Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Janga la uvunaji misitu linavyovimaliza vijiji

Mkazi wa Kitongoji cha Mbala, Jacob Samwel akionyesha baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na uchomaji na uchomaji mkaa. Picha na Kelvin Matandiko

Muktasari:

Changamoto ya uvunaji misitu imeendelea kushamiri maeneo kadhaa nchini, huku viongozi wakikusanya ushuru wa wavunaji hao bila kujali uharibifu unaofanyika.

Chalinze. Changamoto ya uvunaji misitu imeendelea kushamiri maeneo kadhaa nchini, huku viongozi wakikusanya ushuru wa wavunaji hao bila kujali uharibifu unaofanyika.

Miongoni mwa viongozi hao ni wa Kijiji cha Chamakweza, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambapo asilimia 60 ya hekta 12,000 za mipaka yake zimevunwa ndani ya miaka 18 huku wakichukua tozo za wavunaji hao wa mkaa.

Baadhi ya wanunuzi na wasafirishaji wa mkaa huo wamesema Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) hutoza Sh250 ya kibali katika kilo moja ya mkaa, ushuru wa Sh6,000 wa Halmashauri ya Kibaha, Sh1,000 ya maendeleo ya kijiji husika, sawa na jumla ya Sh44,500 kwa gunia tatu za Sh180,000.

Kutokana na uvunaji huo wa mkaa, zaidi ya ng’ombe 7,000 kati ya 22,000 walikufa kutokana na kiangazi kilichotokana na hali ya ukame kama ilivyothibitishwa na Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mika Mashimba.

Kijiji hicho kina idadi ya wakazi 4,712, asilimia 90 wakiwa wafugaji wanaoishi vitongoji vitano vya Chamakweza yenyewe, Mjimwema, Idara ya Maji, Njiapanda na Mbala.

Hata hivyo, Mashimba alikiri kushiriki kwenye uchukuaji wa tozo ya uvunaji wa mkaa usiozidi Sh100,000 tu, ikilinganishwa na makadirio ya Sh3 milioni anayotarajia kwa mwaka, hatua iliyolazimu halmashauri ya kijiji hicho kuweka mpango wa zuio la wavunaji wa mkaa.

“Hakuna faida yoyote na hali inazidi kuwa mbaya, mwaka jana tumepoteza ng’ombe sababu ya ukame ambao thamani yake hailingani na tozo hiyo ya mkaa, ni kuhatarisha maisha tu, mwaka 2014/15 tulijaribu kuzuia hali ikawa nzuri, lakini wakarejea tena, elimu ndogo ya matumizi ya gesi ya kupikia inachangia hali hii,” alisema Mashimba.

Akizungumzia namna wanavyochoma mkaa, Kondo Mwaule (75), mkazi wa kijiji hicho kitongoji cha Mbala alisema huchoma tanuru moja kwa mwezi lenye uwezo wa kuzalisha gunia 18 zenye thamani ya Sh210,000, huku akitumia Sh 50,000 kuandaa na kupata faida ya Sh 160,000 inayomwezesha kuhudumia familia yake yenye watoto 16 na wake watatu.

“Nipo tayari kulinda mazingira lakini kazi hii siiachi kamwe, sina mtaji wala biashara nyingine, hivyo inasaidia kuendesha familia yangu na kupata nishati ya kupikia, sina uwezo wa kununua hiyo mitungi ya gesi ya kupikia, labda hao wenye pesa,” alisema Mwaule.

Kwa upande wa Mbambile Kisanjo, Mwenyekiti mstaafu aliyetumikia kijiji hicho kati ya 2004/2014 alisema wakati anaingia madarakani alikuta asilimia 20 ya kijiji hicho imevunwa miti bila kuwepo juhudi za kuirejesha kutokana na changamoto za wakazi wasiokuwa na vyanzo vya mapato.


Usafirishaji

Suleiman Burega, Ofisa Habari wa TFS Kanda ya Mashariki alisema wanatoa vibali na leseni za uvunaji wa misitu chini ya Sheria ya Misitu namba 14 ya mwaka 2002 inayotoa maelekezo ya uvunaji wa mazao hayo kwa kuzingatia mpango wa uvunaji wanaouandaa kila mwaka na TSF.

“Sina hakika kama hicho kijiji kipo ndani ya mpango huo, kama hakipo basi itakuwa ni uvunaji wa makosa kisheria na adhabu zake zipo, kabla ya uvunaji huwa inafanyika tathmini ili kujiridhisha, uvunaji siyo uharibifu kisheria, kwa hiyo tozo zinatozwa maeneo mahususi,” alisema Burega.

Baadhi ya wanunuzi na wasafirishaji wa mkaa kundi la Tupendane maarufu kama Busta walidai uhalali wa kufanyika biashara hiyo umeongeza kasi ya uvunaji haramu wa mazao hayo ya misitu.

“TFS ilifunga uvunaji katika pori la vijiji vya Lukenge, Kimara Misale, lakini unaendelea. Nafikiria kuacha biashara hii nifanye kazi nyingine,” alisema Kitwana Samatta, mmoja wa wanachama zaidi ya 300 Bodaboda wanaonunua mkaa.