Bei ya pedi mitaani yaendelea kuwatesa wanawake, wasichana

Muktasari:
Bei ya bidhaa hizo imebaki kama ilivyokuwa zamani kwa bei ya jumla na rejareja.
Dar es Salaam. Licha ya Bunge kupitisha msamaha wa kodi kwenye taulo za kike maarufu pedi, Juni 14, bado bei ya bidhaa hizo ipo juu.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa bei ya bidhaa hizo imebaki kama ilivyokuwa zamani kwa bei ya jumla na rejareja.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango alitangaza msamaha wa kodi hiyo bungeni wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2018/19.
Alisema kuondolewa kwa kodi hiyo kutawapunguzia mzigo wa ununuzi wa bidhaa hiyo watoto wa kike na wanawake.
Hata hivyo, ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu msamaha huo uanze kufanya kazi Julai Mosi, wanawake na wasichana wanasema bado bei ni kubwa.
Marion Kaguo, muuza vyakula jijini Dar es Salaam anasema bado ananunua bidhaa hiyo kwa kati ya Sh2,500 hadi 3,500 kama zamani.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Neema Stanford anasema amekata tamaa kwa kuona bado bei ipo palepale licha ya Serikali kutangaza msamaha huo.
“Unafuu wa bei ulipaswa uje mapema ukizingatia kuwa kuna wanafunzi wanaokosa masomo wakati wanapokuwa kwenye siku zao za hedhi hasa wa vijijini,” anasema.
Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Fedha na Mipango, Ben Mwaipaja ameliambia Mwananchi kuwa ni mapema mno kuifanyia tathmini bei hiyo kwa kuwa msamaha wa kodi umeanza mwezi uliopita.
“Serikali inaamini kuwa wapo wafanyabiashara ambao bidhaa zao ziliingizwa nchini kabla ya pendekezo hilo kupitishwa na huenda ndio sababu bei bado imebaki kama ilivyo,” alisema.
“Tunategemea kuwa bei itashuka kutokana na hali ya soko na ushindani baina ya wafanyabiashara walioingiza bidhaa kabla ya msamaha wa kodi na wale walioingiza baada ya msamaha.”
Mwaipaja aliongeza kuwa ni vyema wafanyabiashara wakapungzua bei ya bidhaa hiyo na kutengeneza mfumo utakaohakikisha kwamba hawautumii msamaha huo kwa manufaa yao.
Utafiti wa Mwananchi umebaini kuwa msichana au mwanamke mmoja anaweza kutumia zaidi ya Sh67,000 pamoja na kodi kwa mwaka kwa kununua taulo hizo. Hesabu hii inatokana na wastani wa mwanamke mmoja kutumia pakiti mbili za taulo kwa mwezi zinazouzwa Sh2,800.