TGNP: Teknolojia itumike kama chachu kuimarisha usawa wa kijinsia

Mkufunzi kutoka Tassisi ya Teknolojia Dar Es Salaam(DIT),Nizietha Kimario(wa pili kulia) akiwa na Mtaalam wa masuala ya jinsia Deogratius Temba na baadhi ya wanafunzi wa DIT, katika Wiki ya Azaki inayoendelea Arusha. Picha na Janeth Mushi
Muktasari:
- Wadau wanatakiwa kuondoa hofu ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika utendaji wa majukumu ya kila siku na badala yake wanapaswa kuhakikisha teknolojia haitumiki vibaya na hivyo kuongeza ukatili na udhalilishaji wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto.
Arusha. Ubunifu na teknolojia zinatajwa kuwa miongoni mwa nyenzo muhimu na zinazopaswa kutumika kama chachu ya kuimarisha usawa wa kijinsia.
Aidha wadau wametakiwa kushirikiana kuhakikisha teknolojia haitumiki vibaya kuongeza ukatili na udhalilishaji wa kijinsia au kuongeza tofauti za kiuchumi kati ya mwanamke na mwanaume.
Hayo yameelewa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Ushawishi na Utetezi toka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Florah Ndaba, wakati akichangia katika mjadala wa ubunifu na teknolojia kama chachu ya usawa wa kijinsia ambao umeenda sambamba na wiki ya Azaki jijini Arusha.
Akizungumza katika mjadala huo ambao umewashirikisha wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi, Serikali, asasi za kiraia, katika Wiki ya Azaki inayoendelea jijini Arusha, Ndaba amesema jamii haipaswi kuogopa wala kuwa na hofu juu ya ukuaji wa teknolojia.
Amesema wadau wanatakiwa kuondoa hofu ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika utendaji wa majukumu ya kila siku, hata hivyo, wanapaswa kuhakikisha haitumiki vibaya na hivyo kuongeza ukatili na udhalilishaji wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto.
“Teknolojia, inapunguza gharama za utendeshaji na uzalishaji, ndio maana TGNP tuliingia makubaliano na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), kusaidiana katika kuendeleza na kuhakikisha jitihada za ubinifu wa kisayansi zinazofanywa na taasisi hiyo, zinazingatia usawa wa kijinsia,” amesema na kuongeza,
“...katika makubaliano hayo, pia wasichana wanaochagua fani za sayansi na teknolojia wanapata nafasi na kulelewa vipaji vyao hadi waingie kwenye soko la ajira.”
Mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya kijinsia, Deogratius Temba, amesema kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika teknolojia kunaikosesha nchi fedha nyingi ambazo zingepatikana kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji.
Amesema kutokana na hilo ni wazi kuwa usawa wa kijinsia kwenye eneo la sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati hauepukiki.
Mtaalamu huyo amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na UNWomen kwa nchi 51 mwaka 2022, umeonyesha kwamba nchi za uchumi wa chini na kati ambazo hazina usawa wa kijinsia katika teknolojia zinapoteza Dola za Marekani trilioni moja kila mwaka na ifikapo mwaka 2025 zitapoteza 1.5Trilioni.
Mkufunzi kutoka DIT, Nizentha Kimario, amesema wamekuwa na mtazamo wa kijinsia na kwamba uhusiano wa taasisi hiyo na TGNP umesaidia kujenga uelewa wa masuala hayo na kubadili mitazamo hasi juu ya uwezo wa wasichana katika fani za sayansi na teknolojia.
“Lakini pia wanafunzi wanaona umuhimu wa kwenda kwenye jamii kuangalia changamoto na mahitaji yao kabla ya kuanza kufanya ubunifu na utaona kwamba mashine nyingi za kibunifu zimetokana na mahitaji ya jamii," amesema na kuongeza;
“Wanafunzi wetu baada ya kuona kuna changamoto ya gharama kubwa ya kwenye kutunza na kuwawekea dawa watoto wenye changamoto ya upumuaji hasa asthma, ndio maana vijana wetu tena wasichana wamebuni hii mashine.”
Mbali na mjadala huo, wanafunzi kutoka DIT walionesha mashine mbalimbali ambazo zimebuniwa na wanafunzi wake ikiwemo pikipiki ya magurudumu matatu (bajaji) yenye uwezo wa kubeba watu saba ambayo inatumia nishati ya umeme betri ambayo huchajiwa.