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 17(b) cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 kikisomwa pamoja na kifungu cha 39 cha Sheria Namba 3 ya mwaka 2019 kilichoifanyia marekebisho kifungu cha 2 cha Sheria ya Jumuiya.

“Nakujulisha kuwa nimefuta usajili wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, kuanzia leo (jana) Juni 02, 2025. Unatakiwa kusitisha shughuli za kanisa lako mara moja,” anaeleza Msajili kupitia barua hiyo.

Katika kanisa kuu lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam, tangu usiku wa kuamkia leo Jumanne, Juni 3, 2025, Polisi wamefika na kufunga utepe ili kuzuia mtu yeyote kuingia huku waumini wakiwa kandokando ya kanisa hilo.

Waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima lililopo Ubungo Dar es Salaam wakiwa wamekaa nje ya kanisa hilo baada ya kanisa lao kufutwa Juni 3, 2025.



Mwananchi limetembelea baadhi ya makanisa ya mikoani kuangalia kinachoendelea. Katika kanisa hilo lililopo eneo la soko la Maimoria, Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro limekuta hakuna kinachoendelea kanisani hapo huku kukiwa na hali ya utulivu.

Mwananchi limefikia kanisani hapo na kushuhudia utulivu huo huku kukiwa kumepangwa viti na baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa katika eneo hilo, wakidai katika kanisa hilo, maombi hufanyika kuanzia jioni Kila siku.

Hata hivyo, Mwananchi lilizungumza na baadhi ya waumini wa kanisa hilo ambao walikuwa wakiendelea na shughuli zao za kujipatia riziki nje kidogo ya kanisa hilo, ambapo walidai  wamezuiwa kuzungumza chochote kuhusiana na kinachoendelea.

Viti vikiwa vimepangwa ndani ya Kanisa la Askofu Gwajima, lililopo eneo la soko la Maimoria, Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.

"Kiongozi hamuwezi kumpata, kwani mna shida gani? sisi ni waandishi tuna shida naye, tumeambiwa tusizungumze chochote," amesema muumini huyo ambaye hakutaka kutaja Jina lake.

Hata hivyo, wakati anazungumza hayo walifika wenzake ambapo aliwanyooshea kidole kama ishara ya kuwafunga mdomo kutozungumza chochote kuhusiana na kinachoendelea.


..kufanya mkesha

Mkoani Tanga, baadhi ya viongozi wake wamesema hawana taarifa rasmi ya kufungiwa hivyo wanaendelea na ratiba za ibada zao kama kawaida.

Akizungumza na Mwananchi kwa sharti la kutokutajwa jina lake mmoja wa viongozi wa kanisa hilo amesema ni kweli wameona mtandaoni kanisa lao limefutwa, ila mpaka sasa hakuna taarifa rasmi iliyowafikia.

Muonekano wa Kanisa la Ufufuo na lililopo mkoani Tanga.

Amesema ratiba za ibada zao zitaendelea kama kawaida ambapo kwa leo Jumanne Juni 3,2025 watakuwa na ibada ya mkesha kuanzia saa 4:30 usiku katika kanisa lao la Tanga lililopo maeneo ya Gofu.

“Tumesikia kuhusu taarifa za kufungiwa kanisa letu ila mpaka sasa hatujapata maelekezo yoyote kutoka ngazi za juu kuwa kitu gani kinaendelea, kwani hatujapewa barua rasmi ya kufungiwa hivyo shughuli za ibada zinaendelea kama kawaida na leo saa 4:30 usiku tutakuwa na mkesha wa ibada,” amesema kiongozi huyo.

Mkazi wa Gofu jijini Tanga, Sophia Hussein ambaye anafanya biashara ya mama lishe kwenye eneo hilo,  amesema kwa siku ya jana Jumatatu hawakuona shughuli yoyote ikifanya licha ya kwamba ni siku yao ya kufanya mazoezi.

Amesema mara nyingi asubuhi na jioni wapo waumini hujitokeza hapo kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kwaya ila tangu kuanza vuguvugu hilo hawajaonekana tena zaidi ya viongozi wao pekee.


Kahama…

Katika kanisa hilo wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga baadhi ya waumini ambao hawakutaka kutajwa majina yao wanaoishi jirani na kanisa hilo wameiambia Mwananchi hakuna kinachoendelea kwa leo kanisani hapo na mpaka saa tano asubuhi, na askofu wa kanisa hilo waliyemtaja kwa jina moja la Askofu Amos hakuwa amefika.

Muonekano wa Kanisa la Ufufuo na lililopo mkoani Kahama.

"Hapa kanisani kwa leo hakuna kinachoendelea, labda kwa kuwa bado ni asubuhi. Pastor Amos hajafika bado sijajua atakuja saa ngapi, lakini kwa kawaida huwa anafika mchana mchana," amesema.

Kuhusu kutokuwepo kwa viti ndani ya kanisa hilo ambalo linaonekana kutokuwa na chochote ndani yake, waumini hao wamesema viti huwa vinawekwa sehemu nyingine kwa sababu za kiusalama kutokana na kanisa hilo kutokamilika.

Mwananchi imeshuhudia mazingira ya utulivu kanisani hapo, na alipojaribu kutafutwa kwa simu Askofu Amos hakupatikana kwa maana simu yake haikuwa hewani.