Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mimba za utotoni zapungua, matumizi holela dawa za uzazi wa mpango yaibuka

Muktasari:

  • Elimu ya afya ya uzazi kwa vijana imesaidia kupungua mimba za utotoni katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Dar es Salaam. Wakati mikoa ya Lindi na Mtwara ikipunguza mimba za utotoni kutokana na utoaji elimu ya afya ya uzazi kwa vijana, kumeibuka changamoto mpya ya uwepo wa matumizi holela ya dawa za uzazi wa mpango jambo linalohatarisha afya za watumiaji.

Takwimu za Utafiti wa Afya na Demografia Tanzania (THDS-MIS) za mwaka 2022 zinaonyesha kiwango cha mimba za utotoni katika mikoa hiyo kimepungua kikifikia asilimia 25 ikilinganishwa na mwaka 2015/2016 kilipokuwa asilimia 42, ikishika nafasi ya pili kitaifa nyuma ya Tabora na Kigoma zilizokuwa na asilimia 45 mtawalia.

Kupungua kwa mimba za utotoni ni matokeo ya juhudi madhubuti za utoaji elimu hiyo, vituo vingi vya afya vimekuwa vikitoa huduma rafiki kwa vijana kuwawezesha kupata elimu ya afya ya uzazi, ushauri, na huduma nyingine.

Mratibu wa afya ya uzazi na mtoto Mkoa wa Mtwara, Ashura Ausi, katika mahojiano na Mwananchi, anasema elimu ya afya ya uzazi imeleta matokeo chanya kwa kiwango kikubwa. "Mwaka 2023, mimba za utotoni zilikuwa asilimia 0.2 ya wajawazito wote, lakini mwaka 2024 zimepungua hadi asilimia 0.02," anasema.

Anasema elimu ya afya ya uzazi imefika shule za msingi, sekondari, vyuoni, vituo vya afya na kwenye jamii kwa ujumla, ikiwawezesha vijana kupata taarifa na maarifa sahihi.

Kwa mujibu wa Ashura, awali Mtwara ilikuwa na changamoto nyingi zikiwamo mimba za utotoni, vijana kutotambua miili yao, kuongezeka kwa magonjwa ya zinaa, utoaji wa mimba kwa njia hatarishi na hata vifo.

"Tulikabiliana na utoro shuleni, hasa wakati wa hedhi, matumizi yasiyo sahihi ya njia za uzazi wa mpango na imani potofu dhidi ya njia hizo," anasema.

Matumizi holela

Licha ya elimu kusaidia kupunguza mimba za utotoni, baadhi ya vijana wamekuwa wakinunua dawa za uzazi wa mpango bila kupata ushauri wa kitaalamu, hali inayohatarisha afya zao.

Wapo vijana wanaopata dawa hizo bila ushauri wa kitaalamu, jambo linalosababisha madhara ya kiafya kama vile mabadiliko ya homoni, matatizo ya hedhi, na hata madhara ya muda mrefu katika mfumo wa uzazi.

Zaidi ya hayo, baadhi ya vijana wanazitumia kama kinga ya dharura badala ya njia endelevu na salama, wakikosa uelewa wa kina juu ya athari zake.

Rabia Rashid (19), mkazi wa Kijiji cha Chimbuko wilayani Tandahimba, mkoani Mtwara, anasema alianza kutumia njia za uzazi wa mpango baada ya kupata elimu shuleni.

 "Nilifundishwa kuhusu afya ya uzazi nilipokuwa kidato cha pili katika somo la sayansi. Baada ya hapo nikaenda duka la dawa nikachoma sindano (kinga ya miezi mitatu) kwa Sh3,000 kwa kuwa niliogopa kwenda zahanati nitaonekana," anasema.

Anasema kwa miaka miwili alitumia sindano lakini alibaini inamletea madhara kiafya, hivyo aliamua kutumia njia ya asili ya kalenda kufuata mzunguko wa hedhi. Hata hivyo, baada ya kutokuwa makini kuhesabu mzunguko wa hedhi aliishia kupata ujauzito.

