Hospitali ya Bugando yazindua tovuti ya huduma kidijitali

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando, Dk Fabian Massaga (wa tatu kushoto walioketi) akipozi kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wakuu wa idara za hospitali hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi wa tovuti ya huduma za tiba kidijitali. Picha na Damian Masyenene.
Muktasari:
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) inahudumia wagonjwa kati ya 1, 000 hadi 1, 500 kwa siku. Hospitali hiyo inayotoa huduma za rufaa za kibingwa kwa wagonjwa kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu, Geita, Kagera, Shinyanga, Tabora na Kigoma.
Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) imezindua tovuti itakayowawezesha wagonjwa kuweka miahadi ya kuonana na madaktari na kuwasilisha hoja, malalamiko na ushauri kwa uongozi.
Pamoja na kumaliza tatizo la wagonjwa na watu wenye kuhitaji huduma za kiafya kulazimika kufika hosptalini kuweka miahadi, huduma hiyo ya kidijitali pia itamaliza tatizo la msongamano wa wagonjwa hospitalini kwa wakati mmoja kwa sababu kila mmoja atapangiwa muda maalum kulingana na nafasi ya wataalam na mabingwa wanaotoa huduma.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua tovuti hiyo leo Mei 22, 2023, Mkurugenzi Mkuu wa BMC, Dk Fabian Massaga amesema tovuti hiyo iliyosanifiwa na wataalam wazawa wa Idara ya Tehama hospitalini hapo ni sehemu ya mapinduzi mahususi ya huduma inayotekelezwa kuboresha huduma katika hospitali hiyo inayohudumia wagonjwa kati ya 1, 000 hadi 1, 500 kwa siku.
‘’Hii ni hatua nyingine ya kupanua na kuboresha huduma baada ya kufungua tawi letu katikati ya jiji la Mwanza kuwezesha wagonjwa wasiohitaji huduma za dharura wanaobanwa na shughuli za kijamii na kiuchumi kupata fursa ya kuweka miahadi na kukutana madaktari kwa muda wanaohitaji wao,’’ amesema Dk Massaga.
Kupitia tovuti hiyo, wananchi siyo tu wataweka miahadi, bali pia watapata taarifa zote muhimu za huduma zinazotolewa na Hospitali ya Bugando.
Ofisa Tehama BMC, Joas Dionizi amesema kupitia tovuti hiyo, kila mtu anayehitaji huduma, ushauri na matibabu ataweza kuwasiliana na daktari kwa njia ya mtandao popote alipo duniani.
‘’Uongozi wa hospitali pia utapata fursa ya kupokea na kutatua kero, hoja na changamoto wanazokumbana nazo wananchi wanaohudumiwa na Hospitali ya Bugando,’’ amesema Joas
Kupitia huduma hiyo, wananchi wanaohitaji kuonana na uongozi wa hospitali hiyo akiwemo Mkurugenzi Mkuu hawatalazimika kufika ofisini moja kwa moja kuweka miahadi kwa Katibu Mukhtasi, badala yake, wataweka miahadi na wakati mwingine kuhudumiwa kidijitali bila kuonana na uso kwa uso na ofisa au kiongozi anayemhudumia.
Fursa kwa watafiti
‘’Watafiti nao sasa watahudumiwa ikiwemo kupata fomu ya usajili popte walipo duniani kimtandao bila kulazimika kuja Bugando,’’ amesema mtaalam huyo
Upatikanaji wa taarifa na machapisho mbalimbali za kitafiti ni fursa nyingine itakayoambatana na matumizi ya tovuti mpya iliyozinduliwa BMC.
Elias Samson, mkazi wa jiji la Mwanza amepongeza maboresho yanayoendelea kufanywa na uongozi wa BMC katika huduma zake huku akishauri wanaohusika na kusimamia tovuti hiyo kuhakikisha siyo tu huduma inapatikana muda wote, bali pia madaktari, wataalam na watoa huduma wote wanafikiwa kwa wakati.