Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kishindo cha Samia

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amelihutibia Bunge la 12 akihitimisha shughuli zake, asema atavunja Agosti 3, 2025.

Dar/Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amelihutubia Bunge la 12 akihitimisha shughuli zake kwa kuzungumzia mambo mbalimbali yaliyotekelezwa na Serikali yake, yakiwamo yanayohusu Uchaguzi Mkuu, Katiba mpya na maendeleo ya kiuchumi.  

Samia katika hotuba ya leo Juni 27, 2025 iliyodumu kwa saa 2: 47 ametoa maelekezo kuhusu matukio ya watu kupotea na deni la Serikali. Ameanza hotuba saa 11:32 jioni hadi saa 2:19 usiku.

Rais Samia amehitimisha hotuba akiweka bayana kuwa Bunge litavunjwa rasmi Agosti 3, 2025.

“Baada ya kusema hayo na kwa mamlaka niliyonayo chini ya ibara ya 90(2) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, ninayo heshima kutamka kwamba shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimehitimishwa na Bunge litavunjwa rasmi, Agosti 3, mwaka huu,” amesema.


Katiba Mpya

Samia amewahakikishia Watanzania kuwa suala la Katiba mpya linakwenda kufanyiwa kazi ndani ya miaka mitano ijayo.

Amesema kwa kuwa suala la Katiba ni pendekezo la muda mrefu la tume ya maridhiano, pendekezo hilo litafanyiwa kazi kama inavyoelekezwa na Ilani ya CCM.

“Kwa msingi huo, mchakato wa Katiba mpya ni miongoni mwa ahadi zinazoonekana katika Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030. Hivyo ni kusema kwamba, shughuli ya kuanza kufanya Katiba mpya itatekelezwa katika kipindi kijacho cha miaka mitano,” amesema.

Mchakato wa Katiba mpya uliokwama mwaka 2014, ulianza mwaka 2011 kwa utungwaji wa sheria za kuratibu na kusimamia utekelezaji wa upatikanaji wake.

Sheria hizo ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Namba 83/2011 iliyoelekeza kuundwa vyombo vya kuratibu mchakato wa Katiba – Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mabaraza ya Katiba na Bunge Maalumu la Katiba (BMK) na Sheria ya Kura ya Maoni Namba 11/2013.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba iliratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Kwanza ya Katiba iliyohaririwa na Mabaraza ya Katiba na kupata Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa kwenye BMK.

Katika Bunge hilo ambalo licha ya mvutano wa kiitikadi wa wajumbe uliosababisha baadhi ya wajumbe kususia majadiliano na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lilijadili na Oktoba 2, 2014 lilipitisha Katiba Inayopendekezwa.

Oktoba 8, 2014, aliyekuwa mwenyekiti wa BMK, hayati Samuel Sitta aliikabidhi Katiba Inayopendekezwa kwa Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete. Hata hivyo, Aprili 2, 2015 ilitangazwa kuahirishwa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa kutokana muda kubaki mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Kutokana na hali hiyo vuguvugu la kudai katiba mpya liliendelea lakini Serikali ya awamu ya tano ilieleza halikuwa kipaumbele chake, hadi lilipoibuliwa kwenye awamu ya sita.


Uchaguzi Mkuu

Rais Samia amezungumaia mabadiliko yaliyofanywa kwenye sheria za uchaguzi, akisema kuundwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kumejibu hoja za wadau wa siasa waliokuwa wakiitaka kwa muda mrefu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akihutubia na kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe Juni, 27,2025.

Amesema hatua hiyo imetokana na mapendekezo ya wadau wa demokrasia kupitia Kikosi Kazi alichokiunda, kilichokusanya maoni ya wadau wa makundi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iliundwa kwa sheria yake yenyewe. Tulifanya hivi ili kujibu rai ya muda mrefu ya wadau wa kisiasa,” amesema.

Amesema miongoni mwa maboresho yaliyofanyika katika Sheria ya Uchaguzi ni pamoja kuongeza takwa la mgombea kupigiwa kura ya ‘Hapana’ hata kama yupo peke yake.

“Hatua hii inafuta kilichojulikana kama anapita bila kupingwa,” amesema.

Rais Samia amesema hivi karibuni INEC itatangaza tarehe ya Uchaguzi Mkuu baada ya kukamilika kwa uandikishaji wapigakura na kwamba, anatarajia Tume itawatangaza pia wapigakura.


Agizo kwa Polisi

Akizungumzia utendaji wa Jeshi la Polisi, mbali na kulipongeza kwa shughuli linazofanya, Rais Samia, bila kufafanua, amelitaka jeshi hilo kuongeza jitihada kukomesha matukio ya watu kupotea, yanayoripotiwa sehemu mbalimbali nchini.

Amesema Serikali imeendelea kuliimarisha jeshi hilo kwa kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza miundombinu, akieleza vituo vya polisi 472 vimejengwa hadi ngazi ya kata na shehia.