Abdallah Vitus, dereva wa bodaboda mjini Mtwara, anasema wapo wasichana wanaotumia vipandikizi, vidonge na sindano kama njia ya uzazi wa mpango.

"Hivi sasa wengi wanatumia P2 au sindano ya mara moja. Wengine wanapewa ushauri na madereva wa bodaboda ili wasipate mimba," anadai akieleza baadhi ya madereva hao huwanunulia dawa hizo au kuwashawishi kuzitumia wanapokuwa kwenye uhusiano, huku wakiwabeba bure kuwapeleka shuleni.

Safia Haji (16), mkazi wa Kijiji cha Mnyundo, wilayani Mtwara Vijijini, anasema alianza kutumia sindano baada ya kushauriwa na rafiki yake bila kupitia kwa mtaalamu.

"Nilielezwa na rafiki yangu kwamba sindano inazuia mimba, nikaenda kwenye duka la dawa nikachoma. Baada ya mwezi mmoja nikaanza kupata hedhi mfululizo, nikaambiwa nitumie vidonge kukata damu," anasema.

Subira Mwinyimkuu, mkazi wa Magomeni, mjini Mtwara, anasema baadhi ya wasichana wamekuwa wakitumia njia za muda mrefu za uzazi wa mpango kama vipandikizi.

 "Unakuta mtu ana miaka 16 hajawahi kuzaa lakini ana kijiti cha miaka mitano. Daktari unawekaje kijiti kwa mtu ambaye hata hajaanza kujitegemea? Mimi nilianza kutumia kinga baada ya kuzaa," anasema.

Anasema wasichana wanakimbilia kinga dhidi ya mimba lakini hawazingatii kujikinga dhidi ya magonjwa ya zinaa na maambukizi ikiwamo Virusi vya Ukimwi (VVU).

Hasnath Shafii, mkazi wa Mtama mkoani Lindi, anasema alichomwa sindano kwa ushawishi wa dada yake kutokana na hofu ya kupata ujauzito.

Mhudumu wa afya (jina linahifadhiwa) katika kituo cha afya Mtama anasema wasichana wengi hupelekwa na ndugu au wazazi.

"Hatuwezi kuwakatalia huduma kwa kuwa mzazi au mlezi anakwambia wazi: 'Usipomchoma (sindano) huyu mtoto sina uwezo wa kumlea pamoja na mtoto wake'," anasema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Thea Ntara, Juni 3, 2025, alizungumzia bungeni kuhusu matumizi holela ya dawa za kuzuia mimba za dharura (P2) alipochangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2025/26.

Akinukuu tafiti za wataalamu kutoka Hospitali ya Aga Khan na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), alieleza matumizi yasiyo sahihi ya P2 yanaweza kusababisha madhara makubwa kiafya kama vile mabadiliko ya mzunguko wa damu, kiharusi, kupooza, saratani ya uzazi, kuharibika kwa mimba mara kwa mara, na hata magonjwa ya zinaa.

Watumia kwa siri

Licha ya wanaopelekwa vituo vya afya na ndugu zao, wapo wanaotumia dawa za uzazi wa mpango kwa siri kama anavyoeleza Dalia Chimpota, mzazi kutoka Kijiji cha Chimbuko.

"Mtoto anaweza kuwa amevunja ungo miaka miwili iliyopita na mzazi hajui, wakati mwingine anakuja kushangaa ameshaanza kutumia njia za uzazi wa mpango. Hii inachangiwa na uoga wa wazazi kuzungumza na watoto wao," anasema Dalia akiomba elimu itolewe kwa wazazi wawasaidie watoto wao kwa kuwapa ushauri sahihi.

Fadina Chivanga, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Misri katika Kijiji cha Chimbuko, anasema mabinti wamejifunza kutumia njia za uzazi wa mpango kwa hofu ya kupata mimba.

