ETDCO wakamilisha mradi wa kilovoti 132 Tabora – Ipole

Muktasari:
- Mradi wa Tabora hadi Katavi umegharimu Sh161 bilioni, ambapo awamu ya kwanza umekamilika na wananchi wa Wilaya ya Sikonge watapata megawati 12 kupitia njia mpya ya msongo wa kilovolti 132.
Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imekamilisha ujenzi wa mradi wa laini ya msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilomita 102 kutoka Tabora hadi Ipole. Ikielezwa kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawasaidia wananchi wa Wilaya ya Sikonge kupata huduma ya umeme ya uhakika na kuchochea maendeleo.
Akizungumza leo, Aprili 27, 2025, mkoani Tabora wakati wa kuwasha laini hiyo mpya, Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya ETDCO, Sadock Mugendi amesema kuwa ujenzi wa laini hiyo umekamilika kwa asilimia 100, hivyo wananchi wa Wilaya ya Sikonge watapata umeme wa uhakika.
Mugendi ameishukuru Serikali na Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kuwaamini kutekeleza mradi huo, huku akieleza kuwa wapo hatua za mwisho za kukamilisha kipande cha pili cha kutoka Ipole hadi Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi chenye urefu wa takriban kilomita 133.
Mugendi ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu ya mradi huo kwani, Serikali imetumia gharama kubwa kuutekeleza kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Meneja wa mradi huo kwa upande wa Tanesco, Mhandisi Sospeter Oralo amesema kuwa mradi wa Tabora hadi Katavi umegharimu Sh161 bilioni, ambapo awamu ya kwanza umekamilika na wananchi wa Wilaya ya Sikonge watapata megawati 12 kupitia njia mpya ya msongo wa kilovolti 132.
Amewasihi wananchi wa Wilaya ya Sikonge kutumia umeme huo kama fursa kwa kufanya uwekezaji katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuboresha vipato vyao, huku akisisitiza matumizi ya nishati safi ya umeme majumbani, ambayo inasaidia kupunguza gharama na kuboresha afya na mazingira.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mradi wa Tabora hadi Katavi upande wa ETDCO, Mhandisi Ebenezer Makakala, amesema kuwa wananchi wa maeneo ya mradi wamefaidika kwa kupata fursa ya kufanya kazi kama vibarua wakati wa utekelezaji wake.

Nao, Vibarua wa mradi huo, akiwemo Mateo Daudi, wameeleza shukrani zao kwa Serikali kwa kuleta mradi huo, kwani umekuwa na manufaa makubwa kwao ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kuingiza kipato kilichowasaidia kugharamia mahitaji ya familia zao, ikiwemo kulipa ada za watoto wao.