Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kila wiki mtu mmoja anakufa kwa ajali Mwanza

Muktasari:

  • Kwa kipindi cha Januari Mosi hadi Desemba, 2022 ajali 81 zimetokea mkoani Mwanza zilizosababisha vifo 71 na majeruhi 96.

Mwanza. Imeelezwa kuwa kwa mwaka 2022 ajali kubwa 81 zilitokea mkoani Mwanza na kusababisha vifo 71 na majeruhi 96.

Akizungumza leo Jumanne, Machi 14, 2023 kwenye maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani yanayofanyika Kitaifa viwanja vya Furahisha mkoani Mwanza, Mkuu wa mkoa huo, Adam Malima amesema kutokana na takwimu hizo wastani wa mtu mmoja na zaidi hufariki dunia kutokana na ajali kila wiki.

“Ndugu zangu hiki ni kiwango cha juu sana kwamba kwa kila wiki moja inatokea ajali kubwa ambayo inaondoa binadamu mmoja Mwanza, kwa wastani binadamu mmoja na zaidi,” amesema Malima

Amesema kwa upande wa pikipiki zimetokea ajali kubwa 30 kwa kipindi hicho cha Januari hadi Desemba, 2022 zilizosababisha vifo vya watu 25 na kujeruhi watu 26.

“Mwelekeo wa takwimu hizi sio mzuri kabisa na hivyo nina wataka watumiaji wote wa barabara katika Mkoa wa Mwanza kuzingatia kanuni na sheria za usalama barabarani ili kuweza kupunguza idadi hii ya majeruhi na vifo vya wananchi wenzetu.

“Chanzo kikubwa cha ajali za barabarani ni makosa ya kibinadamu, moja ni madereva kutokufuata sheria za usalama barabarani, nyingine ni mwendo kasi uliopitiliza ambao mara nyingi hauna sababu wala malengo ya huko anapoelekea.

“Nyingine ni madereva kuendesha magari wakiwa wamelewa au kuendesha kwa saa zilizopitiliza mfululizo mpaka usingizi unamchukua,” amesema Malima.

Amesema wapanda pikipiki nao hawavai kofia ngumu na kupakia abiria zaidi ya mmoja, maarufu kwa jina la mishikaki.

“Kwa hiyo ni imani yangu kwamba kwa elimu itakayotolewa katika kipindi hiki cha maadhimisho itakuwa ni chachu kwa madereva, wapanda pikipiki na makundi yote ya watumiaji barabara Mkoa wa Mwanza na maeneo mengine,” amesema.