Prime
Mfahamu bosi mpya wa Tanesco, kibarua kinachomsubiri

Muktasari:
- Lazaro Twage kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) amewahi kuhudumu katika nafasi mbalimbali, ikiwemo naibu mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).
Dar es Salaam. Huenda watu wengi wanahoji iwapo Lazaro Twange anaweza kumudu nafasi aliyopewa ya mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Hiyo ni kutokana na wengi kumfahamu baada ya kuhudumu kama mkuu wa wilaya mbalimbali ikiwemo Babati, Mkoa wa Manyara alipoanzia kabla ya kuhamishiwa Hai, Mkoa wa Kilimanjaro na baadaye Ubungo, Dar es Salaam, ambapo uteuzi huu umemkuta akihudumu.
Lakini ukweli ni kwamba Twange anao uzoefu wa kuhudumu katika nafasi za juu kwani amewahi kuwa naibu mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) anayesimamia operesheni kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo mwaka 2017.
Baada ya kutolewa katika nafasi hiyo, aliyekuwa Rais wakati huo, hayati John Magufuli alimteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati Julai 3, 2020 na alihudumu kwenye wilaya hiyo hadi Septemba 02, 2024 alipohamishiwa Wilaya ya Hai.
Baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo kwa siku 1,522, Twange alihamishiwa Wilaya ya Ubungo Januari 24, 2025 ambapo amehudumu kwa siku 102 kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco.

Twange anachukua nafasi ya kuliongoza shirika hilo akiziba pengo lililoachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa akihudumu kwenye nafasi hiyo, Gissima Nyamo-Hanga aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Aprili 13, 2025 katika ajali ya gari iliyotokea Bunda, mkoani Mara.
Madiwani wamzungumzia
Licha ya kuhudumu kwa siku 102 pekee katika Wilaya ya Ubungo, watu waliopata nafasi ya kufanya naye kazi wameeleza namna uteuzi huu ulivyowaachia pengo.
Diwani wa Makurumla, Bakari Kimwanga amesema kati ya wakuu wa wilaya watano ambao wamewahi kufanya nao kazi Twange ni bora kuwahi kutokea.
Hiyo ni kutokana na aina yake ya utendaji unaojali muda, kuchukia uzembe na kutaka mambo mengi kufanyika eneo la tukio badala ya ofisini.
“Kwenye muda alikuwa anajali sana, kama ni suala la saa 3 asubuhi yeye saa 2:30 anakuwa ameshafika, alijali sana muda. Uteuzi ni suala tu ambalo hatuwezi kulizuia lakini tumeumia kuondoka kwake. Nina imani huko anakokwenda watu watafaidi utendaji wake bora,” amesema.
Amesema katika yote aliyofanya, Twange alikuwa mtu anayeweza kuunganisha, kusimamia na kufuatilia hadi kuhakikisha jambo kusudiwa linakuwa kama lilivyotarajiwa na hakupenda kukaa ofisini, zaidi alikuwa mtu wa ‘field.’
Diwani wa Msigani, Hassan Mwasha amesema watakumbuka aina ya utendaji wake ambao alikuwa hapendi kutumia mamlaka aliyonayo kuwawajibisha watu wengine na badala yake aliamini katika mazungumzo.
“Alikuwa hapendi kusikiliza maneno ya kuambiwa, alikuwa ni mkuu wa wilaya bora kuwahi kutokea, hapendi mtu amseme mwingine na hata ikitokea baadhi ya viongozi wanamshambulia mtendaji wake, hapendi,” amesema Mwasha.
Mbali na kuwa mtendaji mzuri pia aliweza kuishi na watu vizuri, hata ilipotokea malalamiko aliwataka watumishi wake kwenda kusikiliza wananchi kabla ya yeye kufika kupewa kero zao, jambo ambalo linaweza kumfanya asiwaseme mbele yao.
“Aliamini kumsema mtumishi wake mbele ya wananchi itaondoa imani yao kwa jamii wanayoitumikia, hakutaka hilo,” amesema Mwasha.
Kibarua kinachomsubiri
Umeme wa uhakika ndio kubwa ambalo wananchi wanalihitaji ili shughuli zoa za kiuchumi ziweze kufanyika bila kikwazo.
Bila kujali hali iliyopo ikiwemo ya hewa, wananchi wanataka ziwepo taarifa sahihi endapo kutakuwa na kukatika kwa umeme ili wajue namna ya kujiandaa.
Hoja ya kukatikakatika kwa umeme ilikuwa ni moja ya mijadala iliyotawala bajeti ya Wizara ya Nishati 2025/26 iliyowasilishwa bungeni Aprili 28 na 29, 2025.
Wabunge waliibua hoja hiyo pamoja na fidia kwa wanaopisha miradi ya umeme na fedha za CSR za bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP).
Wabunge hao walitaka suala hilo liangaliwe kwa upekee kwani kitendo cha kukatika mara kwa mara, kinarudisha nyuma maendeleo ya jamii na Taifa na kusababisha hasara kwa wananchi na wafanyabiashara.
Mathalani, Mbunge wa Kiteto (CCM), Edward Ole Lekaita alisema jimboni kwake mkoani Manyara kumekuwa na shida ya kukatika kwa umeme.
“Siyo kukatika tu, ni kukatika kwa muda mrefu kunakowaunguzia wananchi vifaa vyao. Ilileta kero kubwa. Niliwahi kumwambia Naibu Waziri (Judith Kapinga – Naibu Waziri wa Nishati) na Mkurugenzi wa REA (Wakala wa Umeme Vijijini) hili jambo,” alisema.
Mbunge wa Nkenge (CCM), Florent Kyombo alisema, ingawa wabunge wengine wamelalamikia suala la umeme kukatika mara kwa mara, Wilaya ya Misenyi, mkoani Kagera hukumbwa na tatizo hilo zaidi kutokana na mvua nyingi.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akihitimisha hoja yake alisema amepokea maoni na ushauri wa wabunge juu ya suala hilo la umeme kukatikakatika na wanakwenda kulifanyia kazi.

