Waziri Gwajima alia na mila ya kuwekeza mke tumboni

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk Dorothy Gwajima.
Muktasari:
- Sakata la mila ya kuwekeza mke akiwa tumboni katika mikoa ya Arusha na Manyara limeibuka bungeni huku Waziri Gwajima akilaani na kusema mila hiyo ni kandamizi.
Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mary Mwinyi amehoji Serikali ina mpango gani wa kufuatilia mila potofu za kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama hasa Manyara na Arusha.
Mbunge huyo ameuliza swali hilo leo Alhamisi Agosti 31, 2023 na kujibiwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk Dorothy Gwajima.
Akijibu swali hilo, Dk Gwajima amesema Serikali inatambua kuna mila zenye faida ambazo zinapaswa kuendelezwa na mila zenye kuleta madhara ikiwemo mila ya kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama.
“Mila hii ina madhara kwa kuwa inachochea ukatili wa kihisia, ndoa za utotoni na ina mnyima mhusika haki yake ya msingi ya kumchagua mwenza wa kuishi naye umri utakapofika,”amesema.
Amesema katika kutokomeza mila za aina hiyo, Serikali imeandaa utaratibu wa kuendesha majadiliano kwa kuwa masuala ya kimila yanahitaji umakini mkubwa katika kuyajadili.
Amesema wizara imeandaa mwongozo wa kuendesha majadiliano unaojulikana kama mwongozo wa Taifa wa uendeshaji majadiliano kuhusiana na mila na desturi zenye madhara kwa jamii wa mwaka 2022.
“Majadiliano hayo yanakuwa ni jumuishi yanayohusisha viongozi wa mila, viongozi wa dini, wazee maarufu na wataalamu waliopo katika ngazi ya jamii ili kuja na ujumbe mahususi wenye lengo la kutokomeza mila zenye madhara ikiwa pamoja na kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama,”amesema.
Ametoa wito kwa wataalamu wa maendeleo na ustawi wa jamii waliopo ngazi za jamii kuandaa majukwaa ya kuongoza majadiliano kuhusu mila hiyo yenye madhara ya kuwekeza mke akiwa tumboni.
Pia amewaagiza kuja na jumbe mahsusi ili kutumika kwenye majukwaa tofauti kutoa elimu ikiwa pamoja na nyumba za ibada.
Aidha, amesema kupitia radio za kijamii zilizopo mikoa ya Manyara na Arusha, jumbe hizo zitawanywe ili kuendelea kuelimisha jamii.