Kikokotoo ngoma bado mbichi, wabunge waliamsha

Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi.
Muktasari:
- Licha ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kutoa nafasi chache kwa wabunge waliotaka kuuliza kuhusu kikokotoo, wabunge wengi zaidi walisimama kwenye swali hilo ili wawaulize maswali ya nyongeza.
Dodoma. Unaweza kusema kuwa sakata la kikokotoo kwa watumishi wanapostaafu bado halijapoa, hii ni baada ya baadhi ya wabunge kutaka sheria ya suala hilo kupelekwa bungeni wakidai watumishi bado hawajalidhika na jambo hilo.
Katika kipindi cha maswali na majibu bungeni leo Jumanne Agosti 29, 2023, idadi kubwa ya wabunge walisimama kuuliza maswali ya nyongeza, wakilalamika kuhusu kikokotoo hicho.
Swali la msingi limeulizwa na Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscus Tarimo, aliyehoji nini mpango wa Serikali kuhusu malalamiko ya wastaafu juu ya kikokotoo kinachotumika katika upigaji wa mahesabu ili waweze kulipya mafao yao.
Mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni, amehoji lini Serikali itapeleka bungeni sheria inayohusiana na kikokotoo hicho ili wakakifute kwa madai watumishi hawakitaki.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi, amesema, Serikali ilitangaza matumizi ya kanuni mpya ya mafao (Kikokotoo) ya pensheni kuanzia Julai 1, 2022 kupitia Gazeti la Serikali Namba 357 toleo la Mei 20, 2022.
Amesema kanuni hiyo iliandaliwa kwa kuzingatia haja ya kuboresha na kuwianisha mafao ya wanachama na kuifanya mifuko ya pensheni kuwa endelevu.
"Mpango wa Serikali ni kuendelea kuwaelimisha wananchi hususani waajiri na wanachama wa mifuko ya pensheni wakiwemo wastaafu kuhusu faida ya kanuni mpya ya mafao ya pensheni," amesema Katambi.
Naibu Waziri huypo amesema Serikali kupitia mifuko hiyo, na kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), imejipanga na inaendelea kutoa elimu ya kanuni hiyo ambapo hadi kufikia Juni 30, 2023, mifuko iliweza kutoa elimu kwa jumla ya waajiri 5,580 (PSSSF 362 na NSSF 5,218) kati ya waajiri 6,200 waliopangwa kufikiwa kipindi hicho.
Aidha Naibu Waziri Katambi amesema wanachama 131,497 (PSSSF 35,133 na NSSF 96,364) walifikiwa na mafunzo hayo.
Kuhusu watumishi kwamba hawakitaki kikokotoo, amewataka wanaotoa kauli hiyo kufanya utafiti kabla ya kusema kwani watumishi wanafurahia utaratibu huo.