Tamasha la Jinsia kuwakutanisha washiriki 1,500 Dar

Muktasari:
- Washiriki Zaidi ya 1,500 kutoka ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam wanatarajiwa kushiriki Tamasha la Jinsia litakaloenda sambamba na maadhimsho ya miaka 30 ya Mtandao wa Jinsi Tanzania (TGNP).
Dar es Salaam. Washiriki Zaidi ya 1,500 kutoka ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam wanatarajiwa kushiriki Tamasha la Jinsia litakaloenda sambamba na maadhimsho ya miaka 30 ya Mtandao wa Jinsi Tanzania (TGNP).
Tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 7 hadi 10 mwaka huu litabebwa na kauli mbiu isemayo ‘Miaka 30 ya TGNP na Tapo la Ukombozi wa Wanawake.’
Hayo yamesemwa leo Septemba 2 na Ofisa Habari wa Mtandao wa Jinsia TGNP, Monica John, katika warsha ya waandishi wa habari la kuwajengea uelewa kuhusiana na tamasha hilo.
Monica ndani ya siku hizo, mambo mbalimbali yataangaziwa ikiwemo harakati za mwanamke nchini kwa miaka 30 iliyopita.
“Pia tutaangazia changamoto za kufikia usawa na namna ya kuzifikia na kutengeneza dira ya kutupeleka miaka mingine 30 ili kuondoa kabisa hali ya kutokuwa na usawa wa kijinsia nchini,” amesema Monica.
Akizungumzia tamasha hilo, Herriet Kabende ambaye ni mmoja wa wahudhuriaji tangu mwaka 1997 amesema limempa wa kufuatilia vitu mbalimbali ikiwemo bajeti kwa mtazamo wa kijinsia, kufuatilia kero mbalimbali kuanzia mtaani kwake pamoja na kuibua mijadala inayolenga kutatua changamoto za wanawake na watoto.
“Kwa muda wote niwemeweza kujifunza kuwa harakati zinaanzia kwako mwenyewe, kwa kulifutailia jambo fulani na kulifikisha hadi ngazi za juu kuona linatafutiwa ufumbuzi,” amesema Herriet.
Naye Hussein Wamarwa naye amesema bado kuna uelewa mdogo kwa wanaume juu ya mtandao wa kijinsia kwani wanaona kama ni kwa ajili ya wanawake jambo ambalo sio sahihi.
“Mimi kwa miaka 13 nimekuwa nikishiriki shughuli mbalimbali zinazofanywa na mtandao huu mpaka nimepewa jina la ‘mwanaume mwenye moyo wa mwanamke’ hivyo kuwa chachu ya makundi mbalimbali,” amesema Wamarwa.