Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamo- Hanga amesema mpaka sasa kuna upungufu wa megawati kati ya 300 hadi 350 za umeme kutoka 400 zilizokuwa wiki iliyopita.
Nyamo-Hanga alisema hayo jana wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga aliyetembelea kituo cha kuzalisha umeme unaotokana na gesi asilia cha Tegeta wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Alisema Tanesco ilifanya juhudi za matengenezo ya mitambo sambamba na kupata gesi zaidi kwa ajili ya mchakato wa uzalishaji umeme ili kukabiliana na upungufu wa megawati 400 katika gridi ya Taifa.
“Kulikuwa na matengenezo ya mitambo na upungufu wa gesi asilia kutoka kwenye visima vyetu, haya yote tuliyafanyia kazi na matokeo yake upungufu wa umeme kwenye gridi unaendelea kushuka,” alisema Nyamo-Hanga.
Septemba 27, mwaka huu, Nyamo-Hanga akizungumza na wanahabari jijini hapa, alisema kuna upungufu wa megawati 400 katika gridi ya Taifa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupungua kwa uzalishaji kutokana na kutokuwepo mvua za kutosha.
“Kiwango cha upungufu kitaanza kutatuliwa polepole, wiki mbili zijazo tatizo litaanza kupungua, mkakati ni kuongeza megawati 100 kila mwezi hadi kufikia Machi mwishoni mwakani changamoto iliyopo sasa itakwisha,” alisisitiza.
Lakini jana alisema; “wiki iliyopita tulisema kwenye gridi ya Taifa kuna upungufu wa megwati 400 za umeme, juhudi za matengenezo zimefanyika ikiwemo kupata gesi asilia hadi sasa upungufu umeshuka hadi megawati 350.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri Kapinga alisema megawati 400 zinatofautiana kulingana na uzalishaji na matumizi kwa siku.
Alisema mahitaji yakiwa juu na kama uzalishaji unakuwa mdogo, upungufu wa umeme unakuwa mkubwa.
“Lakini uzalishaji ukiwa mkubwa na mahitaji yakiwa madogo, namba za upungufu zinakuwa chache. Utakuta kuna upungufu, leo tunakosa megawati 400, kesho kutwa 200 hadi 100,” alisema Kapinga.
Katika hatua nyingine, Kapinga alitoa maelekezo kwa Tanesco, ikiwemo la kuhakikisha shughuli ya kurekebisha mitambo inamalizika kwa wakati ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa nishati hiyo nchini.
Pia, alilitaka Tanesco kuhakikisha wanazifanyia kazi kwa haraka hitilafu zote zinazotokea ili umeme uendelee kupatikana.
“Pamoja na kuja kukagua kituo hiki, nimewaelekeza Tanesco kuendelea kuboresha huduma kwa wateja. Watanzania wanapopata changamoto ndogo ndogo za umeme ikiwemo hitalafu, wahakikishe wanazitatua kwa wakati.
“Tanesco iimarishe mfumo wake wa huduma kwa wateja, hatutakubali wananchi kulala giza kwa sababu transfoma au mita haijarekebishwa kwa wakati. Waimarishe mifumo yao na kufuatilia kwa ukaribu kuhakikisha wateja wanapata huduma bora,” alisema Kapinga.
Mbali na hilo, naibu waziri huyo alilitaka shirika hilo kuunganisha huduma ya umeme maeneo yenye miundombinu kwa wakati ili Watanzania wengi waendelee kufurahia huduma ya upatikanaji wa nishati hiyo.
“Tunaendelea kusimamia kwa wakati ikiwemo kuhakikisha huduma ya upatikanaji umeme inaendelea kuimarika. Jambo jingine mtu aliyekatiwa umeme kwa saa 12 isitokea wakati wa kurejeshewa huduma akaongezewa muda.
“Umeme urudishwe kwa wakati watu waendelea na shughuli za kiuchumi, Tanesco ikae na watu wa maeneo ya uzalishaji na kukubaliana muda sahihi wa kukata na kurejesha umeme,” alisema Kapinga.
Katika ziara hiyo, wanahabari walimuuliza Nyamo-Hanga kwamba Tanesco ipo tayari kununua au kuchukua megawati 100 za umeme kutoka kampuni ya kuzalisha umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL)? Katika majibu yake, alisema wanapokea kila aina ya njia mbadala za kupata nishati hiyo.
“Kuna la kupatikana kwa umeme na suala la gharama ambazo wananchi wanaweza kuzimudu, hayo tunayazingatia. Lakini suala hilo (IPTL) muda wake mwafaka ukifika litazingatiwa kwa sababu hatubagui isipokuwa suala la bei ni muhimu kwa wananchi wetu,” alisema.