Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Azaki zakumbushwa kushiriki uboreshaji elimu

Muktasari:

  • Juma la elimu limezinduliwa mkoani Morogoro, ambapo asasi za kiraia zimekumbushwa wajibu wa kuchangia juhudi za Serikali katika kuboresha elimu.

Morogoro. Asasi za Kiraia zimetakiwa kutimiza wajibu wake wa kuchangia juhudi za Serikali katika utoaji na uboreshaji wa huduma za kijamii hasa elimu.

 Juhudi hizo ni pamoja na kupanga mikakati endelevu ya kuondoa kabisa changamoto za uhaba wa madarasa, walimu, miundo mbinu ya wanafunzi wenye ulemavu, mabweni, madawati, vyoo vya wanafunzi na walimu na nyumba za walimu.

Wito huo umetolewa leo Aprili 17 na Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) Ochola Wayoga wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya juma la elimu yaliyofanyika katika kata ya Mvuha mkoani Morogoro.

Maadhimisho hayo yamebebwa na kauli mbiu ‘Tuwekeze rasilimali za ndani kwenye elimu kwa maendeeo endelevu’ inayolenga kuukumbusha umma umuhimu wa juhudi za pamoja za wadau wa elimu ikiwemo Serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla katika kuendeleza elimu.

Wayoga amesema ni muhimu kwa asasi za kiraia kushirikiana na Serikali katika kuihamasisha wanajamii ili watambue na kuona umuhimu wa uwekezaji kwenye elimu.

“Baadhi ya sababu zilizopelekea kamati kuichagua Morogoro DC ni pamoja na kuwepo kwa uhitaji na changamoto za uhaba wa madarasa, walimu, madawati, vyoo vya wanafunzi, miundo mbinu ya wanafunzi wenye ulemavu, mabweni na walimu,” amesema Wayoga.

Akifungua maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Rebeca Nsemwa amesema licha ya ukweli kwamba Serikali

ina jukumu la kutoa huduma za jamii na hasa elimu bora haiwezi kufanya kila kitu peke yake.

“Ni ukweli kwamba nchi yoyote ili iendelee inahitaji kuwekeza kwenye elimu bora ili kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo ni lazima itolewe kwa usawa wa kijinsia na jumuishi na kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wanafunzi.

“Kufikia lengo la kuwa moja kati ya nchi za kipato cha kati, hakuna budi Taifa kuwekeza katika elimu kwa watu wake kwa ajili ya kupata rasilimali watu ambayo ndiyo injini ya kuleta mabadiliko,” amesema Rebeca.

Mkuu huyo wa wilaya amesema sehemu muhimu ya kuanzia kuwekeza katika rasilimali watu ni kuanzia elimu ya awali na msingi kwa watoto wote bila kuwaacha nyuma watoto wa kike.