Prime
Kardinali Pengo anavyomkumbuka Papa Francis

Muktasari:
- Amezungumzia uongozi wa Papa Francis akilitaja Jimbo Katoliki Bagamoyo.
Mwanza. Wakati mwili wa Papa Francis (88) ukitarajiwa kuzikwa kesho Jumamosi, Aprili 26, 2025, Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo, ameeleza namna anavyomkumbuka.
Papa Francis, aliyezaliwa Desemba 17, 1936 nchini Argentina, alifariki dunia Aprili 21, 2025 akiwa katika makazi yake kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta, Vatican.
Machi 13, 2013, akijulikana kwa jina la ubatizo Jorge Mario Bergoglio, alichaguliwa kuwa Papa, akasimikwa Machi 19, mwaka huo kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha Tumaini jana, Aprili 24, Kardinali Pengo amesema atamkumbuka Papa Francis kwa kutimiza ndoto yake aliyoipigania kwa muda mrefu ya kuanzishwa Jimbo Katoliki Bagamoyo.
Machi 7, 2025, Pap Francis aliunda Jimbo Katoliki la Bagamoyo nchini Tanzania, akimteua Askofu Stephano Musomba kuwa wa kwanza kuliongoza.
Kabla ya uteuzi huo, Musomba alikuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, uteuzi uliofanywa na Papa Francis Julai 7, 2021, na aliwekwa wakfu kuwa askofu Septemba 21, 2021.
Jimbo jipya la Bagamoyo limeundwa kwa kuligawa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Jimbo la Morogoro. Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Bagamoyo ni Kanisa la Moyo Safi wa Bikira Maria, lililoko mjini Bagamoyo.
“Baba Mtakatifu (Papa Francis) amefariki, tunamshukuru Mungu kwamba katika kipindi chake cha mwisho cha maisha amefanikisha shughuli nzima tuliyokuwa na hamu nayo sana ya kuwa na Jimbo Katoliki la Bagamoyo,” amesema.
Kardinali Pengo amesema katika kipindi cha utumishi wake, Papa Francis, pamoja na kuongoza kanisa katika kipindi chenye mvutano ndani yake, aliimarisha mshikamano na kuliunganisha.
Pengo, aliyeteuliwa na Papa Yohane Paulo II (sasa Mtakatifu) kuwa kardinali, amesema katika utumishi wake kama kardinali, alikuwa karibu zaidi na mapapa watatu aliowataja kuwa ni Yohane Paulo II, Benedict XVI na Francis aliyeshiriki kumchagua.
“Mwenyezi Mungu anatenda kila kitu kwa wakati wake. Kama amependa kumchukua sasa, ni kwa sababu ameona kazi yake imekamilika na shughuli ambayo Mungu alitazamia Papa Francis aifanye imefikia wakati wake. Wengine watajua namna ya kuendelea kutokea pale alipoishia,” amesema.
Uchaguzi wa Papa mpya
Kardinali Pengo amesema amekuwa akiulizwa mara kadhaa na waumini na wasio waumini iwapo atashiriki kumchagua Papa mpya.
Amesema sheria za kanisa zinaeleza wazi makardinali wanaokidhi kushiriki uchaguzi wa Papa mpya.
“Sheria ya Kanisa iko wazi juu ya suala hilo kwamba kardinali yeyote baada ya kufikia umri wa miaka 80 ya kuzaliwa, anakuwa hahesabiwi tena kuingia katika shughuli za uchaguzi wa Papa mpya.
“Sasa, sababu za kwa nini, nadhani wataalamu wanaweza kujibu, lakini nafikiri kweli baada ya mtu kufanya kazi hadi umri wa miaka 80, halafu umuongezee shughuli, kwa kweli ni nzito,” amesema.
Amesema alikuwa akimuomba Mungu, Papa Francis abaki kwenye ofisi yake hadi pale atakapotimiza miaka 80, akieleza hakuwa na hamu ya kurudi katika kazi ya uchaguzi wa Papa mwingine.
“Watu wengine wanaweza kufikiri ni heshima au ni kitu gani, lakini ni shughuli inayochosha. Kwa hiyo, sikuwa na hamu ya kwamba nirudi tena kwenye ile shughuli ya uchaguzi. Namshukuru Mungu alisikia ombi langu, Papa Francis amefariki baada ya mimi kutimiza miaka 80 ya kuzaliwa, kwa hiyo huko wataenda wanaohusika,” amesema.
