Mbaroni akituhumiwa kumuua mtoto wake

Picha ya Mtoto Timotheo Joseph (6) enzi za uhai wake.
Muktasari:
- Diwani apigwa bumbuwazi, adai katika kata yake hilo ni tukio la tatu kutokea huku akiomba vyombo vya usalama kufanyia kazi mauaji hayo.
Iringa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linamshikilia Joseph Mhilila (28), mkazi wa Mtaa wa Lukosi, Kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa, kwa tuhuma za kumuua mtoto wake Timotheo Joseph mwenye umri wa miaka sita na kisha kuukatakata mwili wake vipande vidogovidogo alivyovitupa ndani ya tundu la choo kwa lengo la kuficha ushahidi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi baada ya tukio hilo la kusikitisha, Polisi wakishirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji walifika nyumbani kwa mtuhumiwa, walibomoa choo na kufanikiwa kuopoa vipande vya mwili wa mtoto huyo.
Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu leo Jumatano Mei 7, 2025, Diwani wa Kata ya Mtwivila, Aldo Gwegime ameelezea kusikitishwa na tukio hilo la kikatili, akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua kali na za haraka kuzuia matukio ya aina hiyo kuendelea kutokea katika jamii.
“Tukio hili ni la tatu kutokea, la kwanza lilihusisha bibi mwenye umri wa miaka 90 kuuawa na binti yake wa miaka 52 na sasa hili la baba amemuua mtoto wake wa miaka sita kwa kumkatakata. Matukio haya ni ya kusikitisha sana na hayakubaliki katika jamii,” amesema Gwegime.
Amelitaja pia tukio lingine la kusikitisha la baba kumlawiti binti yake mwenye umri wa miaka minne, akisisitiza kuwa vitendo hivyo ni vya kinyama na vinapaswa kulaaniwa vikali.
“Mtoto wa miaka sita hana hatia yoyote na kitendo cha mzazi wake kufanya ukatili wa namna hiyo kinapaswa kushughulikiwa kwa hatua kali za kisheria,” amesema.
Gwegime amesema tukio hilo limewaacha wananchi wa eneo hilo wakiwa na hofu kubwa, huku akiitaka jamii kushirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii.
“Ni jukumu letu sote kuhakikisha jamii yetu inakuwa salama. Watoto na wazee wanapaswa kulindwa dhidi ya vitendo vya kikatili,” amesema diwani huyo, akihimiza pia utoaji wa taarifa mapema kwa vyombo husika.
Kwa upande wake, Mariam Mkwawa, jirani wa familia hiyo, amesema wameshangazwa na tukio hilo kwa kuwa Mhilila (mtuhumiwa) ni kijana anayejiheshimu, mpole na mwenye mawasiliano mazuri na watu wote wa mtaa huo.
“Hakuwahi kuonyesha tabia za ukatili. Tumebaki midomo wazi kwa jinsi tukio hili lilivyotokea,” amesema Mariam.
Naye mtaalamu wa masuala ya kijamii, Grace Mlowe amesema kuna ongezeko la matukio ya ukatili katika jamii, akisisitiza umuhimu wa kuanzisha kampeni maalumu za uelimishaji kuhusu madhara ya ukatili na wa kulinda haki za watoto.