Hii ina maana Twange hiki ni moja ya kibarua kinachomsubiri kuhakikisha kunakuwapo na umeme wa uhakika kama ambavyo wananchi waliozungumza na wananchi wanavyotamani iwe.
“Siyo kukata bila taarifa, tujue ukatika lini kwa muda gani na kwa sababu gani. Akiweza kusimamia suala la utoaji ratiba hata kelele hatozisikia lakini haimaanishi ndiyo wakate kila wakati,” amesema Sheila Juma mkazi wa Kijichi.
Aziza Ibrahim yeye anamtaka kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaimarika ikiwemo uunganishwaji wa umeme, huduma kwa wateja na kushughulikia matatizo yanayowalishwa.
“Nafikiri anatakiwa kukitupia jicho kituo cha huduma kwa wateja ili kiweze kuleta ufanisi, kikifanya vizuri shirika zima litafanya vizuri kwa sababu kuna baadhi ya taarifa zinatolewa lakini zinachelewa kufanyiwa kazi inatukwaza sana wateja,” amesema Aziba mkazi wa Temeke.
Maneno ya wananchi hawa yaliungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), Dk Donald Mmari ambaye amesema jukumu kubwa lililopo mbele ya Twange ni kuhakikisha umeme wa uhakika na nafuu unakuwepo nchini.
Hiyo ni kutokana shughuli nyingi nchini ikiwemo uzalishaji viwandani kuhitaji umeme wa uhakika, ili waweze kuzalisha bidhaa zinazoweza kushindana sokoni.
“Viwanda vinataka umeme, wazalishaji wa mazao hasa bidhaa zinazoharibika wanataka uhakika umeme ili waweze kutunza mazao yao, watoa huduma mbalimbali wanataka umeme,” amesema Mmari na kuongeza.
“Uchukuzi sasa hivi tuna treni ya umeme nao wanataka umeme wa uhakika, kila kitu kinahitaji umeme wa uhakika na gharama nafuu hivyo hili ni jukumu kubwa lililo mbele yake,” amesema Dk Mmari.