Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hamahama Chadema, makosa ya Mbowe au wahamaji

Muktasari:

  • Yamekuwapo madai mengi kuhusu sababu za wabunge wa Chadema kuhama chama hicho na kwenda CCM.
  • Baadhi wakisema kumuunga mkono Rais na wengine kumshutumu Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Ukweli wa sababu hizi unajibiwa na hali ya chama kwa sasa.

Aliyekuwa mbunge wa Serengeti (Chadema), Marwa Chacha ametimiza idadi ya wabunge wanne wa Chadema ambao wamehama chama hicho tangu Godwin Mollel wa Siha, alipofanya hivyo Desemba mwaka jana.

Mollel alihamia CCM, akagombea ubunge na kushinda tena. Sasa ni mbunge wa jimbo hilohilo kwa CCM. Wengine waliojiuzulu ni wawili kutoka CUF – Maulid Mtulia (Kinondoni) na Zuberi Kuchauka (Liwale). Mtulia tayari ni mbunge wa jimbo hilohilo kwa tiketi ya CCM, Kuchauka amepitishwa na CCM kutetea jimbo hilo kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika Jumamosi ijayo.

Ni kipindi cha miezi 10, kinachoshuhudiwa Chadema na upinzani kwa ujumla wakipoteza kila uchaguzi mdogo. Tangu uchaguzi wa ubunge kwenye majimbo ya Longido, Singida Kaskazini na Songea Mjini, Januari 13, mwaka huu, uliosusiwa na Chadema, NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo, CCM wameendelea kuwa wababe kwenye kila uchaguzi, licha ya malalamiko kibao.

Kimahesabu, ndani ya miezi hiyo 10, Chadema imepoteza majimbo sita. Longido, aliyekuwa mbunge wa chama hicho, Onesmo ole Nangole ushindi wake ulitenguliwa na mahakama na uchaguzi ulipofanyika Chadema haikushiriki. Buyungu, Kasuku Bilago alifariki dunia na waliposhiriki waliambulia patupu.

Katika majimbo manne, wabunge wa Chadema wamehamia CCM, Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli), Mollel (Siha) na sasa Chacha (Serengeti).

Kila mbunge aliyehama Chadema na kujiunga na CCM, amepata mbeleko ya kihistoria kwa kupitishwa kugombea bila mchakato wa kura za maoni na baadaye kutangazwa mshindi. Mollel, Kalanga na Waitara ni wabunge tayari kupitia CCM, bila shaka na Chacha naye muda ujao atarejea bungeni kwa tiketi ya CCM. Muda utazungumza.

Tuachane na hoja yenye mshangao mkubwa, kwamba kila mwenye kuhama sababu yake ni kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli kuleta maendeleo. Ipo hoja inayosambaa kwamba Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amechoka au amekaa muda mrefu kuongoza chama hicho, ndiyo maana wabunge wanahama.

Siwezi kupinga maoni ya wengine, huenda wana sababu nyingi, lakini hili la wabunge na madiwani kuhama unamshutumu vipi Mbowe kuwa ameshindwa kuwazuia. Mtu ambaye ni kiongozi kabisa, mbunge au diwani, asubiriwe Mbowe aje amzuie kuhama?

Ukifuatilia wenye kuhama sasa, wao mwenyewe mwanzoni waliwaponda wenzao waliohama kabla yao. Mfano, Chacha na Waitara kuna uthibitisho wa sauti na maandishi, wakisema kuwa wenye kuhama walinunuliwa kwa fedha. Siku zinafuata, hao waliowatuhumu wenzao kununuliwa nao wanahama, kisha wanatoa sababu ya kuhama yenye kufanana na waliowatangulia. Kosa la Mbowe ni lipi?

Hoja nyingi za wenye kuhama ni kwamba wanafanya hivyo ili kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kuwaletea wananchi maendeleo. Hapo Mbowe kosa lake nini? Akazuie Rais Magufuli kuonyesha hizo juhudi?

Awazibe masikio wabunge na madiwani ili wasione hizo juhudi? Mbowe hana Serikali, ni mwenyekiti wa chama cha upinzani na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Kazi yake kuona na kuyasema makosa ya Serikali.

