Mwili wa Nyamo-Hanga kuzikwa Jumatano Bunda

Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamo-Hanga utazikwa nyumbani kwao Mingungani, Bunda mkoani Mara Jumatano ya Aprili 16, 2025.
Nyamo-Hanga na dereva wake, Muhajiri Haule walifariki dunia saa 7:30 usiku wa kuamkia jana kufuatia ajali ya gari iliyotokea wilayani Bunda mkoani Mara.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, chanzo cha ajali hiyo ni baada ya dereva wa gari hilo aina ya Toyota Landcruser alilokuwemo Nyamo-Hanga , kumkwepa mwendesha baiskeli na kupoteza uelekeo na kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa mbele yao.

Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi iliyotolewa na Tanesco leo Jumatatu na kesho Jumanne, Aprili 15, 2025 ni maombolezo nyumbani kwa marehemu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Nyamo-Hanga aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo Septemba 23, 2023 akichukua nafasi ya Maharage Chande, kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).
Moja ya kibarua kigumu kilichomkabili baada ya kuingia katika nafasi hiyo ilikuwa kushughulikia changamoto za muda mrefu za umeme nchini na alifanikiwa.
Endelea kutufuatilia Mwananchi na mitandao yetu.