Erick Kabendera awaliza nduguze mahakamani.

Mwandishi wa habari Erick Kabendera akiwa katika Mahakama ya Hakim Mkazi Kisutu katika shauri linalomkabili la utakatishaji. Picha na Omar Fungo
Muktasari:
Kesi inayomkabili mwandishi wa habari nchini Tanzania, Erick Kabendera imeshindwa kuendelea baada ya upelelezi wa mashtaka yanayomkabili kutokamilika. Katika chumba cha mahakama Erick aliwatoa machozi ndugu, jamaa na marafiki baada ya kuingia mahakamani ikiwa ni siku tatu zimepita tangu mama yake mzazi, Verdiana Mujwahuzi (80) kufariki dunia.
Dar es Salaam. Wakati upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwandishi wa habari wa Tanzania, Erick Kabendera ukieleza kuwa upelelezi wa shauri bado haujakamilika.
Ndugu wa mshtakiwa huyo waliofurika kwa wingi katika Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo Alhamisi Januari 2, 2020 walionekana kulia baada ya kumuona ndugu yao.
Ndugu hao walikuwa wanalia muda mfupi baada ya mshtakiwa huyo kuingizwa katika Mahakamani ya wazi namba moja, kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.
Msingi wa vilio hivyo, unatokana na mshatakiwa huyo kufiwa na mama yake mzazi, Verdiana Mujwahuzi Jumanne ya Januari 31, 2019 katika Hospitali ya Rufaa Amana, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Mwili wa Verdiana (80) utaagwa kesho Ijumaa katika Kanisa Katoliki Chang’ombe, Temeke jijini Dar es Salaam kisha utasafirishwa kwenda Bukoba mkoani Kagera kwa maziko yatakayofanyika Januari 6, 2020.
Hata hivyo, wakati ndugu hao wakilia kimya kimya na kujifuta machozi, Kabendera alionekana naye, akifuta macho mara kwa mara, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa ndani ya Mahakama hiyo kabla ya kesi hiyo kuanza kusikiliza.
Hata kesi hiyo ilipoahirishwa kwa muda, ndugu hao walionekana kulia chini chini na kujifuta.
Mbali na ndugu waliohudhuria kesi hiyo, pia Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe alikuwapo mahakamani hapo.
Kabendera anakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kutakatisha fedha kiasi cha Sh 173milioni.
Mashtaka mengine ni kupanga genge la uhalifu wa mtandao na ukwepaji kodi zaidi ya Sh173 milioni.
Mshtakiwa huyo alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, Agosti 5, 2019.
Hata hivyo, leo Januari 2, 2020 wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.