Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DPP amfutia kesi raia wa Uturuki, Polisi yamdaka tena

Muktasari:

  • Gurses anakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh328 milioni kwa madai kuwa kampuni yake imesajiliwa kufanya kazi za ujenzi, wakati akijua kuwa ni uongo.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) amemfutia kesi raia wa Uturuki, Ugur Gurses, aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu zaidi ya Sh328 milioni.

Gurses ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya ujenzi ya Adamas Conglomerates Company Limited, anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa madai kampuni yake imesajiliwa na inaweza kufanya kazi za ujenzi jengo la NSB, lilipo Masaki jijini Dar es Salaam huku akijua kuwa si kweli.

Mshtakiwa huyo amefutiwa mashtaka yake leo Julai 2, 2025 baada ya DPP kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yake.

Mshtakiwa huyo amefutiwa shtaka lake chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Juni 18, 2025 na kusomewa mashtaka yake na leo kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa.

Uamuzi wa kumwachia huru mshtakiwa huyo, umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo.

Awali, wakili wa Serikali, Titus Aron alidai kuwa DPP, amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya mshtakiwa.

Wakili Aron baada ya kueleza hayo, Hakimu Nyaki alisema kupitia kifungu hicho, mahakama inamfutia mashtaka mshtakiwa hayo.

 Adakwa tena na Polisi

Baada ya kutoka katika chumba cha Mahakama, mshtakiwa alikamatwa na askari Polisi waliokuwepo mahakamani hapo na kumpelekwa Kituo cha Polisi.

 Hati ya mashtaka

Mshtakiwa anadaiwa kati ya Desemba Mosi 2023, na Mei 5, 2024, Dar es Salaam, akiwa na watu wengine ambao hawajafikishwa mahakamani hapo, kwa nia ovu, waliongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh328.5,52 milioni pamoja na dola za Marekani 16,000 sawa na Sh41 milioni kutoka NSD Holding Capital &Consaltance Limited.

Shtaka la pili, siku na eneo hilohilo, mshtakiwa huyo akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya ujenzi ya Adamas Conglomerates Company Limited, kwa uongo, alijipatia kiasi hicho cha fedha.

Ilidaiwa kuwa walijipatia fedha hizo baada ya kudanganya kampuni hiyo imesajiliwa na inaweza kufanya kazi za ujenzi jengo la NSB kitalu namba 1055 Hyleslas Road, iliyopo Masaki wakati akijua si kweli.

Shtaka la tatu, ilidaiwa, katika tarehe hizo, jijini Dar es Salaam alitakatisha kiasi hicho cha fedha ,huku akijua zilitokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kwa muda wote huo alikuwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili kutokuwa na dhamana.