Tanesco Ubungo yapewa saa 6 kurudisha umeme

Muktasari:
- Naibu waziri wa Nishati, Judithi Kapinga ametoa maelekezo kwa watendaji wa Shirika la umeme nchini (Tanesco) kituo cha Ubungo kuhakikisha wanashughulikia kukosekana kwa umeme ndani ya masaa 6.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Nishati, Judithi Kapinga ametoa maelekezo kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Kituo cha Ubungo kuhakikisha wanarudisha umeme ndani ya saa 6.
Akizungumza leo Ijumaa Septemba 29, 2023 wakati alipotembelea kituo hicho cha kuzalisha umeme jijini hapa, Kapinga amesema Kituo cha Ubungo 1 kilizimika umeme tangu jana usiku, huku jitihada za kurejesha uzalishaji zikiendelea.
"Kwenye kituo chetu cha umeme cha Ubungo 1, kuna mashine tatu na mbili ndio zinafanya kazi, moja haifanyi kazi na ipo kwenye matengenezo huku kituo Ubungo 2 kikiwa na mashine 12 na sita hazifanyi kazi na ziko kwenye matengenezo lakini hizo sita zinazofanya kazi ndio zimezimika," amesema.
Aidha ametoa maelekezo kwa wafanyakazi wa shirika hilo kuhakikisha wanakuwa na mpango madhubuti wa kufanya marekebisho kwa nyakati tofauti.
"Matengenezo ambayo yanatakiwa yafanyike kwa muda mfupi yakamilike kwa wakati kwa sababu lengo letu nikuona Watanzania wanapata umeme wa uhakika," amesema.
Ameongeza wizara hiyo inaendelea kufanyia kazi maelekezo aliyoyatoa Rais kuhakikisha kero ya kukatika umeme inakoma ndani ya miezi 6 ikiwa ni pamoja na kutengeneza mashine ambazo zimeharibika.
"Mashine zilizoharibika zina uwezo wa kuzalisha Megawati 43 kila moja, ni umeme mwingi sana. Tunaamini kama matengenezo yakikamilika kwa wakati hali ya upatikanaji wa umeme itaimarika," amesema Kapinga.