Wabunge na madiwani wenye kuhama si watoto wadogo, kusema hawajui gharama za uchaguzi. Wanajua. Wanafahamu hasara ambayo nchi inapata kwa uamuzi wao wa kujiuzulu ubunge na kugombea tena.

Wanajua kazi waliyoomba kwamba ni uwakilishi wa wananchi na kusimamia Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Watu hao wanapoamua kumuunga mkono Rais badala ya kumsimamia, kosa la Mbowe linakuwa lipi?

Mbowe na Chadema

Kwanza ni muhimu kumpongeza Mbowe. Chadema ni chama kikubwa sasa. Hakikufikia kuwa kikubwa kwa mtelezo wa kukanyaga ganda la ndizi, hapana! Kazi kubwa imefanyika. Uwekezaji mkubwa ulifanywa. Mipango na mikakati mingi ilitungwa na kutekelezwa.

Chadema kilivumilia kuwa nyuma ya NCCR-Mageuzi na CUF, kati ya mwaka 1995 na 2000, kikawa nyuma ya CUF kuanzia mwaka 2000 mpaka 2010. Ukipiga hesabu kuanzia kuanzishwa kwake mwaka 1992, unapata jawabu kuwa Chadema kimevumilia kwa miaka 18, kikionekana si tishio dhidi ya CCM.

Miaka 18 ni mingi. Inatosha mtoto kuzaliwa, kukua na kufikisha umri wa kupiga kura. Ni umri unaomtambulisha Mtanzania kama mtu mzima. Ni umri usio na kipingamizi kwa Mtanzania kuanza majukumu ya kifamilia, ndoa na uzazi.

Chadema ilivumilia, maana katika miaka 18 ilipita kipindi cha kuongozwa na wenyeviti watatu, Edwin Mtei, Bob Makani kabla ya Mbowe. Kikawa na makatibu wakuu watatu, Bob Makani, Dk Aman Kaborou na Dk Willibrod Slaa.

Utaona pasipo shaka kwamba Chadema walibadili silaha tofauti kufikia kukaa kwenye mkondo ambao wapo kwa sasa. Mkondo wa kutambulika kama chama kikuu cha upinzani Tanzania.

Hata kabla ya kufikia kuwa chama kikuu cha upinzani, viongozi wake akina Mtei na Makani, walikijenga chama katika msingi wenye kuheshimika. Hakikuwahi kuonekana kuwa chama cha hovyo.

Chadema ni chama ambacho hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikiwashia taa ya kijani. Katika moja ya mikutano ya kampeni kumwombea kura Benjamin Mkapa wakati akiwania urais mwaka 1995, alikibariki Chadema.

Ilikuwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya siasa, Nyerere alisema kuwa Sera za Chadema ni nzuri na kinaweza kupewa hata uongozi wa mamlaka ya Jiji la Dar es Salaam, lakini siyo nchi kwa kile ambacho alikisema kuwa wakati huo wapinzani walikuwa bado wachanga.

Leo hii Meya wa Jiji la Dar es Salaam ni Chadema lakini CCM bado kinaongoza nchi. Maana yake mdomo wa Mwalimu Nyerere umetimiza alichokitamka. Zingatia, wakati huo Chadema hakikuwa tishio, ila kilikuwa chama kizuri.

Ukuaji wa Chadema

Heshima kwa Mtei na Makani maana waliiasisi na kuiongoza Chadema katika nyakati za unyonge, kwa ruzuku duni, bila kuwa na wabunge wengi. Hata hivyo, ukifika kwa Mbowe, unapaswa kupiga saluti kwake.

Vema kukiri mambo mawili au mojawapo. Mosi, Mbowe anazijua siasa za nchi hii na kufahamu tabaka lenye nguvu kisiasa. Pili, ana akili na maarifa mengi ya kuteka tabaka husika.

Mbowe baada ya kushika uongozi wa Chadema, alitambua kuwa ushiriki wa vijana kwenye siasa za nchi ulikuwa mdogo. Alitambua pia kuwa ukiwa na chama ambacho ni kivutio cha vijana hapo umeua.

Sijawahi kuketi na Mbowe akanisimulia chochote, isipokuwa najaribu kuzisoma fikra zake na kuelimika kupitia vitendo vyake na kila hatua alizochukua. Aliamua kuwekeza kwa vijana na matokeo yakaonekana.

