Kikwete atua Sabasaba, awashauri wafanyabiashara

Rais Mstaafu ,Jakaya Kikwete akizungumza na Mtu mwenye ulemavu, Abdul Kipara ambaye ni fundi wa kushona nguo alipotembelea banda la VETA wakati wa maonyesho ya 43 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaa yanayoendelea katika viwanja vya JK Nyerere barabara ya Kilwa. Picha na Anthony Siame
Muktasari:
- Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameungana na Watanzania katika maonyesho ya 43 ya kimataifa ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya Julius Nyerere kandokando ya barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam
Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameungana na Watanzania katika maonyesho ya 43 ya kimataifa ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya Julius Nyerere kandokando ya barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Kikwete amefika katika maonyesho hayo leo Jumamosi Julai 6, 2019 na kutembelea mabanda mbalimbali.
Katika banda la Jeshi la Magereza lenye samani na viatu alishauri jeshi hilo kuzalisha bidhaa zenye viwango vya kimataifa.
“Kazi nzuri lakini msiangalie tu viwango vya ndani mnatakiwa kufikisha viwango vya kimataifa ili na sisi tuweze kutambulika kimataifa,” amesema.
Kikwete pia alitembelea banda la mbegu za mazao mbalimbali, akiwa katika banda la mbegu za mahindi ameshauri wauzaji hao kutumia majina ya mbegu yenye mvuto.
“Mbadilishe haya majini, kama hapa naona majina ya Tumbili, Simba, Twiga wakati mwingine mkulima ataogopa kununua kutokana na haya majina,” amesema Kikwete.
Rais huyo wa Awamu ya Nne amewapongeza wafanyabiashara hao wa ubora wa mbegu zao.