Kuhusu iwapo anaweza kushiriki mazishi ya Papa Francis, amesema: “Ni wazi, ungekuwa ni mtu una uwezo wa kusafiri, hukatazwi kwenda kwenye mazishi hasa kwa nafasi yangu kwamba ni mmoja kati ya wale waliompigia kura, l akini kwa hali yangu ya kiafya, kusafiri kwenda Roma siyo kitu ambacho nakitamani sana.”
Amewatoa hofu waumini wa Kikatoliki nchini, akisema Mungu amekuwa akifanya muujiza kwa Tanzania kupata uwakilishi katika uchaguzi wa mapapa wapya tangu uchaguzi wa Papa Yohane Paulo II.
“Na hivi sasa tunaye Kardinali Protase Rugambwa, kwa hiyo hata kama ningekuwa nina uwezo wa kwenda, sioni kama Tanzania tumepungukiwa kitu,” amesema.
Kardinali Pengo amewataka Watanzania hususan Wakatoliki kuomba Papa mpya atakayechaguliwa aendeleze alichokifanya Papa Francis, ikiwamo kuimarisha uhusiano wa Kanisa Katoliki Tanzania na Roma.
“Tunaloweza kufanya kwa sasa, anapozikwa Papa Francis, tumuombe Mungu ajalie Kanisa lake, Papa atakayekuja awe kwa ajili ya manufaa ya kanisa zima na Tanzania ibaki katika uhusiano mzuri na Kanisa la Roma.
“Enzi za uhai wake, Papa Francis amejitahidi katika hali yake kwenda Sudan Kusini, katika nchi za Afrika Mashariki ama nchi za Amecea. Kwa hali yake ilikuwa ni nafasi ya neema na baraka. Tunatamani tuendelee kupata baraka hizo kwa mapapa watakaokuja,” amesema.
Kauli ya Askofu Kassala
Wakati huohuo, waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita wameungana katika misa maalumu kumuombea Papa Francis kwa Mungu ili amjalie thawabu ya kuufikia uzima wa milele.
Misa hiyo imefanyika jioni ya Aprili 24, 2025, katika Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani, ikiongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassala.
Akizungumza katika misa hiyo, Askofu Kassala amesema Papa Francis ameacha alama ya pekee duniani, ikiwemo kuishi kwa unyenyekevu, kuwa mpigania haki, amani, utunzaji wa mazingira, na maisha ya binadamu kwa ujumla. Amewaasa Wakatoliki kumuenzi kwa kuyaishi matendo hayo.
“Alitukumbusha thamani ya umaskini, alisema umaskini ni mzuri siyo kwa sababu binadamu kuishi kwenye mahangaiko, hapana! Ila kama fursa ya binadamu kusaidiana. Kweli katika hilo alionyesha hakuna asiye maskini,” amesema.
Askofu Kassala amesema: “Unaweza kuwa na utajiri wa mali ukawa na upungufu wa afya; na ukawa na afya ukawa na upungufu wa mali.”
Amesema Papa alifanya juhudi katika kupinga uharibifu wa mazingira kupitia waraka wake wa ‘Laudato Si’, akisisitiza dunia inaharibiwa na tamaa ya wachache wanaotafuta utajiri kwa gharama ya uhai wa wengi.
“Papa alionya uharibifu wa mazingira unatokana na wale wanaokula dunia hii. Alipigania haki kule kwenye msitu wa Amazon, watu wanasafisha msitu mkubwa na kuuteketeza ili wapate mafuta yaliyoko chini, huku mazingira yakiharibiwa,” amesema.
Akitoa salamu za Serikali katika misa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, amewataka waumini kuendeleza mema yaliyofanywa na Papa kama vile kuenzi amani, upendo na kuwajali maskini.
“Wapo watu wanataka kuondoka kwenye umaskini lakini wakiondoka wanasahau na kuanza kuwacheka wengine wamekuwa maskini, ama ana madaraka anamdharau asiye na madaraka, au yeye amejaliwa afya njema anawacheka wagonjwa na wenye upungufu. Badala ya kufanya hivyo, tuwaone kama ndugu zetu, huo ndiyo upendo,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Saphia Jongo, aliyehudhuria misa hiyo, amehimiza amani na kuwataka waumini kumuenzi Papa kwa kuishi kwa amani, mshikamano na upendo.
Kwa upande wake, Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Dar es Salaam, kesho Aprili 26 litaadhimisha misa ya kumuombea Papa Francis.
Taarifa ya jana, Aprili 24, ya Chancellor Padri Vincent Mpwaji kwa mapadri, watawa na waamini walei jimboni humo, imeeleza Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi anawaarifu kwamba misa hiyo itafanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu kuanzia saa 3:00 asubuhi.