Jalada kesi ya anayedaiwa kujifanya Polisi, kwenda Uturuki kununua silaha lipo kwa DPP

Muktasari:
- Maulid anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 26, 2024 katika ofisi za Suma JKT, Jijini Dar es Salaam, ambapo alijitambulisha kwa Kepteni Cheo kuwa yeye ni askari Polisi, wakati akijua kuwa ni uongo.
Dar es Salaam. Jalada la kesi ya kujitambulisha kuwa askari polisi inayomkabili mfanyabiashara, Msafiri Maulid (48) lipo ofisini kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kupitiwa na kutolewa uamuzi.
Hayo yameelezwa na Wakili wa Serikali, Frank Rimoy mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatatu, Juni 23, 2025 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali baada ya upelelezi kukamilika.
Maulid, maarufu kwa jina la Msafiri Mahita mkazi wa Mbezi Juu, Dar es Salaam, anadaiwa kutenda kosa la kujitambulisha kwa kapteni wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuwa ni askari polisi na kisha kuongozana na maofisa wa jeshi hilo kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya ununuzi wa silaha, wakati akijua kuwa ni uongo.
“Leo kesi hii imeitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali, lakini jalada la kesi liko ofisini kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa ajili ya kupitiwa na kutolewa uamuzi. Hivyo, tunaomba Mahakama ipange tarehe nyingine,” amesema Wakili Rimoy mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.
Baada ya kauli hiyo, Wakili wa Utetezi, Aloyce Komba akaiambia Mahakama kuwa hana pingamizi kuhusu maelezo hayo.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Hakimu Lyamuya ameiahirisha kesi hiyo hadi Julai 16, 2025, wakati mshtakiwa atakaposomewa hoja za awali.
Hata hivyo, mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.
Katika kesi ya msingi, Maulid anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 26, 2024, katika ofisi za Suma JKT jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa siku hiyo, mshtakiwa huku akijua si askari polisi, alijitambulisha kwa Kapteni Leslie Cheo kuwa ni askari polisi jambo alilojua ni uongo.
Baada ya utambulisho huo, anadaiwa kushiriki kwenye mchakato wa ununuzi wa silaha na kusafiri hadi Uturuki akiwa pamoja na maofisa wa Suma JKT, ambako walikamilisha ununuzi wa silaha hizo.