Prime
Ugomvi, kujichukulia sheria mkononi kulivyopoka uhai wa watu 2024

Muktasari:
- Watu 2,263 walipoteza maisha mwaka 2024 kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni sawa na watu 6 kila siku, huku ugomvi, kujichukulia sheria mkononi, wivu na ugoni vikichukua nafasi. Imani za kishirikisha zachangia matukio mengi, Kagera kinara.
Dar es Salaam. Watu sita waliuawa kila siku mwaka jana ugomvi ukitajwa kuwa sababu namba moja iliyochangia vifo hivyo, ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) 2024, inaeleza.
Ripoti hii ya Jeshi la Polisi inayozungumzia hali ya uhalifu Tanzania kwa mwaka 2024, inabainisha kuwa jumla ya watu 2,263 walifariki dunia mwaka 2024 katika matukio 2,193 yasiyo ya kawaida.
Katika vifo hivyo, wanaume waliouawa walikuwa 1,682 ambapo ni sawa na asilimia 74.3 ya wote waliouawa mwaka 2024, wanawake wakiwa 582 (asilimia 26.7).
Kwa mujibu wa polisi, mabadiliko ya kukua kwa teknolojia na maendeleo ya nchi vimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa matukio ya uhalifu nchini.
Katika orodha hiyo ugomvi ulibeba vifo 658 ambao ulibeba wa majumbani uliosababisha vifo 454 na vilabuni 204.
Watu kujichukulia sheria mkononi kulisababisha vifo 405, wivu na ugoni vifo 277, visasi (84) huku vifo vya bahati mbaya vikiwa 25.
Migogoro ya ardhi ilisababisha vifo 47, kubaka (21), vichaa (18), kuwania mali (71), imani za kishirikina (168) na sababu nyingine (489).
Waliouawa kwa imani za ishirikiana vikongwe walikuwa 138, mtu mwenye ualbino mmoja na wengineo walikuwa 29.
Migogoro ya ardhi nayo ilikuwa sababu ya matukio yanayoripotiwa kusababisha vifo, yakiwemo ya wakulima na wafugaji, wakulima kwa wakulima, wananchi na wawekezaji/Serikali au mwananchi kwa mwananchi.
Hali hii ilisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali katika jamii na katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, jumla ya migogoro ya ardhi 199 iliripotiwa na vifo vilivyotokana nayo ni 47, majeruhi 70 na uharibifu wa mali yakiwemo mashamba 15 na madhara kwa mifugo 19.
Mikoa inayoongoza
Kwa mujibu wa takwimu hizo, makosa mengi ya mauaji yalitokea mkoa wa Kagera ambao uliongozi kwa vifo 182, Dodoma (151), Singida (106), Mbeya (99) na Mwanza (99).
Mikoa ambayo ilirekodi idadi ndogo ya matukio haya ni Ilala iliyokuwa na matukio 21, Rufiji matukio 26, Simiyu 32, Mtwara 39 na Lindi matukio 41.
Mikakati polisi
Katika kukabiliana na matukio ya mauaji, Jeshi la Polisi limedhamiria kuendelea kuelimisha jamii kuachana na vitendo vya kishirikina vya mauaji ya watoto, wazee na wenye ualbino.
Pia limedhamiria kutoa elimu kwa umma kwa njia mbalimbali ili jamii ibadilike na kuacha kujichukulia sheria mkononi, na kuhamasisha jamii ili ijihusishe na shughuli zilizo halali katika kujipatia kipato.
“Pia Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutafuta ufumbuzi wa migogoro katika jamii, kushirikisha taasisi za kidini katika kuhamasisha jamii ili kuachana na imani potofu za kishirikina,” imesema taarifa hiyo.
Pia limesema litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kwa madhumuni ya kuimarisha utoaji wa elimu rika kwa vijana, ili waweze kuzikabili changamoto za mahusiano ya kijinsia, kuhamasisha jamii kuwatumia wataalamu wa ushauri nasaha pindi wanapopatwa na changamoto za afya ya akili na migogoro mbalimbali katika jamii.
