Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mvua yakata barabara Malinyi, wananchi wakosa mawasiliano

Muktasari:

  • Tayari wananchi wameanza kuonja machungu ya uharibifu wa miundimbinu hiyo wakihofia bei za vyakula kupanda.

Malinyi. Ni siku ya tatu sasa wananchi wa Malinyi hawana mawasiliano na maeneo mengine ya wilaya kutokana na karavati linalounganisha barabara ya Malinyi na mji wa Ifakara wilayani Kilombero, kusombwa na maji.

Hali hiyo inatokana na mvua kubwa zinazoendelea na kuharibu miundimbinu ya barabara, ambapo kwa siku ya tatu sasa barabara hiyo haipitiki, huku wananchi wakiiomba Serikali kuweka mkazo kwenye ujenzi wake ili kunusuru bei za bidhaa kupanda.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti Alhamisi, Aprili 24, 2025, wananchi hao wamesema tangu karavati la barabara hiyo lisombwe na mvua, wamekuwa wakipitia adha kubwa, huku wanafunzi na wafanyabiashara wakikwama kuendelea na shughuli zao.

Mkazi wa Kijiji cha Misegese katika Kata ya Malinyi, Rehema Nganyanga, amesema barabara hiyo ni muhimu, kwani ndiyo inayowafikisha katika Hospitali ya Lugala inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Amesema wajawazito wanaopatwa na uchungu katika kipindi hiki wamekuwa wakipata shida ya kutembea kwa mguu ama kupanda bodaboda kufuata huduma za kujifungua katika hospitali hiyo.

Naye Veronica Mkana, mkazi wa kitongoji cha Mchanga anayejishughulisha na biashara ya mamalishe, amesema kutokana na kukatika kwa barabara hiyo, kumefanya biashara ya chakula kuwa ngumu kutokana na mabasi ya abiria kutofika eneo la standi kubwa ya mjini.

"Sisi kinamama na baba lishe, wateja wetu wakubwa ni abiria wanaokuja hapa Malinyi kwa shughuli za kibiashara na kilimo. Kwa sasa mabasi hayafiki, hivyo hali za biashara ni mbaya," amesema.

Modestus Lyasa, mkazi wa Malinyi, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati na kuharakisha matengenezo kwenye eneo hilo, ili shughuli zirejee kama kawaida.

"Niwaombe viongozi wangu watujengee daraja la kudumu katika eneo hili badala ya makaravati ambayo kila mwaka yameshindwa kuhimili wingi wa maji na kusababisha adha kubwa kwa wakazi wa Malinyi," amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, akiwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, jana Aprili 24, 2025, wamefika kwenye eneo hilo kwa ajili ya hatua za haraka za kurejesha eneo hilo kwenye hali yake ya kawaida.

Akizungumza na wananchi wa eneo hilo, Ulega amesema tayari Serikali imeshatenga Sh18 bilioni kwa ajili ya kujenga madaraja mawili ya barabara ya Misege kuelekea mjini Malinyi ambako ndiko lilipokatika karavati, pamoja na kutengeneza daraja katika kivuko cha Kikove katika mto Mnyera.

Pia, amesema fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ya Lupiro hadi Malinyi yenye urefu wa kilometa 110 ipo na kinachoendelea kwa sasa ni kukamilisha hatua za kumpata mkandarasi.

Hii ni mara ya pili kwa barabara hiyo kukatika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ambapo, mwaka 2024 ilikatika wakati wa mvua na kusababisha mto Fulua kufurika na kusomba kipande cha barabara hiyo.