Fahamu umuhimu wa lishe ya mbogamboga na matunda

Muktasari:
Mei 21 ya kila mwaka, ulimwengu unaadhimisha siku ya ulaji wa matunda na mbogamboga.
Dar es Salaam. Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya ulaji wa matunda na mbogamboga kila Mei 21, Ofisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Walbet Mgeni amesema ulaji wa vyakula hivyo nchini uko chini kwa sababu watu hawapendi.
Siku hii ilianzishwa kwa lengo la kuhamasisha ulaji wa mbogamboga na matunda ili kuwasaidia watu kukabiliana na magonjwa yasiyoambukia ikiwemo unene uliopitiliza.
Kihistoria, kilimo cha mbogamboga na matunda kilianza zaidi ya miaka 30,000 iliyopita na inaadhimishwa ili kuwalika watu mbalimbali kula kachumbari za matunda na mbogamboga kwa ajili ya afya zao.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Mei 21, 2024, Mgeni amesema takwimu za ulaji wa matunda na mbogamboga ni changamoto, lakini watu hawapendi kula vyakula hivyo kwa kisingizio kuwa mlo huo ni gharama.
“Tunasisitiza watu wale matunda na mbogamboga zilizopo kwenye msimu mfano, huu ni msimu wa machungwa, tunashauri watu wale machungwa ambayo ni gharama nafuu ya Sh100 tofauti na kutaka kula tunda ambalo sio la msimu ambalo lazima gharama zake zitakua juu,” amesema.
Mgeni ameongeza watu hawazingatii hayo, wanatafuta vitu visivyo vya msimu ambavyo ni gharama kubwa, huu mlo wa mbogamboga na matunda ni muhimu kwenye mwili wa binadamu, una vitamini na madini yanayosaidia mwili usipatwe na magonjwa mbalimbali.
Mafua ni moja ya ugonjwa unaochochewa na ukosefu wa matunda na mbogamboga mwilini, hivyo ulaji wa mbogamboga na matunda unasaidia kupandisha kinga ya mwili.
“Kuna muda sahihi wa kula mbogamboga na matunda. Kitaalamu ndani ya saa 24, hakikisha katika mlo mmoja umekula matunda na mwingine umekula mbogamboga, utachagua mwenyewe ule asubuhi, mchana au jioni,” amesema Mgeni.
Ofisa huyo amesema magonjwa yote yanayosababishwa na ukosefu wa vitamini C kama vile kutokwa na damu kwenye fizi, meno kung’oka, kuwa na ngozi kavu, wekundu kwenye vinyweleo, kuchubuka kwa urahisi, kuvimba viungo vyote, yanasababishwa na kutokula matunda na mbogambonga ambayo ndiyo inaongeza vitamin c mwilini.
Akizungumzia faida za matunda na mbogamboga kwenye ngozi: “Ukosefu wa vitamin A katika mwili wa binadamu unasababisha ukavu katika ngozi, kupata vidonda kwenye ngozi, kuwa na uoni hafifu na macho kuwasha, haya yote husababishwa na kutokula mbogamboga na matunda.”
Vyakula vingine vyenye vitamin A ni kama vile maboga, viazi vitamu hasa vya njano, mbogamboga zenye ukijani kwa wingi, lakini pia mahindi ya njano, siagi, samaki, kiini cha yai, figo za wanyama na matunda ya njano kama papai, karoti na maembe.
“Magonjwa mengine yanayosababishwa na ukosefu wa vitamini K inayotokana na mbogamboga na matunda ni damu kutoganda. Kuna watu wengine wakijikata tu damu inatoka kwa wingi bila kuganda, hii moja kwa moja ni upungufu wa vitamini K, ila akila mbogamboga na matunda yenye vitamini K, tatizo litaisha kabisa,” amesema Mgeni.
“Hakikisha unakula matunda na mbogamboga zenye rangi mbalimbali, utofauti wa rangi ndivyo zinavyotofautiana kwenye swala zima la vitamini, hatushauri ulaji wa mboga au tunda hilohilo kila siku , matunda machachu kama vile ukwaju, chungwa, limao ya vitamini kwa wingi,” amesema Mgeni.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Lightness John amesema hana desturi ya kula matunda lakini anapendelea zaidi mbogamboga na juisi tu licha ya kufahamu faida ya matunda katika mwili wa binadamu.
“Hakuna uhaba wa matunda lakini sipendelei kuyala, kwa siku zijazo nitajitahidi kuwa na desturi hiyo kwa afya yangu,” amesema Lightness.
Kwa upande wake, Carlos Banda amesema: “Nina desturi ya kula matunda kila ninapopata muda na kila mlo wangu nahakikisha unakuwa na mbogamboga hasa nikienda mahali kula, lakini ninapokuwa nyumbani ni ngumu kuandaa mlo huo kwa sisi tusio na familia bado.”