Kamati ya wafanyabiashara kuwasikiliza wa mikoani kwa siku nne

Kamati ya kusikiliza kero za wafanyabiashara nchini iliyoundwqa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Muktasari:

  • Kamati hiyo iliyojumuisha wajumbe 14,  iliundwa Mei 17 katika hitimisho la kikao kati ya wafanyabiashara wa Kariakoo na Waziri Mkuu kwa  ajili ya kushughulikia changamoto za soko hilo na kuja na suluhusho baada ya kufanyika kwa mgomo wa siku tatu katika soko hilo la Kimataifa.

Dar es Salaam. Kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa ajili ya kutatua migogoro baina ya wafanyabiashara na Serikali, imemaliza kazi ya kukusanya maoni jijini hapa na sasa inaelekea mikoani ambako itakaa huko kwa siku nne.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mei 26, 2023 Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk John Jingu alisema tayari wameshamaliza kazi ya kupokea maoni ya  wafanyabiashara na wadau katika Jiji la Dar es Salaam na sasa ni zamu ya kuwasikilizana wa mikoani.

Katika kuifanya kazi hiyo, Dk Jingu alisema wamegawa mikoa katika Kanda tano ambapo wanatarajia hadi kufika Mei 31 watakuwa wamemaliza kazi hiyo na kujiandaa kwa ajili ya kuikabidhi ripoti yao.

“Kwa kuwa tulipewa siku 14 za kufanya kazi hii, tumejidhatiti kufanya kazi usiku na mchana ili kuweza kuimaliza kwa wakati,”alisema.

“Nitumie nafasi hii kuwashukuru wafanyabiashara wa Kariakoo na wa maeneo mengine katika jiji hilo kwa namna walivyotupatia ushirikiano kwani bila wao tusingeweza kufanya kazi hii,”aliongeza.

Aidha Dk jingo alisema wamekutana na wadau mbalimbali wanaohusika na masuala ya biashara wa akiwemo Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mamlaka za Udhibiti   wakiwemo Shirika la Viwango Tanzania(TBS),  TASAC, Tume ya Ushindandi Nchini (FCC), Jeshi la Polisi, Jeshi la Uhamiaji na Jeshi la Zimamoto.

Tangu wameanza kazi hiyo, Dk Jingu amesema mafanikio mbalimbali yamejitokeza ikiwemo wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao, kusitishwa kwa kamatakamata na kuachiwa kwa mizigo mingi ambayo ilikuwa imekamatwa na TRA.

“Wito wetu ni wote kuendelea kutimiza wajibu wetu ili biashara ziendelee kufanyika vizuri ikiwemo wafanyabaishara kulia kodi ili kumwezesha Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza wajibu wake vizuri,”amesemaMwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti mwenza na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Hamis Luvembe, alisema kwa siku 12 walizofanya vikao jijini hapa kazi nzuri imefanyika na kushukuru namna wafanyabiashara walivyoweza kufunguka bila woga na wengine kukiri kufanya makosa lakini ilikuwa kwa kutojua.

Kamati hiyo iliundwa na Waziri Mkuu baada ya mgomo wa siku tatu mfululizo wa wafanyabiashara wa soko la Kariakoo wakishinikiza kuondolewa kwa ushuru was too na kamatakamata waliyodai inafanywa na maofisa wa TRA sokoni hapo.