Dk Nchimbi asema urithi wa hayati Mkapa unaendelea kuibeba afya ya Taifa
Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi akiwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Hussein Mwinyi katika mkutano wa nne wa kumbukumbu ya mafanikio ya hayati Rais Mkapa (Mkapa Legacy Summi)
Muktasari:
- Makamu wa Rais Dk Emmanuel Nchimbi amesema urithi wa hayati Benjamin Mkapa unaendelea kupitia taasisi alizoanzisha, akisisitiza uwekezaji katika rasilimali watu, teknolojia na mifumo imara ya afya kuboresha huduma nchini.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi amesema baada ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu, hayati Benjamin Mkapa, urithi wake bado unaendelea kuonekana kupitia taasisi alizozianzisha, huku akitaja sekta ya afya kuwa miongoni mwa maeneo yaliyonufaika zaidi.
Amesema hayati Rais Mkapa aliamini kujenga taasisi imara na alitumia muda, nguvu na jitihada kuhakikisha zinaendelezwa kwa manufaa ya Watanzania.
Dk Nchimbi ametoa kauli hiyo leo Julai 16, 2026 Dar es Salaam wakati akizungumza katika mkutano wa nne wa kumbukumbu ya mafanikio ya hayati Rais Mkapa (Mkapa Legacy Summi) ulioambatana na maadhimisho ya miaka 20 ya Taasisi ya Benjamin Mkapa.
Mkapa, alifariki dunia usiku wa kuamkia Julai 24, 2020, na akazikwa kwa heshima za kitaifa Julai 29, 2020 katika Kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.
Dk Nchimbi amesema mafanikio ya Taasisi ya Benjamin Mkapa ni ushahidi kwamba, maono ya Mkapa ya kujenga taasisi imara yameendelea kuzaa matunda hata baada ya kuondoka kwake.
“Ushahidi unaonesha taasisi nyingi zilizoasisiwa katika uongozi wa Rais Mkapa bado zinaendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ikiwamo Benjamin Mkapa Foundation ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kuboresha huduma za afya,” amesema Dk Nchimbi.
Amesema taasisi hiyo iliyoanzishwa kusaidia mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), sasa imepanua wigo wake kwa kuimarisha mifumo ya afya nchini, ikiwamo kujenga nyumba za watumishi wa afya katika maeneo yenye uhaba wa wataalamu ili kuwavutia na kuwabakiza kazini.
Dk Nchimbi amesema uwekezaji katika rasilimali watu ni msingi wa mifumo imara ya afya, akisisitiza maendeleo ya sekta hiyo yanahitaji viongozi wenye ujuzi, mafunzo na malezi ya kitaaluma yanayokwenda sambamba na mabadiliko ya dunia.
“Uongozi wa afya ni taaluma yenye maarifa na ujuzi wa kipekee unaojengwa kupitia mafunzo, uzoefu na 'mentorship' (ulezi wa kitaaluma), ni muhimu viongozi kuelewa uhusiano kati ya afya, uchumi, siasa na utamaduni,” amesema.
Akizungumzia mustakabali wa sekta hiyo, Dk Nchimbi amewataka vijana kutumia teknolojia mpya, ikiwamo akili unde (AI), tiba kwa njia ya mitandao na uchambuzi wa takwimu ili kuongeza ubora wa huduma za afya.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Hussein Mwinyi amesema mafanikio ya Taasisi ya Benjamin Mkapa yanaonesha umuhimu wa taasisi imara katika kuendeleza ajenda ya afya barani Afrika.
Amesema mchango wa taasisi hiyo umeonekana kupitia uimarishaji wa mifumo ya afya, kuendeleza wataalamu wa sekta hiyo na kuboresha huduma za afya ya msingi, hatua ambazo zimeongeza uwezo wa sekta ya afya kukabiliana na changamoto zinazoibuka.
"Urithi wa hayati Benjamin Mkapa haupaswi kubaki kwenye historia pekee, bali uendelee kuishi kupitia uwekezaji katika vijana, uongozi bora na mifumo madhubuti ya afya," amesema.
"Serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi waendelee kushirikiana ili kujenga Afrika yenye wananchi wenye afya, mifumo imara ya huduma za afya na viongozi watakaoendeleza maono ya maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho," amesema.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi amesema mifumo imara ya afya inategemea uwepo wa watumishi wenye ujuzi na uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazolikabili Bara la Afrika, ikiwamo ongezeko la mahitaji ya huduma za afya, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya teknolojia.
Amesema kwa kipindi cha miaka 20, Taasisi ya Benjamin Mkapa imekuwa mshirika wa kimkakati anayeaminika na Serikali katika kuendeleza rasilimali watu kwenye sekta hiyo.
Amesema takribani watumishi 19,000 wamenufaika kupitia programu mbalimbali za taasisi hiyo, ikiwamo uboreshaji wa huduma za afya nchini.
"Mkutano wa rasilimali watu wa afya Afrika unaonesha umuhimu wa kuendeleza dhamira ya kisiasa, uwekezaji wa ndani na kuwapa vijana nafasi ya kushiriki katika kuleta maendeleo ya sekta ya afya, huku Tanzania ikiendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika safari hiyo ya mageuzi," amesema.