Jela miaka mwili kwa kujifanya ofisa wa Takukuru

Mshtakiwa Edson Beyanga aliyejifunika uso akiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi, baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani, baada ya kupatikana na hatia kujifanya ofisa wa Takukuru na kughushi kitambulisho cha NEMC. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Beyanga ametiwa hatiani katika mashtaka matatu ambayo ni kughushi fumo ya kuondoa kesi ya jinai, kughushi kitambulisho cha kazi na kujifanya ofisa wa Takukuru.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Kisutu, imemhukumu mfanyabiashara Edson Beyanga(37), kifungo cha miaka minne jela baada ya kupatikana na hatia ya kughushi fomu ya kuondolewa kesi ya jinai iliyotolewa na Takukuru.
Pia Beyanga amehukumiwa kwa kutengeneze kitambulisho cha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ( NEMC) chenye jina la mtu mwingine.
Kadhalika mahakama hiyo imemhukumu kulipa faini Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kujifanya Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa( Takukuru).
Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa, Machi 28, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.
Hata hivyo, Hakimu Nyaki alisema adhabu hizo zinakwenda kwa pamoja, hivyo mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka miwili jela.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Nyaki alisema: "Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watani na vielelezo viwili ambavyo ni barua ya kuondolewa kwa kesi ya Jinai na kielelezo kingine ni kitambulisho cha NEMC, ambavyo vimethibitisha mashtaka bila kuacha shaka" alisema hakimu Nyaki.
Alisema baada ya kupitia ushahidi na vielelezo, mahakama imemtia hatia mshtakiwa kama alivyoshtakiwa.
Awali, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Takukuru, Imani Nitume, aliomba mahakama itoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa kwa sababu makosa yake yanaleta madhara makubwa kwa jamii.
Mahakama ilimpa nafasi mshtakiwa ajitete, kwa nini asipewe adhabu kali ambapo, Beyanga aliomba mahakama imfutie mashitaka yote, kwa sababu ana mtoto mlemavu anayemtegemea na kwamba akifungwa atakosa msaada.
Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza hoja za pande zote, alitupilia mbali ombi la mshtakiwa na kukubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela kutokana na adhabu hizo kwenda kwa pamoja.
Katika kesi hiyo, mshtakiwa anadaiwa kati ya Desemba 11 na Desemba 15, 2020 ndani ya Dar es Salaam, alijifanya yeye ni Ofisa wa Takukuru kwa jina la Juma Tambwe.
Shtaka la pili ni kughushi, tukio analodaiwa kulitenda Agosti 4,2018 akiwa jiji la Dar es Salaam, kwa udanganyifu alitengeneza fomu ya kuondoa kesi ya Jinai iliyotolewa na Takukuru.
Shtaka la tatu, siku hiyo ndani ya Jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa alitengeneza kadi ya mfanyakazi yenye majina ya Boniface Mrema ikionyesha kwamba ni kitambulisho cha NEMC, wakati akijua kuwa ni uongo.