Rashid Yusuph, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnyundo, anasema ofisa maendeleo wa kata amekuwa akitoa elimu ya afya ya uzazi na matokeo yake ni kupungua kwa mimba za utotoni.

"Wengi wanatumia sindano, vipandikizi na vidonge lakini siyo kwa shinikizo la mzazi. Ni uamuzi wao baada ya kufikia umri wa kujielewa," anasema.

Anasema pia wamekuwa wakiwajumuisha vijana wa kiume kwenye elimu ya uzazi wa mpango ili kusaidia kupunguza vitendo vya mimba na ngono isiyo salama.

Yusuph anasema licha ya mafanikio ya kupungua kwa mimba za utotoni, bado changamoto ya matumizi holela ya uzazi wa mpango inahitaji kuangaliwa kwa kina.

"Elimu endelevu kwa vijana, wazazi na jamii kwa ujumla ni muhimu ili matumizi hayo yawe salama, sahihi na kwa ridhaa inayotokana na uelewa na siyo hofu au ushawishi wa nje," anasema.

Salama Mshamu, mhudumu katika duka la dawa Tandahimba, anasema wateja wengi ni mabinti wanaoogopa kwenda hospitali kwa hofu ya kukutana na watu wanaowajua.

"Wanakuja hapa kwa sababu ya uoga, wanahofia kuonekana. Huku wanapata kwa siri na hakuna anayewauliza mengi," anasema.

Ushauri wa kitaalamu

Mtaalamu wa masuala ya uzazi wa mpango na mhudumu wa afya kutoka Hospitali ya Marie Stopes, Emmiliana Woisso, anasema matumizi ya njia za uzazi wa mpango hayana madhara iwapo yanazingatia ushauri wa wataalamu wa afya.

"Inapotokea changamoto kama vile kutokwa damu mfululizo, tunashauri kubadilisha njia ili kusaidia kurekebisha homoni za mwili," anasema.

Amewatahadharisha wasichana na wanawake ambao hawajawahi kupata watoto na wanaotumia uzazi wa mpango bila ushauri wa daktari, akieleza kuna uwezekano wa kuchelewa kupata ujauzito watakapohitaji watoto baadaye.

"Ni muhimu kufuata ushauri wa wataalamu kabla ya kuanza kutumia njia yoyote ya uzazi wa mpango. Kuna vipimo vya kitabibu vinavyotakiwa kufanyika ili kubaini ni njia ipi inafaa kwa mwili wa mtu husika," anasema.

Anasema mtu anayepanga kutumia njia zaidi ya moja kwa wakati mmoja, anapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kiafya ili kubaini kiasi cha homoni mwilini, badala ya kujihudumia moja kwa moja kwenye maduka ya dawa bila mwongozo wa kitaalamu.


Msimamo wa wizara

Akizungumza na Mwananchi Mei 20, 2025, Mratibu wa Huduma za Uzazi wa Mpango kutoka Wizara ya Afya, Zuhura Mbuguni, anasema ni kosa kisheria kwa maduka ya dawa kutoa huduma ya sindano za uzazi wa mpango, hata kama baadhi ya wahudumu wake wamepata mafunzo, bali inapaswa kutolewa kwenye vituo vya afya.

"Ni kosa kisheria kutoa huduma ya uzazi wa mpango kwenye maduka ya dawa. Mhudumu akikamatwa atachukuliwa hatua. Huduma pekee wanazoweza kutoa ni vidonge na kondomu. Sindano zinapaswa kutolewa kwenye zahanati au vituo vya afya," anasema.

Amewataka vijana wanaotumia njia za uzazi wa mpango kufuata utaratibu kwa kufika vituo vya afya ili wapatiwe elimu sahihi kutoka kwa wataalamu wenye ujuzi.

Amesema matumizi holela yanaweza kuleta madhara kiafya, kwa kuwa kila aina ya uzazi wa mpango ina utaratibu na mwongozo maalumu wa matumizi. "Kuna baadhi ya njia zinaweza kuonekana salama lakini endapo zitatumika visivyo huleta madhara mwilini," anasema.

