Prime
Ilivyokuwa kabla, baada ya maziko ya kada wa Chadema

Viongozi mbalimbali wakiwa msibani kwa aliyekuwa kada wa Chadema, Ali Kibao nyumbani kwake mkoani Tanga, katika shughuli ya mazishi yake akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni. Picha na Rajabu Athumani
Muktasari:
- Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masuani amesema Serikali haitavumilia na haijawahi kuvumilia jambo lolote linalokiuka haki ya mtu kuishi.
Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya Chadema, Ally Kibao umezikwa eneo la Kijiji cha Tarigube kata ya Togoni mkoani Tanga, huku ujumbe uliotawala kwa walio wengi ni kulaani na kuchukuliwa hatua kwa waliohusika na mauaji yake.
Kibao, alichukuliwa ndani ya basi la Tashrif jioni ya Ijumaa Septemba 6, 2024, eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam na watu waliokuwa na silaha, wakati akisafiri kwenda nyumbani kwake, mkoani Tanga.
Tukio hilo lilianza kujadiliwa maeneo mbalimbali Jumamosi ya Septemba 7, 2024, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alizungumza na waandishi wa habari kuzungumzia tukio hilo na kutoa wito kwa vyombo vya usalama kulichunguza.
Katikati ya mijadala hiyo, asubuhi ya Jumapili, Septemba 8, 2024, kuliripotiwa mwili wa Kibao kuonekana umetupwa eneo la Ununio, jirani na viwanja vya NSSF. Ulichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Dar es Salaam.
Kutokana na tukio hilo, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alitumia akaunti zake za kijamii kulilaani na kuagiza uchunguzi wa haraka kufanyika.
Rais Samia alisema: “Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya mauaji ya kiongozi wa Chadema, Mohamed Ali Kibao. Natoa pole kwa viongozi wa chama hicho, familia ya Mzee Kibao, ndugu, jamaa na marafiki.
“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,” alisema.
Kauli za waombolezaji
Leo Jumatatu, Septemba 9, 2024 wakiwa nyumbani kwa Kibao katika eneo la Usagara mkoani Tanga kulipofanyika swala kabla ya kwenda kuzikwa, waombolezaji walisema ni vigumu kwa Rais Samia kuagiza tukio hilo kufanywa uchunguzi na vyombo vya dola, ambavyo ndio watuhumiwa wa kwanza kwenye tukio hilo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mbele ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masuani, amemtaka kiongozi huo kumfikishia ujumbe Rais Samia kuwa vyombo vya dola kuchunguza tukio ambalo wao ndio watuhumiwa namba moja, haiwezekani.
"Wewe (Masauni) kama mwakilishi wa Rais katika msiba huu, mwambie mheshimiwa Rais rai ya waombolezaji katika msiba huu yeye pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuunda tume ya kijaji ya kimahakama ambayo inaweza kuchunguza matukio haya yote na yaliyojificha," amesema.
Mbowe amegusia suala la kupotea kwa kiongozi wao, Dionis Kipanya, Kombo Mbwana wa mkoa wa Tanga ambaye alikamatwa bila kuwepo taarifa akisisitiza ni lazima watu walalamike.
“Leo mnaweza kuona amani hii inayumba katika msiba huu, ipo siku amani hii msipoangalia itayumba katika mitaa yote ya nchi hii,” amesema.
“Sisi tunapokasirika ni kielelezo cha ukubwa wa tatizo ambalo inawezekana mliopo kwenye mamlaka hamuioni kwa sababu ninyi mkifika kuzika mnazika ndugu zetu waliokufa mazingira ya kawaida, sisi tunazika ndugu zetu ambao siku zao za Mungu hazijafika,” amesema.
Msingi wa hoja hiyo ni baada ya waombolezaji kuoneshwa kuchukizwa na alichokuwa akikizungumza awali Waziri Masauni hadi kukatishwa na kutakiwa kuondoka. Hata hivyo, Mbowe aliwasihi waombolezaji kuheshimiana na kumwacha Masauni amalizie hotuba yake.
Mbowe amesisitiza, tume itakayoundwa itatoa fursa ya ushahidi ambao hawawezi kuupeleka Polisi.

Makundi ya wafuasi wa vyama vya siasa, viongozi wa Chadema na ACT-Wazalendo wakiwa nyumbani kwa aliyekuwa kada wa Chadema, Ali Kibao katika eneo la Usagara mkoani Tanga kwa ajili ya kushiriki mazishi ya kiongozi huyo. Picha na Rajabu Athumani
Kiongozi huyo wa Chadema amesisitiza kupitia vyombo vya habari wapo watu aliowataja kwa majina hata hivyo bado wana ushahidi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo-Bara, Isihaka Machinjita, amesema tayari chama hicho kimetoa wito wa Waziri Masauni kuachia ngazi.
Sambamba na hilo amesema ni muhimu Rais Samia kuunda tume ya kijaji kuchunguza matukio yanayoendelea kutokea nchini, kwani ni ngumu sasa kufanyika uchunguzi.
“Kwa matukio yanayoendelea tumeshatoa wito Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camilius Wambura kuachia ngazi na Rais Samia aunde tume ya kijaji kuchunguza matukio yanayoendelea kutokea nchini kwani ni ngumu sasa kufanyika uchunguzi,” amesema.
Wito kwa Waziri Masauni kuachia ngazi, umezungumzwa pia na Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini wa Chadema, Godbless Lema pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika wakisema anapaswa kuachia nafasi hiyo kwani tukio hilo halikubaliki.
Alichosema Masauni
Akizungumza kwenye msiba huo, Waziri Masauni kwa niaba ya Serikali alitoa salamu za pole akisema Rais Samia ameguswa na tukio la kifo cha Ally Kibao.
“Niwape salamu za Serikali kupitia viongozi wetu Rais Samia Suluhu Hassan ambaye mmeona namna alivyoguswa na jambo hili, mliona taarifa aliyoitoa na maelekezo ya kufanyika uchunguzi kwa haraka wahusika wote wachukuliwe hatua kwa mujibu wa Sheria," amesema.
Masauni amesema tukio la mauaji ya kiongozi huyo halikupaswa kutokea kwani Tanzania, inasifika duniani kote kwa usalama na amani.
Kiongozi huyo amewahikikishia waombolezaji wote hususan familia ya marehemu, Serikali halitaliacha jambo hilo liende hivi hivi na tayari maelekezo ya Rais Samia yameanza kutekelezwa na wote watakaobainika hatua zitachukuliwa.
Waziri huyo ametoa maelekezo kwa watu kuacha kutoa shutuma, badala yake kwa mwenye ushahidi wowote anapaswa kuwasilisha ili hatua zichukuliwe kwa wahusika.
Kauli hii haikuwafurahisha waombolezaji na kuanza kumtaka kuacha kuongea na ndipo Mbowe alipoingilia kati.