Kikwete avuta wengi Sabasaba

Muktasari:
- Kiongozi huyo mstaafu leo ametembelea maonyesho ya kimataifa ya biashara maarufu Sabasaba
Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete leo Jumapili Julai 8, 2018 amevuta wengi katika maonyesho ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba baada ya wananchi wengi kumfuata kila banda alilokuwa akitembelea.
MCL Digital limeshuhudia baadhi ya wananchi, wakiacha kutembelea mabanda mbalimbali ya biashara na kumfuata rais huyo mstaafu.
Kiongozi huyo mstaafu leo ametembelea maonyesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jijini hapa.
Saa nane mchana Kikwete alikuwa kwenye banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), huku nje ya banda hilo kukiwa na idadi kubwa ya wananchi, wengi wakiwa na shauku ya kumuona.
Hali ilikuwa hivyo katika kila banda alilotembelea, licha ya wananchi hao kuzuiwa na askari walizidi kuongezeka kadri kiongozi huyo mstaafu alivyokuwa akitembelea maeneo mbalimbali.
“Baba tumekukumbuka uko wapi baba,” walisikika wakisema baadhi ya wananchi hao.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Kikwete ameishauri Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuwawezesha wafanyabiashara kupenya katika soko la kimataifa.
“Ni jukumu lao kuwasaidia wafanyabiashara kufikia soko la kimataifa kwa sababu biashara ni nzuri na zina ubora,” amesema.
Aliwataka wafanyabiashara wa ndani kujifunza kwa wafanyabiashara waliopiga hatua zaidi.