Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kissu Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu

Shaaban Kissu.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Shaaban Kissu kuwa naibu mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais, Ikulu, uteuzi unaotazamwa kama hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa mawasiliano baina ya Serikali na wananchi.

Taarifa kuhusu uteuzi huo imetolewa leo Jumatano ya Mei 7, 2025 na Katibu wa Rais, Waziri Salum, katika hafla ya chakula cha mchana iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo ilikuwa maalumu kwa wanahabari waliopewa tuzo katika mashindano ya Samia Kalamu Awards, tuzo zinazotolewa kwa waandishi waliofanya kazi bora za kiuandishi zinazochochea maendeleo.

Shaaban Kissu, ambaye alikuwa mshereheshaji wa hafla hiyo, alionekana kushangazwa na tangazo hilo ambalo lilitolewa mbele ya hadhira ya wageni mashuhuri na wanahabari kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

"Hii taarifa nafikiri ni ‘surprise’ hata kwa Kissu mwenyewe kwa sababu hakuwa na taarifa," alisema Waziri Salum, akiongeza kuwa kuchelewa kwake kufika haflani kulisababishwa na kushughulikia masuala ya uteuzi huo.

Kissu ana historia ndefu na tajiri katika tasnia ya habari na mawasiliano.

Alianza kazi yake kama mtangazaji wa michezo katika Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), ambapo aliibuka kuwa miongoni mwa watangazaji wenye sauti maarufu zilizohusishwa na matangazo ya moja kwa moja ya mechi za soka redioni.

Umahiri wake katika lugha ya Kiswahili, upangaji wa hoja na ushawishi wa kisauti ulimpa umaarufu mkubwa ndani na nje ya vyombo vya habari.

Baadaye, alipata nafasi ya kufanya kazi na Televisheni ya Taifa (TVT), na baadaye Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), ambapo aliendelea kuonyesha umahiri kama mtangazaji wa runinga.

Uzoefu huu wa miongo kadhaa ulimwezesha kujijengea hadhi kama mmoja wa wataalamu wanaoheshimika katika sekta ya mawasiliano nchini.

Mbali na taaluma ya uandishi na utangazaji, Shaaban Kissu pia aliwahi kuhudumu katika nafasi ya uongozi wa kisiasa.

Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, nafasi aliyoitumikia kwa weledi kabla ya kurejea katika sekta ya habari, ambapo alikuwa Mkurugenzi wa Africa Media Group hadi uteuzi huu mpya.

Uteuzi wa Kissu unakuja wakati Serikali ya Rais Samia inazidi kuimarisha mifumo ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kwa uwazi, haraka na kwa lugha sahihi.

Kissu anatazamwa kama chaguo sahihi kutokana na uelewa wake wa vyombo vya habari, mawasiliano ya kisiasa, na uhusiano na jamii.