Elimu nasihi muhimu
Salma Mashaka, mkazi wa Kijichi jijini Dar es Salaam, amesema ili kukabiliana na hali hiyo ni vyema elimu ya unasihi na namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo ikawa ni kitu kinachotolewa wakati wote katika jamii, ili watu wajue kukabiliana na hasira zao.
“Watu wawe wanajua kufanya hivi ni kosa na kuwa kabla sijafanya natakiwa kujizuia vipi, bila hivyo tutakuwa tukihangaika na matokeo badala ya kuzuia vyanzo vya tatizo,” anasema.
Akizungumzia suala hilo, Wakili Dominic Ndunguru amesema ili kujua namna ya kumaliza hali hii ni vyema ukafanyika utafiti ambao utakuja na suluhisho la kudumu la muda mfupi au mrefu.
Hiyo ni kutokana na kuwapo kwa sababu mbalimbali ambazo zinatajwa kuwa chanzo cha mauaji hayo ambazo zinahitaji uchambuzi wa kina kujua suluhisho lake.
“Lakini huenda matukio haya yanaonekana zaidi sasa kunatokana na kuongezeka kwa vyombo vya habari ambavyo vinafanya matukio yaliyokuwa yakifanyika bila kusikika, sasa kuwekwa wazi,” amesema.
Amesema moja ya sababu inayoweza kuchangia hali hii ni kuwapo kwa uwezeshaji wanawake katika upande wa masuala ya jinsia, hali hii imefanya baadhi yao kuacha kusikiliza waume zao.
“Hili linaweza kuwafanya wanaume kutumia nguvu kuonyesha mamlaka yao, matokeo yake wanaweza kufanya kitu ambacho kinaweza kuleta mtafaruku kama hiki,” anasema.
Amesema jambo hili limefanya watoto wengi wa kiume kubaki nyuma, ikiwemo katika suala la elimu, kwani wasichana wamekuwa wakifuatiliwa zaidi kuliko wao, jambo ambalo linawafanya kuhisi kutengwa.
“Pia katika uchumi, wakati mwingine mwanamke akimzidi mumewe kipato anaweza kutumia vibaya nafasi aliyonayo na kuanza kumuona yuko chini. Nadharia hizi zote zikifanyiwa tafiti vizuri tunaweza kupata majibu kamili,” amesema.
Mtaalamu wa saikolojia, Charles Kalungu amesema ripoti ya polisi inasema ukweli kwani katika jamii kuna migogoro mingi ya kifamilia kwa kuwa wenza hawasikilizani, hali inayotengeneza usugu na baadaye huleta madhara makubwa.
Amesema watu wanapokosa upendo huwafanya wanapokuwa na kitu cha kuzungumza kukosa wa kumsikiliza, hivyo wakati mwingine huweza kulazimika kutumia nguvu ili wasikilizwe.
“Lakini kuna wengine furaha yao inaweza kuwa ni kuumiza wengine, hawana huruma na kujali watu wengine,” anasema Kalungu.
Pia amesema mfadhaiko kwa mtu unaweza kufanya watu kufanyiana ubaya, mfano baba kufanya kitu kibaya kwa mke bila kujali madhara yatakayotokea kwa watoto au kufanya kitu kibaya kwa watoto bila kujali jamii itawachukuliaje.
“Kinachopaswa kufanyika kukomesha hali hii ni kutolewa elimu ya mahusiano na malezi kwa watu. Wengi wanaingia katika mahusiano bila kuwa na elimu akipata utofauti wa kihisia wanakuwa hawaelewi, uelewa wa elimu ya mahusiano unahitajika zaidi kwani hata ndoa zinazovunjika zinaongezeka na bora wapeane talaka kuliko kuuana,” anasema.