Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maji yachelewesha uunganishaji wa barabara Malinyi

Muktasari:

  • Leo ikiwa ni siku ya tano tangu kukatika kwa barabara ya Ifakara-Malinyi eneo la Misegese, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba amesema kwa sasa maji bado ni mengi.

Malinyi. Hali imeendelea kuwa tete kutokana na kukatika kwa barabara ya Ifakara-Malinyi na wananchi wanaotegemea barabara hiyo wameanza kulalamikia kupanda kwa gharama za maisha.

Hali hiyo imekuja kufuatia mvua kuharibu barabara hiyo na kukata mawasiliano baina ya pande hizo mbili, hivyo kuongeza gharama za usafiri.

Leo ikiwa ni siku ya tano tangu barabara hiyo iharibike, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba amesema itawalazimu kusubiri maji yapungue, ili kazi ya kuweka karavati na tuta ifanyike kurudisha mawasiliano.

Waryuba amesema licha ya viongozi kutoa maelekezo kazi hiyo ifanyike kwa haraka, inalazimika kusubiri kwa sababu eneo hilo bado lina maji mengi.

"Kwa sasa maji bado ni mengi, hivyo hata ile barabara ya dharura ambayo iko chini ya Tarura haiwezi kupitika kwa gari. Kinachofanyika kwa sasa ni kwamba wataalamu wetu wanaangalia namna ya kuweka karavati na kuinua tuta ili barabara iweze kupitika, wakati tukisubiri apatikane mkandarasi wa kujenga daraja kwenye hii barabara kuu ambayo iko chini ya Tanroads.

“Hata hivyo, maji yamekuwa yakipungua na kuongezeka mara kwa mara kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha," amesema na kuongeza;

“Mvua zitakapokata na maji kupungua, mara moja kazi itaanza kwa sababu tayari wataalamu wote pamoja na vifaa, ikiwemo mitambo, vimeshafika eneo la kazi (site)."

Kwa upande wake, mbunge wa Malinyi, Antipas Mgungusi, amesema mbali na kukatika kwa barabara hiyo, mvua zimesababisha nyumba zaidi ya 40 katika Kijiji cha Luwale na Lugala, Kata ya Igawa, kuzingirwa na maji.

Mgungusi ametahadharisha kuwa kama mvua hizo zitaendelea kwa zaidi ya wiki zijazo, ipo hatari ya kuibuka kwa mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali muhimu.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Hamisi Khatimba amesema uingizaji wa bidhaa mbalimbali wilayani humo kwa sasa umekuwa mgumu, hasa baada ya barabara hiyo kukatika na hivyo kufanya magari makubwa kushindwa kuingia mjini Ifakara.

Mkazi wa Kijiji cha Misegese, Kata ya Malinyi, Rehema Nganyanga amesema kwa sasa wanatumia fedha nyingi kwa nauli ya kutoka Malinyi hadi Ifakara kwa sababu wanalazimika kupanda bodaboda hadi kwenye eneo ambalo mabasi yanaishia.

"Mabasi hayafiki Malinyi. Tukiwa na safari ya kwenda Ifakara au Morogoro mjini, inabidi tukodi bodaboda Sh3,000 hadi 5,000 ili ikutufikishe kwenye eneo ambalo mabasi yanaishia. Kabla ya kufika kwenye eneo la mabasi, inabidi uvuke maji na mtu anayekuvusha inabidi umlipe Sh 2,000, yaani ni changamoto kwetu," amesema Nganyanga.

Amesema kuna maeneo yenye maji mengi, hivyo wanafunzi hasa wenye umri mdogo wamekuwa wakipata tabu kufika shule.

Naye, Veronica Mkana, mkazi wa Kitongoji cha Mchanga ambaye anajishughulisha na biashara ya mama lishe, amesema kutokana na kukatika kwa barabara hiyo kumefanya biashara ya chakula kwao kuwa ngumu kutokana na mabasi ya abiria kutofika katika eneo la standi kubwa ya mjini.

Kwa upande wake, Modestus Lyasa, mkazi wa Kata ya Malinyi, ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Miundombinu kuharakisha matengenezo kwenye eneo hilo ili shughuli zirejee kama kawaida.