Prime
Kesho kicheko, maumivu

Muktasari:
- Juni 24, 2025, Bunge lilipitisha bajeti ya Sh56.49 trilioni katika mwaka 2025/26. Bajeti hiyo inayoanza kutekelezwa kesho, inang’ata na kupuuliza kwa wafanyabiashara na bodaboda
Dodoma. Mwaka mpya wa Serikali wa 2025/26 unaanza kesho Jumanne, Julai mosi, 2025 kwa bodaboda na wafanyabiashara kufurahia punguzo la tozo, ada huku wanywaji wa vilevi, wachezaji wa michezo ya kubashiri wakianza kuonja joto la kupanda kwa ushuru.
Juni 24, 2025, Bunge lilipitisha bajeti ya Sh56.49 trilioni katika mwaka 2025/26.
Bajeti hiyo inayoanza kutekelezwa kesho, inang’ata na kupuliza kwa wafanyabiashara na bodaboda ambao wameondolewa baadhi ya kodi na tozo.
Kwa bodaboda ni kicheko baada ya Serikali kupunguza ada ya usajili wa pikipiki za biashara kutoka Sh340,000 hadi Sh170,000 kwa miaka mitatu.
Pia, Serikali imefuta kodi ya mapato kwa mwaka inayolipwa kwa utaratibu wa ‘presumptive tax’ badala yake imeanzisha mfumo wa ulipaji wa mara moja wa ada pamoja na ‘presumptive tax’ kwa Sh20,000 badala ya Sh290,000.
Pia, bodaboda wamepunguziwa ada ya leseni ya uendeshaji wa pikipiki, bajaji na guta kutoka Sh70,000 hadi Sh30,000.
Pia, mamlaka za utoaji wa leseni zikiwamo halmashauri zimeondolewa uwezo wa kufunga biashara pale mfanyabiashara anapokiuka taratibu.
Bunge pia limeweka sharti la waziri mwenye dhamana na biashara, kuidhinisha biashara ambazo hazipaswi kufanywa na raia wa kigeni.
Serikali imepunguza kiwango cha ada ya ushuru wa hoteli kutoka asilimia 10 hadi asilimia 2 na kuweka kiwango mfuto cha ushuru wa huduma cha asilimia 0.25.
Hata hivyo, bajeti hiyo, imeng’ata kwa kuongeza Sh1,000 katika tozo inayotozwa kwa kila abiria anayesafiri wa ndege na Sh500 kwa abiria wa usafiri wa treni.
Pia, Serikali inaanza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye aisikrimu (ice cream) zinazotengezwa nchini kwa kutumia kakao au malighafi nyingine na ushuru wa bidhaa wa Sh134.2 kwa kila lita kwenye vinywaji vya kuongeza nguvu.
Aidha, kuna ongezeko la ushuru wa bidhaa kwa Sh10, 15 na 25 kwenye lita ya bia, mvinyo na vinywaji vikali mtawalia.
Serikali imeongeza kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye zawadi ya ushindi kwenye michezo ya kubashiri matokeo kutoka asilimia 10 hadi 12 na michezo ya kasino ya ardhini kutoka asilimia 12 hadi 13.
Pia, tozo ya ongezeko la Sh10 itakayotozwa kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli itaanza kukatwa ili kugharamia Bima ya Afya kwa Wote.
Vilevile kuanzia kesho, kutakuwa na mgawanyo wa asilimia 91 ya mapato yatokanayo na huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Asilimia 51 itawekwa katika akaunti ya taasisi hiyo iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na asilimia 40 itawekwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Sheria ya Fedha inaeleza Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro itaweka mgawanyo wa asilimia 91 ya mapato yatokanayo na huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alipowasilisha Muswada wa Sheria ya Fedha uliopitishwa, alisema asilimia 51 itawekwa katika akaunti ya mamlaka hiyo iliyopo BoT na asilimia 40 itawekwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Wananchi wachekelea
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 30 2025, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Lutengano Mwinuko amesema mambo mengi yalikwenda sawa kutokana na wabunge kuwa na mamlaka ya kujadili na kushauri kuhusu bajeti.
