Azaki, waandishi wa habari wakutanishwa kujenga mahusiano

Muktasari:
Waandishi wa habari na Asasi za Kiraia ( CSOs) zimekutanishwa jijini Mwanza kufundwa na kujadili namna bora ya kushirikiana katika utendaji kazi ili kuibua changamoto na fursa kwa ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Mwanza. Waandishi wa habari na Asasi za Kiraia ( CSOs) zimekutanishwa jijini Mwanza kufundwa na kujadili namna bora ya kushirikiana katika utendaji kazi ili kuibua changamoto na fursa kwa ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa warsha ya siku mbili iliyokutanisha makundi hayo mawili leo Jumatatu Septemba 4, 2023; Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Internews nchini, Agnes Kayuni amesema mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na USAID yataleta umoja baina ya waandishi wa habari na Asasi za Kiraia katika kutekeleza majukumu yao.
“Ni muhimu kwa haya makundi mawili kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja. Natumaini kukutana huku kutatuleta umoja na kujenga mahusiano makubwa mbeleni,”amesema
Katika mafunzo hayo yanayoratibiwa na Internews Tanzania kupitia mradi wa Boresha Habari na kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari wa kupinga vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (Ojadact), washiriki wamepata fursa ya kuchangia sababu zinazowafanya kutofanya kazi kwa ukaribu zaidi na namna ya kuzikabili.
Mwenyekiti wa Ojadact, Edwin Soko amesema vyombo vya habari na CSOs vikiwekwa pamoja nakuwa na ukaribu vitaboresha maisha ya watu na jamii.
“Changamoto zipo kwa sababu kuna wakati unaweza kukuta azaki zinawatumia waandishi wa habari kwenye shuguli tu na hii inaleta mapungufu makubwa sana kwa sababu inabidi mwandishi afahamu taasisi inajikita na nini na inatetea nini ili aweze kuandika in details (kwa undani),”amesema
Mshiriki wa mafunzo hayo, Neema Emmanuel ameishukuru Internews kwa kutambua umuhimu wa waandishi wa habari na vyombo vyao kuwa na ushirikiano wa karibu na asasi za kiraia kwakuwa kwa namna moja ama nyingine wote wapo kwenye mrengo mmoja wa kuhakikisha wanaibua na kutetea maslahi ya wananchi.