Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Safari ya Nyamo-Hanga ilivyohitimishwa Bunda

Muktasari:

  • Mtoto wa Nyamo-Hanga aeleza baba yao alivyokuwa na mapenzi na ndugu na jamaa zake hadi kufikia kuwajengea nyumba na wengine kuwapa mitaji kwa ajili ya kufanya biashara

Bunda. Majonzi yametawala miongoni mwa viongozi wa umma, binafsi, wafanyakazi, familia, ndugu jamaa na marafiki waliokusanyika mjini Bunda, mkoani Mara katika

maziko ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamo-Hanga.

Maziko yamefanyika leo Jumatano, Aprili 16, 2025, eneo la Migungani mjini Bunda, waombolezaji wakiongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.

Kwa nyakati tofauti waombolezaji wakiwamo wanafamilia walishindwa kujizuia, hivyo kuangua vilio, akiwamo Dk Biteko aliyekuwa na wakati mgumu alipomzungumzia Nyamo-Hanga.

Jeneza lililobeba mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Gissima Nyamo-Hanga likiimgizwa eneo la ibada tayari kwa ibada ya mazishi. Picha na Beldina Nyakeke

Baada ya ibada iliyoongozwa na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya mkoani Mara, John Maguge jeneza lenye mwili wa Nyamo-Hanga lilibebwa na wakurugenzi wa idara mbambali kutoka Tanesco kuelekea eneo lilipokuwa kaburi, mita chache kutoka jukwaa kuu.

Viongozi wachache wakiongozwa na Dk Biteko, ndugu zake na watoto wa marehemu, ndio walikwenda lilipokuwa kaburi, waombolezaji wengine walifuatilia kilichoendelea kupitia runinga zilizofungwa eneo hilo.

Ulikuwa wakati wa majonzi wakati mwili ukishushwa kaburini kwa kutumia kifaa maalumu, huku waombolezaji waliokuwa eneo hilo wakipunga mkono wa kwaheri ikiwa ishara ya kumuaga Nyamo-Hanga.

Dk Biteko aliongoza uwekaji udongo, shughuli iliyohitimishwa na familia ya marehemu ikitanguliwa na wajane wawili, baadhi ya ndugu wakishindwa kuhimili, hivyo msaada ulihitajika.

Jeneza lililobeba mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco likiwa eneo la ibada ya mazishi. Picha na Beldina Nyakeke




Kama ilivyo ada, shughuli za maziko zilihitimishwa kwa kuweka mashada ya maua juu ya kaburi.


Upendo kwa familia

Bernard Gissima, mtoto wa kwanza wa kiume wa Nyamo-Hanga akisoma wasifu wa baba yake amesema alioa wanawake watatu lakini hadi umauti unamfika ameacha wajane wawili.

"Gissima Nyamo-Hanga ameacha wajane wawili, watoto 15 wa kiume sita na wa kike tisa, pamoja na wajukuu watano wa kiume wanne na wa kike mmoja," amesema.

Bernard amesema enzi za uhai wake, baba yao alikuwa nguzo kuu ya familia na ukoo kwa jumla, alikuwa na mapenzi na ndugu na jamaa zake hadi kufikia kuwajengea nyumba na wengine kupewa mitaji kwa ajili ya kufanya biashara.

Askofu Maguge akizungumzia ushiriki wa kanisa licha ya Nyamo-Hanga kuwa na wake wawili kinyume cha sheria na taratibu za kanisa amesema:

"Tumefuatilia huko alikokuwa akisali tukajiridhisha baadaye marehemu alishiriki sakramenti maalumu, hivyo kuruhusiwa kuendelea kuwa muumini ndiyo maana na sisi leo tuko hapa kwa ajili ya kuendesha misa hii. Nimelazimika kutoa ufafanuzi huu ili kuondoa sintofahamu." 

Askofu Maguge ameitaka familia ya Nyamo-Hanga kushikamana wakati huu mgumu kwa maelezo kuwa, shetani hutumia kifo kuleta migogoro katika familia.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati (katikati) pamoja na viongozi wengine wakiwa kwenye ibadabya mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Gissima Nyamo-Hanga. Picha na Beldina Nyakeke

"Biblia inatuambia tushukuru kwa kila jambo hata liwe gumu kiasi gani, pale unapofikiri hakuna Mungu basi yeye anakuwapo, hivyo tunapaswa kumuita na kumtegemea," amesema.


Makofi msibani

Baadhi ya watumishi wa Tanesco walipiga makofi mara kwa mara, hasa Dk Biteko alipoeleza namna Nyamo-Hanga alivyoishi na kufanya kazi na watumishi wa shirika hilo.

"Ni kweli hakuna kipindi wafanyakazi wa Tanesco wamefanyakazi kwa kujiamiani na katika mazingira rafiki kama kipindi cha uongozi wa Nyamo-Hanga, hata kama ulikuwa umekosea alikuwa na namna ya kukosoa na kukuelekeza," amesema mmoja wa watumishi ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Amesema awali walikuwa wakifanyakazi kwa wasiwasi, kukiwa na hofu ya kufukuzwa kazi, huku masilahi yao hayapewi kipaumbele.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Biteko alipotoa salamu akimzungumzia Nyamo-Hanga alijikuta akitokwa machozi akikatiza hotuba mara kadhaa. Alimuelezea Nyamo-Hanga kwamba alikuwa mchapakazi.

