Chama cha Wagumba chaibukia tamasha la jinsia Dar

Muktasari:
- Tamasha la Jinsia linaendana sambamba na miaka 30 ya kuanzishwa kwa mtandao TGNP
Dar es Salaam. Chama cha Wagumba na Tasa chaibukia tamasha la jinsia linaloendelea katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia (TGNP), Mabibo jijini humo.
Tamasha hilo la siku nne, limewakutanisha wadau mbalimbali wanaopigania haki za usawa wa kijinsia ndani na nje ya nchi lengo likiwa kupata fursa ya kutafakari mafanikio, changamoto, mambo waliojifunza pamoja na kubadilishana uzoefu ambapo pia kuna mijadala na midahalo ya mada mbalimbali inafanyika.
Wakati tamasha hilo linaendelea, Mwenyekiti wa chama hicho cha wagumba na tasa, Shamila Makwenjila, aliweza kuibukia katika mdahalo uliobeba mada ya 'miaka 30 baada ya mkutano wa Beijing, zipo wapi fedha kugharamikia uratibu na mabadiliko endelevu ya Haki za wanawake' uliokuwa ukiendeshwa na mwanzilishi wa Women Fund Trust, Marry Rusimbi.
Wakati tamasha hilo linaendelea, Mwenyekiti wa chama hicho cha wagumba na tasa, Shamila Makwenjila, alielezea kuhusu kundi hilo, ambapo amedai kuwa wanachama wake wanaonekana kutothaminiwa kuanzia ngazi ya familia, kwenye vyombo vya sheria na jamii kwa ujumla.
"Hivyo tunaumia, tunanyanyasika, hatuna sehemu ya kupaza sauti zetu, hivyo nimeona nije kwenye tamasha hili ili watu wajue tupo na kuona namna gani wanaweza kutusaidia kujikwamua na haya tunayopitia,” amesema na kuongeza;
"...huko vijijini ndio balaa, watu hawa wanashindwa hata kujikwamua kiuchumi kutokana na kutothaminika kwenye jamii, hivyo tunaomba mashirika wahisani wanapotoa fedha walifikirie na kundi hili pia.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mfuko wa Mashirika ya Watetezi wa Haki za Wanawake, Wasichana na Watoto (Women Fund Tanzania Trust), Rose Marandu, mesema mjadala huo ulikuwa unaangazia makundi yote ya kuanzia ngazi ya taifa mpaka ngazi ya jamii na makundi yaliyo pembezoni.
"Tunaangalia makundi haya je tangu yameanza kufanya kazi ya utetezi kuanzia wakati ule wa Beijing ambapo makundi mengi yalipata ulingo na kiringe cha kuongea...hata sisi tumeona ni makundi ambayo bado yapo pembezoni na hayajafikiwa katika kuleta usawa wa kijinsia ikiwemo hili la wenye ugumba na utasa,” amesema na kuongeza;
"...kupitia mwenyekiti wao tumeweza kusikia sauti zao kwa sababu sisi kama watetezi wa wanawake sauti za kila kila mtu ni muhimu kuzisikiliza na kuweza kuweka nguvu ya pamoja kupaza sauti zao."
Naye Jane Magigita kutoka Shirika la Equality for Growth (EfG), amesema amefarijika kuona watu wanaopitia changamoto hizo za ugumba na utasa wanajitokeza mbele ya jamii na kuahidi kuwakutanisha na mashirika yanayotetea haki za wanawake ikiwemo ya kisheria kuona namna gani watasaidiwa.
Kwa upande wake Agnata Rutazaa kutoka Shirika la Tusonge la mkoani Kilimanjaro, ametaka masuala ya sera kuwekwa pembeni na kuzingatia zaidi mahitaji ya watu.
Deo Bwire kutoka Shirika la Msaada wa Kisheria (LSF), amesema katika kuyajadili hayo kuna haja pia ya kuangalia nafasi ya Serikali kwani wamekuwa wakitoa ahadi ambazo utekelezaji wake ni hafifu.
"Kwani hata Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu ambayo inayosimamia makundi hayo, bajeti yake bado ni ndogo ukilinganisha na kazi wanazotakiwa kufanya,” amesema Bwire.