Mbowe aliamua kutengeneza nadharia na falsafa za uwekezaji wa chama kwa vijana vyuoni. Kati ya mwaka 2003 na 2005, Chadema kilipitia mabadiliko kutoka kuwa chama chenye taswira ya kujengwa na wazee na kugeuka chama cha vijana wa kizazi kipya cha siasa.

Mwaka 2005, Mbowe aligombea urais, pamoja na kutoka wa tatu, nyuma ya Rais wa nne, Dk Jakaya Kikwete na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, hatua hiyo ilipiga mstari kwa sababu ilikuwa mara ya kwanza kwa Chadema kugombea urais.

Ni baada ya mwaka 2005, Chadema ikapata wabunge watano wa kuchaguliwa na sita wa viti maalumu. Uwepo wa wabunge hao, ulitengeneza ‘amshaamsha’ ya kisiasa kwa vijana.

Aliposimama Zitto Kabwe, alikuwa kivutio na kila mtu alitaka kumwona na kumsikia akijenga hoja bungeni. Zamu ya Chacha Wangwe (marehemu) ilikuwa ya mshikemshike kati yake na Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta (marehemu). Wangwe hakuwahi kuwa na sifa ya woga na alikufa akiwa si mwoga.

Vijana wanawake, Halima Mdee na Mhonga Ruhanya. Ubishi wa Halima ukamfanya akawa kivutio cha wanawake wengine wengi kuipenda Chadema. Ongezea Anna Komu, Lucy Owenya, Suzan Lyimo na Grace Kiwelu.

Timu ilikamilishwa na Ndesa Pesa, Philemon Ndesamburo kisha kiongozi wa timu, mtu mwenye dakika zake za thamani bungeni, Dk Slaa, ambaye kila aliposimama, hujuti kumtazama kwa hoja zake.

Haiba ya Zitto ilikuwa kishawishi cha vijana wengi zaidi kukimbilia Chadema. Wakati huo, tayari John Mnyika alikuwa akifanya vizuri nje ya Bunge. Hiyo ndiyo Chadema yenye thamani. Hiyo ndiyo Chadema iliyokuwa na sababu nyingi za kuchukua uongozi wa Kambi ya Upinzani baada ya Uchaguzi Mkuu 2010.

Kabla ya kuanza 2010 na kuja 2018, hapa naomba nitamke kuwa yeyote ambaye anaweza kukosa adabu kwa Mbowe juu ya siasa za nchi hii, na kwa hatua ambayo tumefikia, huyo ni zuzu. Upinzani siyo kupingana na ukweli.

Ukiona anatokea mtu anamtusi Mbowe au anamtaja kwa namna yoyote bila adabu, huyo hayuko vizuri kichwani au ana sababu anazozijua yeye. Unaweza kumpinga na kumkataa mtu ukiwa unamheshimu. Mbowe anastahili heshima kubwa kwa mahali alipoitoa Chadema mpaka alipoifikisha.

Kama tunawaheshimu watu wengi kwa historia, wakianzia sifuri au padogo hadi kufikia pakubwa, unaweza vipi kuacha kumpa heshima Mbowe? Tena hiyo heshima si kwa kuombewa, anastahili na apewe. Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.

Hata hivyo, ushauri lazima utolewe. Na Mbowe lazima aupokee. Maneno yenye kusemwa na watu japo mabaya kiasi gani, ukiyageuza hasi kuwa chanya, hayakosi faida ndani yake. Chadema ni chama kikubwa, inawezekana Mbowe alimaanishwa kukikuza ili kikifika hatua fulani ili kiongozwe na mtu mwingine wa kukiwezesha kushika dola.

Inawezekana ni miluzi tu ya nje yenye kuamini Mbowe kachoka. Wanasema miluzi mingi kumpoteza mbwa. Anatakiwa abaki kwenye mstari na akiongoze chama chake kufikia malengo kusudiwa. Wabunge na madiwani kuhama ni upepo, tena ni makosa zaidi ya wahamaji wenyewe. Mbona wanaohama CUF makosa habebeshwi mtu mwingine? Mbowe hawezi kuhukumiwa kwa uhamaji wa wabunge na madiwani.