Rais Samia Suluhu Hassan akilihutubia bunge kabla ya kulivunja Bunge la 12, jijini Dodoma leo Juni 27, 2025. Picha na Edwin Mjwahuzi

“Kasi ya kuwabaini wahalifu na kuwafikisha mahakamani imeongezeka, jambo ambalo hatujafanikiwa vya kutosha ni ajali za barabarani, lazima nazo tuendelee kufanyia kazi,” amesema na kuongeza:

“Nalielekeza Jeshi la Polisi kuongeza jitihada katika kukomesha matukio ya watu kupotea.”

Amesema Serikali imeboresha makazi ya askari na vitendea kazi, ikiwamo magari na pikipiki kwa ajili ya kazi za utawala na operesheni. Aidha, askari 16,000 wameajiriwa huku maofisa na wakaguzi 13,633 wakipandishwa vyeo.

“Natoa pongezi nyingi kwa Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya. Hatuna budi kutambua kwamba, uhalifu unaozuiliwa kwa jitihada za Jeshi la Polisi ni mkubwa kuliko unaofanyika,” amesema.

Kuhusu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amesema uimara na usalama wa mipaka ya Taifa ni matokeo ya jeshi hilo kutimiza jukumu lake la kulinda uhuru na mipaka ya nchi.

“Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limetimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, katika kipindi hiki tumewekeza sana kuliimarisha kwa vifaa, zana za kisasa na mafunzo,” amesema.

Samia ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu amesema weledi na nidhamu ya wanajeshi ni ya hali ya juu na ya kupigiwa mfano.

Amesema Serikali imejenga nyumba mpya za makazi ya wanajeshi 6,064 na kulifanya jeshi hilo kushiriki ipasavyo katika shughuli za kitaifa na kimataifa.

“Hii ikiwemo ulinzi wa rasilimali, miradi ya kimkakati na operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa,” amesema.


Falsafa ya 4R

Amesema alipoingia madarakani aliona haja ya kuhakikisha wanaendelea kujenga Taifa la maelewano na maridhiano ili kwenda pamoja katika mwelekeo wa maendeleo.

“Dhima hii ilinisukuma kubuni na kutekeleza falsafa ya 4R, tukiongozwa na falsafa hiyo ilituelekeza kwenye mageuzi, maridhiano, ustamihilivu na kujenga upya.

“Tuliweza kuwaleta wadau wa kisiasa na wengine pamoja na kufanya uamuzi na maboresho mbalimbali yaliyojumuisha na kushirikisha wadau wote.”

Samia amesema Serikali iliunda Tume ya Maridhiano iliyofanya kazi nzuri ya kuja na mapendekezo ya muda mrefu na mfupi.

“Katika kutekeleza mapendekezo ya tume, Serikali iliondoa zuio la mikutano kwa vyama vya siasa na wote tumeshuhudia vyama vikiendelea kufanya shughuli zao kwa uhuru, ikiwemo mikutano ya hadhara,” amesema.

Vilevile, Baraza la Vyama vya Siasa limefanya mikutano sita na kutoa mawazo na ushauri uliowasilishwa serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

 Amesema kutokana na mashauriano hayo yaliyohusisha wadau wote, Bunge lilitunga sheria ya INEC ya mwaka 2024, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.

Amesema Serikali imeendelea kuimarisha uendeshaji wa shughuli za vyama vya siasa na hadi Juni 2025, Serikali imetoa ruzuku ya Sh87.87 bilioni kwa vyama vinavyostahili.

Kuhusu Muungano, amesema ufumbuzi wa hoja 15 umeongeza imani ya Watanzania kwa Serikali.

“Pamoja na hayo niwaase Watanzania wenzangu tuendelee kushikamana na kuwa makini na vitisho vyovyote dhidi ya Muungano wetu. Niwasihi pia kuendeleza utulivu na amani vitu ambavyo ni sifa njema kwa nchi yetu,” amesema.


Hali ya uchumi

Hotuba hiyo haikuacha kuzungumzia uchumi, amesema wakati uchumi wa dunia ukitarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 2.3 mwaka 2025, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), linakadiria kasi ya ukuaji uchumi Tanzania itafikia asilimia sita.

Amesema pato ghafi la Taifa limeongezeka kutoka Sh156.4 mwaka 2021 hadi Sh205.84 trilioni mwaka 2024 na pato la wastani la Mtanzania limeongezeka kutoka Sh2.36 milioni mwaka 2020 hadi Sh2.93 milioni mwaka 2024 na shilingi imeimarika.

Kiashiria kingine cha utulivu wa uchumi, amesema ni mfumuko wa bei aliosema umeendelea kuwa chini ya asilimia tano ndani ya miaka minne na kwamba ni kiwango bora Afrika Mashariki na chini ya wastani wa mfumuko wa bei ulioshuhudiwa Afrika.

Amesema hali hiyo inatokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti, uhakika wa upatikanaji wa chakula katika masoko ya ndani kutokana na kukuza tija katika uzalishaji chakula.

