Bodaboda kizimbani akidaiwa kumuua mwanaye

Picha ya Mtoto Timotheo Joseph (6) enzi za uhai wake.
Muktasari:
- Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa la mauaji ya kukusudia Aprili 11, 2025 katika Mtaa wa Lukosi, Kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa.
Iringa. Dereva wa bodaboda, Joseph Muhulila amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa akishtakiwa kwa mauaji ya kukusudia kwa kumkatakata mwanaye wa kumzaa, Timotheo Muhulila (6).
Muhulila (28) anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 11, 2025 katika Mtaa wa Lukosi, Kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa.
Mshtakiwa amefikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo leo Mei 14, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Rehema Mayagilo.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Radhia Njovu amemsomea mashtaka akidai ametenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Baada ya kusomewa mashtaka mshtakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi ya mauaji isipokuwa Mahakama Kuu.
Kwa mujibu wa sheria, kosa la mauaji halina dhamana, hivyo mshtakiwa amepelekwa rumande. Kesi itatajwa Mei 28, 2025.
Awali, taarifa kwa umma iliyotolewa na Polisi Mkoa wa Iringa ilieleza linamshikilia Muhulila kwa tuhuma za kumuua mtoto wake Timotheo kisha kuukatakata mwili wake vipande na kuvitupa ndani ya tundu la choo, kwa lengo la kuficha ushahidi.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi ilieleza polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji walibomoa choo na kuopoa vipande vya mwili wa mtoto huyo.