“Ninaamini mambo yaliyopangwa yatakwenda kama yalivyopitishwa, ila jambo la msingi ni kuhakikisha fedha zilizopangwa zinapatikana na kufika katika maeneo husika ya vipaumbele na kutekelezwa,” amesema.
Mwinuko amesema jambo kubwa katika utekelezaji wa bajeti ni kuhakikisha mambo yaliyopangwa katika kipindi cha robo mwaka yanayogusa Taifa ikiwamo maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, yanafanyika.
“Ninaamini kuwa, eneo hili litapewa kipaumbele kikubwa ili tuweze kuwa na kipindi kizuri cha maandalizi, mwishoni tuje kuwa na uchaguzi ambao ni wa amani, kwa hiyo kubwa ni hilo maeneo yaliyowekewa kipaumbele yaweze kuangaziwa,”amesema Dk Mwinuka ambaye ni mchumi kitaaluma.
Mmoja wa madereva bodaboda Dodoma, Alex Musa amepongeza Bunge kwa kupitisha bajeti hiyo kwa kuwa inakwenda kutoa nafuu ya tozo na kodi kwa bodaboda kwa sababu ilikuwa kubwa.
“Miongoni mwa vitu ambavyo vimekuwa vikituumiza ni hiyo ada ya leseni tuliyokuwa tukilipa Sh70, 000 na hii itaongeza idadi kubwa ya watu watakaohakikisha wanakuwa na leseni. Hii ilikuwa ni miongoni mwa kilio kikubwa sana kwetu,”amesema.
Katibu wa Ushirika wa Wakulima wa Zabibu Mpunguzi mkoani Dodoma, Emmanuel Temba amesema ahueni kwa bajeti hiyo ni kutofungiwa biashara hata kama kuna mazingira ambayo hayajakaa sawa.
“Sasa hivi (mamlaka za kodi) wamekuwa rafiki kwa wafanyabiashara kwa hiyo hata kama kuna changamoto imetokea ambayo zamani walikuwa wanafungia biashara, lakini sasa hawafanyi hivyo,” amesema.
“Sasa kuna mwanya ambao mnaweza kukaa na kujadiliana lakini kama kulikuwa na deni fulani wanaweza kugawanya ukalipa kidogo kidogo ukaendelea kufanya biashara, kwa hilo tunaipongeza Serikali,” amesema Temba.
Pia, amesema bajeti iko vizuri lakini kwa wao ambao wako katika sekta ya mvinyo bado wanaona kodi ni nyingi sana.
Mfanyabiashara maarufu jijini Dodoma, Peter Olomi amesema bajeti hiyo imeonekana kuwajali wafanyabiashara kwa kuwa maeneo mengi waliyokuwa wakililia yamerekebishwa kwa kufanyiwa kazi.
“Kuna kodi moja ya hotel levy (ushuru wa hoteli) tulikuwa tunaipigia kelele imepungua kutoka asilimia10 hadi asilimia 2 kwa watu wa hoteli ni habari njema sana. Hakukuwa na ushindani mkubwa katika ku-defend (kujitetea) kwa sababu ni bajeti ya mwisho ya uchaguzi,”amesema Olomi.
Olumi amesema bajeti inapowajali bodaboda, wakulima na wafanyabiashara, hakuna cha kupinga bali ni bajeti nzuri ambayo imegusa kwenye maeneo yote.
Mkazi wa Msalato, Hashim Said amesema michezo ya kubahatisha na vilevi kuongezewa kodi ni sawa kwa sababu sio jambo la lazima kwa binadamu lakini hili la petroli linaweza kuongeza gharama za usafiri ikaleta changamoto kwa wananchi wengi.
“Sioni kama ina tabu sana kwa kuwa, vitu kama hivyo (vilevi) si lazima kwa binadamu, mtu mwenyewe anahiari ya kwenda kunywa au asinywe. Lakini pia imeelezwa fedha zinakwenda katika Bima ya Afya kwa Wote, afya ni hitaji la kila mtu,”amesema Said.