Zuhura anasema wamejikita kutoa elimu katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambako mila na desturi zimekuwa na mchango katika kulinda watoto wa kike wanaopata ujauzito wakiwa bado wadogo.

"Mikoa hii imeanza kubadilika kutokana na elimu tunayoitoa kupitia kampeni maalumu ya afya ya uzazi. Kupitia kitengo chetu cha elimu kwa umma, tumeandaa muongozo wa utoaji wa ujumbe sahihi wa uzazi wa mpango kwa hadhira mbalimbali," anasema.

Kampeni hizo anasema huhusisha pia matumizi ya vyombo vya habari kusambaza ujumbe sahihi kuhusu matumizi salama ya njia za uzazi wa mpango.

"Tunatoa elimu kwa vijana ili wawe na uelewa mpana wa matumizi sahihi ya dawa na njia mbalimbali za uzazi wa mpango. Hili limechochea mabadiliko chanya katika mikoa ya kusini na kupunguza mimba za utotoni," anasema.

Tanzania kupitia Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa Uzazi wa Mpango Uliohuishwa wa 2019–2023 inalenga kuimarisha huduma za uzazi wa mpango, kulinda haki za afya ya uzazi na kupunguza mimba zisizotarajiwa, hasa kwa vijana na wanawake.

Unalenga kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma za uzazi wa mpango, hasa kwa vijana na wanawake wa vijijini. Pia kuzuia mimba za utotoni na zisizotarajiwa kwa njia ya elimu na huduma rafiki kwa vijana, na kutoa elimu ya afya ya uzazi shuleni na kwenye jamii.

Mkakati pia unalenga kuweka mazingira ya kisera na kisheria yanayowezesha upatikanaji wa huduma bila unyanyapaa, na kuongeza ushirikiano wa sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo.


Mipango iliyopo

Mratibu wa afya ya uzazi na mtoto mkoani Mtwara, Ashura Ausi, anasema mkoa umeandaa mkakati unaolenga kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wakiwamo wanafunzi kupitia vyumba maalumu katika vituo vya afya.

Anasema mkazo umewekwa kwa kutumia walimu waliopatiwa mafunzo maalumu kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Ashura anasema wahudumu 57 wa Serikali na tisa kutoka mradi wa USAID Afya Yangu wamepata mafunzo maalumu ili kufundisha masuala ya afya ya uzazi kwa njia rafiki na ya wazi kwa vijana.

Anasema baadhi ya shule hutoa vipindi maalumu kwa vijana ambavyo vimechangia kuwaongezea uelewa kuhusu kujikinga na mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa.


Changamoto zilizopo

Anasema baadhi ya kata hazijafikiwa na huduma kutokana na uhaba wa wataalamu wa afya ya uzazi na ukosefu wa rasilimali fedha.

Hata hivyo, anasema Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa vyumba maalumu katika vituo vya afya kwa ajili ya kutoa elimu rafiki kwa vijana.

Anasema kwa mwaka 2025 Serikali mkoani Mtwara inatarajia kukarabati na kuboresha vituo vya afya vya Likombe, Nagaga na Masasi kwa ajili ya huduma hiyo.

Kwa upande wake, mhudumu wa afya ya uzazi, kituo cha afya Kitomanga, Manispaa ya Lindi, Zawadi Ramadhani, anasema uelewa mdogo kwa baadhi ya wasichana na wazazi ni changamoto inayosababisha elimu kutopokewa ipasavyo.

Anasema baadhi ya mabinti huona aibu kupata elimu ya afya ya uzazi kwenye vituo vya afya wakidai masuala hayo ni ya watu wazima au walio kwenye ndoa.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, anasema wameweka ratiba maalumu kwa siku za Jumatano na Jumamosi kwa ajili ya vijana.

Imeandaliwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Gates Foundation