Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kapinga ataka vijana kubeba ajenda nishati mbadala

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizungumza na wanahabari baada ya kutembelea kituo cha kuzalisha umeme kwa gesi cha Tegeta leo Jumatatu Oktoba 2, 2023.

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewataka vijana kubeba ajenda ya nishati mbadala ili kulinda mazingira.

Songea. Vijana mkoani Ruvuma wametakiwa kubeba ajenda ya matumizi ya nishati mbadala, kwa ajili ya Taifa ili kupunguza changamoto za uharibifu wa mazingira unaofanywa na jamii.

Hayo yalisemwa juzi Oktoba 5 na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga katika mkutano wa Baraza Maalum la Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Ruvuma lililokwenda sambamba na ugawaji wa majiko, mitungi ya gesi yaliyotolewa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

 “Hii ni ajenda ambayo Rais ameibeba kwa dhati kabisa kuhakikisha tunaanza mchakatowa kuelimisha Watanzania ili kuondokana na nishati ambazo sio rafiki kwa mazingira, na kutumia zilizo rafiki kwa mazingira,” amesema Kapinga.

Kapinga ambaye pia ni Mbunge wa Vijana Mkoa wa Ruvuma aliwataka vijana kushirikiana na wanawake, wazee na makundi mengine katika kuhakikisha wanapunguza changamoto za kimazingira kwa matumizi ya nishati mbadala.

Akiwasilisha mada kuhusu nishati safi ya kupikia, Mhandisi Kelvin Tarimo kutoka REA amesema Wakala inaendeshwa kwa mipango mikuu mitatu ambayo ni Mpango wa Sera ya Taifa wa Upelekaji Nishati Vijijini, Mpango wa usambazaji wa huduma ya umeme vijijini, pamoja na Mpango wa Nishati safi za kupikia.

Kuhusu Mpango wa nishati safi ya kupikia, Mhandisi Tarimo amesema umelenga kuhamasisha matumizi ya nishati iliyo salama kwa mtumiaji na kwa mazingira, ubora, upatikanaji wake, gharama nafuu, rafiki kwa mazingira na iliyo endelevu.

Akizungumzia aina za nishati za kupikia na kiwango cha matumizi yake kwa hapa nchini, Mhandisi Tarimo amebainisha kuwa kuni inaongoza kwa asilimia 63. 5 ikifuatiwa na mkaa asilimia 26.2, gesi oevu asilimia 5.1, umeme asilimia 3 na asilimia 2.2 vyanzo vinginevyo.

Alisema, kutokana na matumizi makubwa ya mkaa na kuni, imechangia uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na ukataji miti.

Amesema athari nyingine ni za kiafya kwa watumiaji wa nishati hizo ambapo vifo zaidi ya 33,000 hutokea kwa mwaka kutokana na kuvuta hewa ya ukaa. Vilevile, kiuchumi amesema matumizi ya nishati zisizo salama yanachelewesha maendeleo ya shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Ruvuma, Kelvin Challe aliishukuru serikali kupitia wizara ya nishati na wakala wa umeme vijijini (REA) kwa kuwapa elimu wananchi wakiwemo vijana juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati mbadala ambao ni rafiki wa mazingira.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kapinga amekabidhi msaada wa gari aina ya Toyota Noah lenye thamani ya zaidi ya Sh18 milioni, kompyuta na nukushi sita kwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoani Ruvuma.