"Gissima was a man... alikuwa mtu anayekuja mbele yangu kwa unyenyekevu licha ya kuwa alikuwa mkubwa kuliko mimi," amesema na kueleza aliiongoza Tanesco kwa ufanisi na viwango vya hali ya juu kiasi cha kusababisha wengi kuridhika na hali ya shirika hilo kwa sasa.

Amesema licha ya kuteuliwa kuongoza Tanesco ikiwa katika hali mbaya, aliwaongoza wafanyakazi na kuwafanya kuwa wamoja bila kumbagua yeyote hivyo kulifanya kuwa shirika bora.

"Alibeba lawama kwa niaba ya wafanyakazi wake pale wanapofanya makosa, alitaka kila mmoja awe na furaha mahali pa kazi na hata kama alitaka kumuadhibu mtu lazima angekueleza kosa lako, badala ya kukasirika kuhusu adhabu yako basi utafurahia adhabu," amesema.

Amesema baada ya Nyamo-Hanga kuteuliwa kushika wadhifa huo, Rais Samia Suluhu Hassan alimweleza (Dk Biteko) kuwa amemteulia mtu anayejua sekta ya nishati vizuri, asiyekuwa msemaji bali mtu wa vitendo na msikivu zaidi, mambo aliyoyabaini kuwa ya kweli baada ya kufanya naye kazi.

Baadhi ya waombolezaji wakiwa kwenye ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Gissima Nyamo-Hanga.  Picha na Beldina Nyakeke

Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Rhimo Nyansaho amesema Nyamo-Hanga alifariki dunia akiwa njiani kuelekea wilayani Butiama mkoani Mara kutatua changamoto ya umeme katika shule ya mfano ya amali inayojengwa wilayani humo.

Nyansaho amesema Nyamo-Hanga alimuaga baada ya kikao cha kamati ya bodi ya Tanesco kilichoketi jijini Dodoma Aprili 12, 2025 ambacho ajenda kuu ilikuwa namna ya kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa Tanesco.

"Aliniambia mwenyekiti nitakwenda Butiama kuna changamoto ya umeme kwenye shule ya mfano inayojengwa pale, nikimaliza nitapitia kwenye shamba langu nililonunua huko Mara ambalo natarajia kufanya makazi yangu baada ya kustaafu," amesema.

Ili kuhakikisha uamuzi na maelekezo ya kikao cha kamati ya bodi yanaanza  kufanyiwa kazi kwa wakati, amesema Nyamo-Hanga alimweleza atamuacha msaidizi wake aanze kuratibu na kuyafanyia kazi.

Amesema hilo lilikuwa tofauti na ilivyokuwa kawaida, kwani mara nyingi yeye na msaidizi wake walikuwa wakisafiri pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumzia changamoto ya umeme katika shule ya mfano ya amali, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amesema aliwasiliana na Nyamo-Hanga awasaidie kuitatua.

"Wiki iliyopita niliwasiliana naye kuhusu umeme kwenye shule yetu ya amali inayojengwa Butiama, alikubali kushugulikia changamoto hiyo kwa haraka na siku zote amekuwa mtu mwenye utayari wa kushughulikia jambo lolote pale nilipowasiliana naye," amesema.

Irene Kowelo, akisoma wasifu wa Nyamo-Hanga  amesema kupitia maisha ya utumishi wake Taifa limepata mafanikio katika nyanja za upatikanaji wa nishati endelevu, uongozi thabiti na maboresho ya taasisi za umma.

Amesema Taifa limepoteza mtu muhimu, kiongozi mwenye maono, mzalendo wa kweli na mtumishi asiyechoka, ambaye alama alizoacha katika taasisi alizozitumikia zitadumu milele.

"Alisimamia kwa ufanisi mabadiliko makubwa katika upatikanaji wa umeme vijijini na mijini, upanuzi wa mitandao ya usambazaji, usimamizi wa miradi mikubwa ya nishati," amesema.

Amesema uongozi wake umewezesha kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya umeme, ukiakisi maadili, haki, uwazi na uwajibikaji.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo amesema Nyamo-Hanga alikuwa mchapakazi na alimsaidia kufanikisha majukumu yake, alipokuwa Waziri wa Nishati na Madini.

Amesema Nyamo-Hanga alikuwa miongoni mwa wataalamu walipendekeza na kuwezesha kushushwa kwa bei ya kuunganishwa umeme kutoka Sh300,000 hadi 27,000 kutokana na weledi na ujuzi wake.

"Aliwezesha Tanzania kuwasilisha sera ya umeme nafuu wa uhakika na unaopatikana kwenye sera za UN hadi kupelekea Obama kuja Tanzania kuzindua mradi wa Power Afrika, " amesema Profesa Muhongo.

Nyamo-Hanga aliyezaliwa Septemba 10, 1969 mkoani Mara, alifariki dunia usiku wa kuamkia Aprili 13, 2025 katika ajali ya gari iliyotokea wilayani Bunda mkoani Mara.

Gari alilopanda liligongana uso kwa uso na lori, dereva alipokuwa akimkwepa mwendesha baiskeli kisha kupoteza mwelekeo na kugongana na lori. Dereva wa Nyamo-Hanga pia alifariki dunia katika ajali hiyo.