Serikali yatoa maagizo saba kwa Tanesco

Muktasari:
- Serikali yatoa maelekezo saba kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), likitaka yafanyiwe kazi ili kuimarisha huduma ya umeme kwa Watanzania.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ametoa maelekezo saba kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), likiwemo la kuhakikisha shughuli ya kurekebisha mitambo inamalizika kwa wakati ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa nishati hiyo.
Waziri Kapinga amesema masuala mengine kuhakikisha wanazifanyia kazi kwa haraka hitilafu zote zinazotokea ili umeme uendelee kupatikana.
Ametoa maelekezo hayo leo Jumatatu Oktoba 2, 2023 alipotembelea kituo cha kuzalisha umeme wa megawawati 43 unaotokana na gesi asilia cha Tegeta wilayani Kinondoni. Akisema hali ya uzalishaji wa umeme katika kituo hicho unaendelea vema.
"Pamoja na kuja kukagua kituo hiki nimewaelekeza Tanesco kuendelea kuboresha huduma kwa wateja. Watanzania wanapopata changamoto ndogo ndogo za umeme ikiwemo hitalafu wahakikishe wanazitatua kwa wakati.
"Tanesco iimarishe mfumo wake wa huduma kwa wateja, hatutakubali wananchi kulala giza kwa sababu transfoma au mita haijarekebishwa kwa wakati. Waimarishe mifumo yao na kufuatilia kwa ukaribu kuhakikisha wateja wanapata huduma bora," amesema Kapinga.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizungumza na wanahabari baada ya kutembelea kituo cha kuzalisha umeme kwa gesi cha Tegeta leo Jumatatu Oktoba 2, 2023.
Mbali na hilo, Kapinga amelitaka Tanesco kuunganisha huduma ya umeme maeneo yenye miundombinu kwa wakati ili Watanzania wafurahie huduma ya upatikanaji wa nishati hiyo.
"Tunaendelea kusimamia kwa wakati ikiwemo kuhakikisha huduma ya upatikanaji umeme inaendelea kuimarika. Jambo jingine mtu aliyekatiwa umeme kwa saa 12 isitokea wakati wa kurejeshewa akaongezewa saa.
"Umeme urudishwe kwa wakati watu waendelea na shughuli mbalimbali za kiuchumi, Tanesco ikae na watu wa maeneo ya uzalishaji na kukubaliana muda sahihi wa kukata na kurejesha umeme," amesema Kapinga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Gissima Nyamo- Hanga amesema hadi sasa upungufu wa umeme uliopo ni 350 kutoka 400 akisema bado shirika hilo linaendelea kufanya kazi ili kukabiliana na hiyo.
"Wiki iliyopita tulisema kwenye gridi ya Taifa kuna upungufu wa megawati 400 za umeme, juhudi za matengenezo zimefanyika ikiwemo kupata gesi asilia hadi sasa upungufu umeshuka hadi megawati 350," amesema Nyamo- Hanga.