Kuhusu deni, amesema hadi Mei mwaka 2025, deni la Serikali lilifikia Sh107.7 trilioni, kati ya hilo la nje ni Sh72.94 trilioni na ndani ni Sh34.76 trilioni.

Kuongezeka kwa deni hilo amesema kumetokana na kupokelewa kwa fedha za mikopo mipya na ya zamani ambayo mikataba yake iliingiwa na Serikali za awamu za nyuma kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Ni vema tukafahamu kuwa mkopo unaweza kusainiwa leo, lakini fedha husika zikaanza kupokewa baada ya maandalizi ya mradi kukamilika au mradi kuanza. Hivyo ili liwe deni au mkopo uingie kwenye deni la Serikali ni lazima Serikali iwe imepokea fedha hizo, huduma au vifaa tulivyokubaliana,” amesema.

Amesema Serikali pamoja na kusaini mikopo mipya, imeendelea kupokea fedha za mikopo iliyosainiwa katika vipindi tofauti na kuongeza kiasi cha deni la Serikali.

“Kwa mfano awamu ya sita imepokea kiasi cha Sh11.3 trilioni ikiwa ni mikopo iliyosainiwa na awamu zilizopita. Sababu nyingine za kuongezeka kwa deni la nje ni kuimarika kwa Dola ya Marekani dhidi ya shilingi ya Tanzania,” amesema.

Amesema Machi 2021 kiwango cha kubadilisha Dola kilikuwa Sh2,298.5 wakati Machi mwaka huu ilikuwa Sh2,650, hivyo iwapo deni la Serikali litatajwa kwa Shilingi za Tanzania lazima lionekane limeongezeka.

“Kwa mfano deni la Serikali kwa sasa limeongezeka kwa zaidi ya Sh3.9 trilioni kutokana na kiwango cha kubadilisha fedha. Hatua hii ya kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani isichukuliwe kama hatua hasi bali ilikuwa hatua muhimu ya kukabiliana na mtikisiko wa uchumi wa dunia,” amesema.

Kuhusu mwenendo wa ulipaji wa deni la Serikali, amesema yamekuwa yakiongezeka kutoka Sh8.22 trilioni mwaka 2020/21 hadi kufikia makadirio ya Sh14.2 trilioni kwa mwaka 2025/26, kutokana na kuiva kwa mikopo ya muda mrefu na ile yenye masharti ya kibiashara iliyokopwa katika awamu zilizopita kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Amesema kuongezeka kwa malipo ya deni hasa ya nje kumesababishwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya viwango vya riba.

Mabadiliko hayo, amesema yamesababisha baadhi ya nchi hasa zinazoendelea Afrika kushindwa kulipa madeni.


Kuhusu Kilimo

Rais Samia amesema shabaha ya Serikali ni kuongeza tija katika sekta ya kilimo na kujitosheleza kwa chakula.

Katika kufanikisha hayo, amesema upatikanaji wa mbegu bora umeongezwa kwa asilimia 41.9 kutoka tani 50,747 mwaka 2021 hadi tani 72,031 mwaka 2024 na uzalishaji wa mbegu bora ndani umeongezeka kwa asilimia 61 kutoka tani 34,797 mwaka 2021 hadi tani 56,114 mwaka 2024.

Amesema Serikali imewezesha maabara ya mbegu na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu kupata ithibati ya kimataifa ya uzalishaji wa mbegu.

Rais Samia amesema upatikanaji wa mbolea umeongezwa na Serikali kutoka tani 6,76,017 mwaka 2021 hadi tani milioni 1.21 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 80.9.

Sambamba na hilo, amesema Serikali imetoa ruzuku ya mbolea yenye thamani ya Sh300 bilioni kwa mazao yote na kuongeza matumizi ya mbolea kwa hekta kutoka kilo 19 mwaka 2021 hadi kilo 24 mwaka 2025 na hivyo kuongeza tija kwenye uzalishaji.


Kuhusu bandari

Rais Samia amesema maboresho ya bandari za Tanzania na ushirikishwaji wa sekta binafsi kwenye uendeshaji wa gati umepunguza muda wa meli za makasha kusubiri kutoka siku tano na sasa kuingia moja kwa moja gatini pindi zinapowasili katika Bandari ya Dar es Salaam.

Makasha yanayohudumiwa, amesema yameongezeka kwa asilimia 35 kutoka 159,807 hadi 215,286 na jumla ya uzito wa shehena iliyohudumiwa imeongezeka kwa asilimia 14 kutoka tani milioni 14.42 hadi milioni 16.87.

Uwekezaji huo, amesema umeongeza makusanyo ya kodi kutoka Sh850 bilioni mwaka 2023/24 hadi Sh1 trilioni kwa mwezi mwaka 2025.

Matumizi kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), amesema yamepungua kwa mwezi kutoka Sh262.15 bilioni hadi Sh166.3 Mei 2024 hadi Machi 2025.