Barabara iliyokatika Ulanga yaanza kutengenezwa

Wananchi wakiwemo wasafiri wakiangalia namna barabara ya Ulanga - Malinyi ilivyokatika kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Mei 3 Wilayani humo na kusababisha makaravati yaliyokuwepo eneo hilo kusombwa na maji. Picha Hamida Shariff, Mwananchi
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Khamana Simba, amesema matengenezo ya barabara iliyokatika eneo la Ilagua yameanza rasmi, ingawa hajatoa tarehe ya kukamilika kwa kazi hiyo. Asisitiza kuwa jitihada zinaendelea ili kurudisha mawasiliano kwa wananchi.
Ulanga. Matengenezo ya barabara iliyokatika Mei 3, 2025, katika eneo la Ilagua wilayani Ulanga yameanza kufanywa na wahandisi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad), kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Khamana Simba.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Mei 6, 2025, Simba amesema tangu kukatika kwa barabara hiyo, wasafiri waliokuwa wakielekea Ifakara, Malinyi na maeneo mbalimbali ya Ulanga wamekwama katika kijiji cha Ilagua.
Hata hivyo, amesema juhudi za kukarabati eneo hilo zinaendelea kwa kasi. “Kwa sasa siwezi kusema lini kazi ya matengenezo itakamilika, lakini ninachoweza kusema ni kwamba kazi inaendelea ili kuhakikisha magari na wananchi wanarejea kutumia barabara hii haraka,” amesema Simba.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dastan Kyobya, akizungumza na Mwananchi amesema mvua zinaendelea kunyesha kwa wingi katika maeneo mengi ya wilaya hiyo, hali ambayo imesababisha baadhi ya maeneo ya makazi kuzungukwa na maji.
“Hatuna madhara makubwa ya kutisha, lakini kuna maeneo yaliyomezwa na maji kutokana na jiografia ya wilaya yetu, ambayo ina muonekano wa bakuli,” amesema Kyobya.
Katika Wilaya ya Malinyi, mkuu wa wilaya hiyo, Sebastian Waryuba, amesema kukatika kwa barabara ya Ifakara–Ulanga kumeathiri pia wakazi wa Malinyi, kwa kuwa wanategemea barabara hiyo kusafiri kwenda Ifakara na Ulanga.
“Wilaya hizi tatu, Ifakara, Ulanga na Malinyi zinategemea barabara moja kuu kutoka Ifakara, na kwa sasa wananchi wa Malinyi wamejikuta wapo kisiwani, hawana njia mbadala ya kufika maeneo hayo,” amesema Waryuba.
Amesema kutokana na mvua zinazoendelea, haiwezekani kufanya matengenezo ya kudumu kama kuweka daraja hata la muda katika eneo hilo. Kwa sasa, wananchi wanatumia barabara mbadala inayosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) ambayo imefanyiwa matengenezo ya muda.
“Matumizi ya barabara ya Tarura ni ya muda tu, hali ya hewa haijaruhusu matengenezo makubwa kufanyika kwenye barabara kuu ya Tanroads kwa sasa,” amesema Waryuba.