Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DC Same aagiza Takukuru kuchunguza mradi wa maji wa Sh1 bilioni

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Vumari, wilayani humo.

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) wilayani humo kufanya uchunguzi kuhusu mradi wa maji wa Sh1 bilioni uliokuwa ukitekelezwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) katika vitongoji 7 vya Kata ya Vumari.

Same. Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni  ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) wilayani humo kuchunguza mradi wa maji wa Sh1 bilioni uliokuwa ukitekelezwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) katika vitongoji 7 vya kata ya Vumari.

 Amesema vitongoji viwili pekee kati ya 7 ndiyo vyenye uhakika wa maji huku vitongoji vingine 5 vikiwa havina maji kabisa na kupelekea wananchi kupata adha ya maji ilhali Serikali imetoa fedha za kutosha ili wananchi waweze kunufaika na miradi hiyo ya maji.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa maagizo hayo, wakati alipokwenda kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa wilayani humo, ikiwemo miradi ya maji, ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Mbono unaotekelezwa  na mradi wa Boost utakaogharimu Sh181 milioni.

"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan  amejitahidi kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo hii ya maji ambayo ametoa Sh1bilioni kwa ajili ya ukamilishwaji katika katika vitongoji hivi 7 lakini kwenye usimamizi wa miradi hii kuna changamoto, na wananchi wanashindwa kunufaika na hii miradi," amesema.

"Takukuru naomba mfuatilie na kuchunguza hili, tujue ni kitu gani kinachofanya  wananchi hawa wa vitongoji vitano wasinufaike na miradi hii ya maji na ni kwanini maji hayawafikii wananchi wa vitongoji hivi vitano wakati serikali ilishatoa fedha siku nyingi kwa ajili ya mradi huu wa maji katika vitongoji hivi," amesema.

Pamoja na mambo mengine, ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo na kusema wataendelea kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali zinatumika vyema kwa kutekeleza miradi iliyokusudiwa.

Akizungumzia kukosekana kwa maji katika vitongoji hivyo vitano, Meneja wa Ruwasa wilayani humo, Abdalah Jendaeka alisema mradi huo ulimalizika muda mrefu na kwamba changamoto iliyojitokeza ni kwamba wananchi hawatunzi miundo mbinu ya maji ambapo baadhi ya wananchi waliharibu miundo mbinu hiyo ya maji.

"Mkandarasi alishamaliza kazi yake na mradi ulishakamilika, changamoto iliyojitokeza ni kwamba wananchi waliharibu miundombinu ya maji na kuharibu baadhi ya vifaa ambayo vilikuwa vikitumika katika miradi hiyo," amesema.

Asha Abdallah na Herman Mgonja ambao ni wananchi wa kata ya Vumari, wilayani humo wamesema upatikanaji wa maji katika kata hiyo imekuwa ni changamoto kubwa hasa wakati wa kipindi cha kiangazi ambapo wanalazimika kunywa maji yasiyosafi na salama.