Hoja kubinafsisha vituo vya afya, zahanati yaendelea bungeni

Mbunge wa Musoma Mjini (CCM), Vedastus Manyinyi akizungumza wakati akichangia mjadala wa makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu leo Jumatatu Aprili 8, 2024. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
- Mbunge Mayinyi aungana na Shabiby kutaka Serikali ijiondoe kusimamia zahanati, vituo vya afya na hospitali. Manyinyi amesema kwa Musoma, mjamzito akienda hospitali maana yake ni pesa. Waziri wa Afya ampa taarifa ya mafanikio, yeye (Manyinyi) ameikataa.
Dodoma. Hoja ya kutaka vituo vya afya, zahanati na hospitali vinavyomilikiwa na Serikali wapewe sekta binafsi na taasisi za dini, imeendelea kuzungumzwa bungeni na Mbunge wa Musoma Mjini (CCM), Vedastus Manyinyi.
Hoja hiyo imetolewa leo Jumatatu Aprili 8, 2024 na Manyinyi ikiwa ni mara ya pili baada ya mwishoni mwa wiki kutolewa bungeni na Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, huku akitoa mifano ya Abu Dhabi na Korea Kusini.
Manyinyi na Shabiby wametoa hoja hiyo kwa siku tofauti, wakati wakichangia makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakishauri Serikali ijiondoe na kubinafsisha vituo vya afya, zahanati na hospitali.
“Kwa hiyo ndio nasema mimi ushauri wangu tuiondoe kabisa Serikali katika kuhudumia wananchi kwenye upande wa afya, maana imejaribu mara nyingi na mara nyingi imeendelea kushindwa kwa hiyo. Hilo ndio ombi langu kubwa kwenye huona upande wa afya,” amesema Manyinyi.
Shabiby mbali na kutaka wamiliki wa laini za simu wakatwe Sh2,000 kila mwezi kuchangia Bima ya Afya, pia alishauri zahanati, vituo vya afya na hospitali zibinafsishwe kuepuka ubadhirifu na watumishi wasio na uzalendo, wakati Bima ya Afya kwa wote itakapokuwa imeanza.
Leo Jumatatu, Manyinyi ameunganisha hoja yake hiyo na Bima ya Afya kwa wote akisema Serikali ikijiondoa na kuachia sekta binafsi itaepuka vitendo vya kilaghai kama kughushi nyaraka wakati wa matumizi ya bima ya afya.
“Tunavyoelekea kwenye Bima ya Afya kwa wote mimi ushauri wangu hebu tuondoe kabisa Serikali kwa maana ya kuwa na vituo vya afya na zahanati. Na kwa sababu tutaumia bima ya afya ni vizuri hivyo vituo vya afya, zahanati na hospitali tukayapa kwanza yale mashirika ya kidini, ili yaweze kuhudumia, lakini tofauti ya hapo tuwape wa ‘private’ (binafsi).
“Maana tukiendelea kuwa sisi kama Serikali kuendesha maana yake ni kwamba zile huduma zitaendelea kuwa za hovyo ni kwamba ‘forgery’ (kughushi) nyingi zitaendelea kufanyika kutokana na zile bima za afya, nadhani haiwezi kusaidia,” amesema.
Hata hivyo, Manyinyi tofauti na ilivyokuwa wakati Shabiby akichangia, leo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesimama bungeni kumpa taarifa kuhusiana na hoja yake hiyo.
“Mheshimiwa Naibu Spika (Mussa Azan Zungu) pamoja na mchango mzuri wa mheshimiwa mbunge (Manyinyi), napenda nimpe taarifa tunavyo vituo vya kutoa huduma za afya vinavyomilikiwa na Serikali ambavyo vinatoa huduma bora kuliko huko ‘private’ (binafsi) na hapa nataka kusema aende Muhimbili akaone mapinduzi makubwa chini ya Profesa Mohamed Janabi.
“Kwa hiyo kuwa sasa hivi Serikali tunajikita katika kuzingatia kuimarisha usimamizi wa utoaji huduma za afya katika ngazi zote,” amesema Mwalimu.
Hata hivyo, Manyinyi amekataa kuipokea taarifa hiyo akisema; “mheshimiwa Naibu Spika, mimi taarifa ya mheshimiwa Waziri siipokei kwa sababu gani, yaani ni hivi, yaani leo ukienda pale Musoma (Mkoani Mara), ukitembelea zahanati, ukitembelea vituo vya afya, mjamzito akienda kujifungua pale ni pesa,” amesema Manyinyi na kukatishwa na Naibu Spika kwa kuwa muda wake wa kuchangia ulikuwa umekwisha.
“Mheshimiwa Manyinyi una hoja mwandikie waziri, kwa sababu sasa unachukua muda wa mchangiaji mwingine,” amesema Naibu Spika Zungu.
Alichosema Waziri Mkuu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye hotuba yake kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/2025, alitaja mafanikio katika sekta ya afya.
“Serikali imeendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ambapo hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umefikia wastani wa asilimia 81 katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma za afya ambapo kwa zahanati imefikia asilimia 77, vituo vya afya asilimia 71, hospitali za halmashauri asilimia 73, hospitali za rufaa za mikoa asilimia 99 na hospitali za rufaa za kanda, maalumu na Taifa asilimia 86,” amesema.