Kawaida: Tutawashughulikia wanaokejeli viongozi wetu

Muktasari:
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mohamed Ali Kawaida amesema watawashughulikia wanaowabeza viongozi wakuu wa nchi bila kujali nafasi zao walizo katika taifa hilo.
Zanzibar. Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mohamed Ali Kawaida amesema watawashughulikia wanaowabeza viongozi wakuu wa nchi bila kujali nafasi zao walizo katika taifa hilo.
Ametoa kauli hiyo leo jioni Desemba 10, 2022 katika ofisi za Jumuiya hiyo Gymkhana Mjini Unguja wakati wa mapokezi yake na kuwaagiza viongozi wote kuanzia ngazi za chini hadi taifa kushughulika na watu aliodai wanakejeli viongozi hao
"Viongozi mliochaguliwa, lazima tujue kwamba sisi ndio askari namba moja kuwalinda viongozi wetu wa taifa, hatutakubali kuona anajitokeza mtu yeyote anawakejeli viongozi wetu.
"Na hili niliseme wazi wenyeviti wa mikoa nawaagiza hakikisha hawa watu wanashughulikiwa, msipowashughulikia mimi nitawashughulikia ninyi," amesema.
Mbali na hilo amewataka viongozi hao ngazi za chini kutengeneza uchumi wa Jumuiya badala ya kuendelea kuwa tegemezi kwa ngazi zingine.
Naye Makamu Mwenyekiti , Rehema Sombi amesema wanapaswa kwenda na kasi ya Serikali huku wakizitumia fursa mbalimbali.
Awali Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Kenani Kihongosi amesema kazi hiyo ya kuongoza Jumuiya hiyo ni ngumu lakini itakuwa nyepesi iwapo watakuwa na ushirikiano.