Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kanisa lamburuza DC mahakamani

Mwanza. Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, imetoa siku tano kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi kuwasilisha kiapo kinzani mahakamani kuhusu shauri la madai ya ugomvi wa kanisa.

Amri hiyo ilitolewa jana na Jaji Wilbert Chuma, wakati shauri la maombi madogo namba 68/2023, lilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa.

Ugomvi huo unahusisha kanisa lililopo eneo la Bugando, jijini Mwanza, ambalo umiliki wake unagombewa na uongozi wa kanisa la Assemblies of God Gospel Church International (AGGCI) na Kanisa la Evangelical Assemblies of God in Tanzania (EAGT).

Mleta maombi ambaye ni Mchungaji wa AGGCI, Benson Kitonka, kupitia wakili wake, Gibson Ishengoma alisema pamoja na Mahakama kutoa amri Desemba 20, 2023 kwa Mkuu wa Wilaya, Makilagi ikimtaka asitishe uamuzi alioutoa wa kuzuia ibada za waumini wa AGGCI kufanyika ndani ya kanisa hilo, amri hiyo haijatekelezwa.

Hivyo, mleta maombi kupitia wakili wake anaiomba Mahakama Kuu itoe maelekezo kwa DC Makilagi awasilishe utetezi wake kwa nini hajatekeleza amri ya Mahakama hiyo, iliyomtaka awaruhusu waumini wa AGGCI kusali katika kanisa hilo.

“Kwa kuwa mjibu maombi (Makilagi) hajawasilisha kiapo kinzani wakati amepatiwa samansi (wito wa Mahakama) ya kufanya hivyo, tangu mwaka jana, mheshimiwa tunaiomba Mahakama yako ichukue hatua dhidi yake ili kutenda haki kwa mteja wangu, kwani haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyonyimwa,” alisema Ishengoma.

Amri ya Mahakama iliwasilishwa katika ofisi ya DC Makilagi tangu Desemba 21, 2023, na dalali wa Mahakama kutoka Kampuni ya Isangi Auction Mart & Court Broker, Silas Isangi.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Sabina Yongo aliieleza Mahakama kuwa mjibu maombi (DC Makilagi) alishindwa kuwasilisha kiapo kinzani kwa sababu yupo mapumzikoni, huku akiomba Mahakama kutoa muda kwa mjibu maombi kutekeleza amri hiyo.

“Mheshimiwa amri ya Mahakama yako iliwasilishwa wakati mjibu maombi hayupo ofisini, hivyo hakukuwa na uwezekano wa kusaini kiapo kinzani.

“Niiombe Mahakama yako kutoa muda ili mjibu maombi asaini na kuwasilisha kiapo kinzani ili kutenda haki kwa pande zote,” alisema wakili Yongo.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Chuma alitoa siku tano kuanzia jana Januari 5, upande wa mjibu maombi kuwasilisha kiapo kinzani mahakamani hapo, kisha akaahirisha shauri hilo hadi Januari 10, 2024 litakapoanza kusikilizwa.
 

Mgogoro ulivyoanza

Akizungumza baada ya shauri hilo kuahirishwa, wakili Ishengoma alisema mwaka 2022, baada ya kutokea mpasuko ndani ya Kanisa la EAGT na kutokuwepo dalili za mgogoro huo kwisha, Msajili wa Jumuiya aliamuru makanisa hayo kutengana.

Pia aliamuru fedha na vyombo vya kusalia vibaki chini ya umiliki wa EAGT.

Ishengoma alisema miongoni mwa makanisa yaliyojitenga ni kanisa la AGGCI lililopo eneo la Bugando, jijini Mwanza chini ya mchungaji Benson Kitonka.

Hata hivyo, EAGT iliendelea kusisitiza kanisa hilo kuwa liko chini ya usimamizi wake.

Baada ya mvutano huo, kanisa la AGGCI lilifungua shauri mama la madai namba 28015/2023, mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Stanley Kamana na kuiomba Mahakama itoe amri kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi kutengua amri yake ya kuzuia ibada za AGGCI ndani ya kanisa hilo, huku akiruhusu ibada za waumini wa kanisa la EAGT.

“Pamoja na Mahakama kutoa amri hiyo tangu Desemba 20, 2023, Mkuu wa Wilaya alikaidi na kuagiza kanisa liwe chini ya EAGT na kuzuia waumini wa AGGCI kuabudu katika kanisa hilo, hatukuridhishwa na kauli ile ndiyo maana tumefungua shauri lingine mahakamani,” alisema Ishengoma na kuongeza:

“Kwa kipindi chote hicho mteja wangu na waumini wake wamekuwa wakiendesha ibada chini ya mti nyumbani kwake. Ndiyo maana tumeleta maombi mengine mahakamani katika shauri namba 68/2023, kwa sababu tunaamini haki ndipo inapotolewa,” alisema.

Kwa upande wa Askofu wa AGGCI Kanda ya Ziwa Mashariki, Julius Mbaraka, alisema kanisa hilo ni moja kati ya makanisa 542 yaliyojitenga nchi nzima baada ya mgogoro wa muda mrefu ndani ya EAGT, huku makanisa 87 yakiwa mkoani Mwanza.