Hivi ndivyo kada Chadema alivyotekwa ndani ya basi

Muktasari:
- Gari mbili, watu wanne ndiyo waliotajwa na mashuhuda kuhusika na utekaji wa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao. Kondakta wa gari hilo aeleza ilivyokuwa.
Dar es Salaam. Magari mawili yaliyokuwa na namba za usajili zisizo za kawaida, ndizo zilizotajwa na mashuhuda kuhusika katika tukio la ukamatwaji wa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao Ijumaa ya Septemba 6, 2024.
Kwa mujibu wa mashuhuda tukio hilo lilitokea saa moja jioni, muda ambao tayari giza lilishaanza kuingia na hakukuwa na aliyekuwa na wasiwasi kwa kuwa walidhani wakamataji ni askari wa Jeshi la Polisi.
Kibao, alikamatwa Ijumaa ya Septemba 6, 2024 Tegeta mbele ya Jengo la Kibo Complex na siku moja baadaye mwili wake uliripotiwa kupatikana Ununio, jijini Dar es Salaam akiwa ameuawa huku uso wake ukiwa umeharibika kiasi cha kutotambulika.
Mwili wake ulipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na ulifanyiwa uchaguzi wa kitabibu na taarifa yake bado haijawekwa wazi. Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amedai kifo cha Kibao kilikuwa cha mateso na uso wake ulimwagiwa tindikali.
Tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kusikitishwa na tukio hilo akisema: “Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya mauaji ya kiongozi wa Chadema, Mohamed Ali Kibao. Natoa pole kwa viongozi wa chama hicho, familia ya Mzee Kibao, ndugu, jamaa na marafiki.
“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,” amesema.

Alivyokamatwa
Leo Jumatatu, Septemba 9, 2024, Mwananchi imefika Tegeta alikokamatwa Kibao ambako ni umbali wa takriban mita 20 kutoka Jengo la Kibo Complex, ni eneo ambalo aghalabu mabasi yanayoelekea Tanga, Moshi na Arusha husimama kupakia abiria.
Kama ulivyo utaratibu wa kawaida, basi la Tashriff alilokuwa amepanda Kibao lilisimama kupakia abiria kwa mujibu wa mashuhuda, gari mbili zenye namba nyeupe ambazo zimeandikwa kwenye vibao vyeusi.
Shuhuda huyo ambaye ameomba hifadhi ya jina lake, amesema gari moja iliegeshwa mbele ya basi hilo na lingine liliegeshwa nyuma ya basi hilo, kisha watu wanne walishuka kwenye gari hizo.
“Wanne wote walikuwa na risasi (akimaanisha bunduki) alienda kwenye mlango wa basi na wawili wakaingia ndani, wawili walibaki mlangoni,” amedai.
Alichokisikia shuhuda huyo ni kauli kutoka kwa mmoja wa watu hao kuwa, ‘tumemfuata mtu wetu’ na kwa namna walivyokuwa kila mmoja alidhani ni polisi.
Amedai walioingia ndani ya basi walitoka na Kibao wakiwa wamemfunga pingu na hata aliyekamatwa naye hakuwa na wasiwasi, hali iliyofanya mashuhuda waondoe wasiwasi zaidi.
“Walivyotoka naye wakamuongoza hadi kwenye Land Cruiser wakamwingiza humo na wengine wakaenda kupanda V8 wakaondoka naye,” ameeleza.
Uelekeo wa safari hiyo, shuhuda mwingine amesema ni Bagamoyo, lakini gari hizo awali zilifika hapo zikitokea uelekeo wa Mwenge.
“Kila mmoja akawa anasema jamaa amekamatwa na polisi atakuwa mhalifu, hakuna aliyekuwa na mashaka. Mimi niliangalia namba za usajili wa gari wakati zinaondoka lakini sikuzizingatia, nilichoona ni rangi nyeupe na zimeandikwa kwenye kibao cheusi, sio za kawaida,” amedai.
Naye Kondakta wa basi hilo la Tashriff Express, Abdul Mvumo amedai baada ya basi hilo kusimamishwa, watu watatu bila kutaja aina ya nguo walizovaa waliingia wakiwa wamebeba bunduki mkononi.
"Baada ya kuingia walienda moja kwa moja hadi alipokaa abiria wangu na kumchukua, kisha kuondoka naye. Kwa namna walivyokuwa, walivyoingia na silaha walizobeba mikononi hatukuwa na ujasiri wa kuhoji," amedai.
Abdul amezungumza na Mwananchi mchana wa leo Jumatatu, Septemba 9, 2024 katika ofisi zao za Magomeni Mwembechai, Dar es Salaam akitokea Tanga kwenda mkoani Mtwara.
Katika maelezo yake amedai hawezi kuzungumza zaidi kwa kuwa yupo nje ya muda, baada ya kuchelewa kuhojiwa na Polisi ingawa hakutaja ni kituo gani cha polisi aliitwa.
Alipoulizwa katika basi hilo kuna kamera za kurekodi matukio katika majibu yake amedai:"Basi halijafungwa kamera. Nikuambie kama unataka kupata tukio hili kwa undani nenda kaongee na mashuhuda Kibo Complex watakueleza."
Alichoshuhudia mwandishi
Eneo kilipo kituo hicho ni mita 20 kutoka Jengo la Kibo Compex lenye Kamera za CCTV. Kwa namna ilivyo, isingekuwa rahisi kwa Kamera za Kibo Compex kuona kinachofanyika katika kituo hicho.
Mbali na mazingira hayo, woga na hofu zimekita mizizi katika mioyo ya mashuhuda wa tukio hilo, wengi walioulizwa walidai hawafahamu kilichotokea.
Wachache waliosimulia, waliomba hifadhi ya majina yao kwa kile walichodai wana familia zinazowategemea na mazingira yaliyomtokea Kibao yasije kuwatokea wao pia.
“Kama mtu amekuja kumchukua mtu hapa mbele yetu na baadaye akamuua, anashindwa vipi kunifuata mimi hohehahe akanimaliza,” ameeleza shuhuda mmoja.
Mwingine amesema ameshafuatwa na watu zaidi ya watatu kuulizwa kuhusu alichoshuhudia wakati wa tukio hilo, lakini hakutoa ushirikiano kwa hofu ya kuhusishwa katika kesi hiyo.